Ndugu wasomaji wangu leo ninaanza safari mpya tena ndefu hasa
kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambao kimsingi ni mgumu
sana, kwani rais wetu Profesa Jakaya Kikwete anaondoka na ni lazima
tuchague rais mwingine.
Ugumu mwingine ambao ndiyo mkubwa ni mgongano wa
vizazi katika uchaguzi ujao, kwani uchaguzi ujao utatawaliwa sana na
ajenda ya umri ambalo ni kosa, lakini ajenda yenyewe hasa ni mgongano wa
vizazi, kwani kwa kawaida taifa lolote duniani linaongozwa na kizazi
kila wakati katika maisha ya taifa husika.
Naandika makala haya mara baada ya Krismasi, pia
kabla ya kuvuka mwaka mpya najua mada hii italeta mjadala mkali sana na
mpana, kwani ilishaanza kujadiliwa kupitia hoja ya umri, lakini mimi
nitaijadili kupitia hoja ya kizazi au vizazi yaani generation.
Ukisoma kamusi ya TUKI toleo la tatu generation
maana yake kizazi, three generations maana yake vizazi vitatu (Baba na
wanawe na mjukuu) maana nyingine ni kipindi cha wastani cha umri wa mtu
wa kuoa na kuwa na watoto, rika, watu waliozaliwa wakati mmoja, wa rika
moja.
Katika uhai wa taifa lolote lile duniani ni uamuzi
wa taifa lenyewe kuamua kuongozwa na kizazi gani kila wakati, kwani
taifa lazima lizijue changamoto zake linazokabiliana nazo kila wakati
ili liweze kujua kwamba kutokana na changamoto zinazolikabili taifa
ndizo zinasaidia taifa husika kujua na kufanya uamuzi sahihi na wa
busara kwamba waongozwe na kizazi gani katika taifa husika katika jamii
yao.
Mwanafalsafa na Mwandishi maarufu wa vitabu ndugu
Frantz Omar Fanon ambaye alizaliwa mwaka 1925 aliandika kwenye kitabu
chake cha the wretched of the earth kuwa “kila kizazi lazima kigundue
utume wake, ni jukumu lake kuutimiza au kuusaliti utume huo”.
Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais wa pili wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania aliwahi kusema “kila kizazi na kitabu chake”.
Viongozi wote hawa wawili wanachosema ni kwamba kila kizazi kina mambo
yake na majukumu ya wakati wake ambayo yanaweza kutekelezwa vyema zaidi
na uongozi wa wakati wa kizazi husika.
Kwa mujibu wa Biblia Yoeli 2:28 na Matendo ya
mitume 2:17 Wazee wanatakiwa kuota ndoto na vijana wanatakiwa kutabiri
na kuona maono. Vijana na wana hao Mungu anawaona kama wanaona mbele
zaidi wakati wazee wanaota ndoto kuwakumbusha vijana yalitokea kuelezea
uzoefu wao wa nyuma na kuwashauri vijana nini kifanyike.
Kwa kifupi wazee ni washauri na vijana ndiyo
watendaji maana mahali pengine Biblia inawataja vijana kama wenye nguvu
kuweza kukimbia kimbia na kukabili changamoto za wakati huku
wakisikiliza ushauri wa wazee wao ambao wamekuwepo duniani kwa muda
mrefu na wana uzoefu mkubwa zaidi wa mambo.
Kizazi cha kwanza ni kile kizazi ambacho kilileta
uhuru na kuendelea baada ya uhuru ambacho ni cha Rais wa Kwanza wa
Tanganyika, Julius Nyerere alizaliwa mwaka 1922, alianza kuongoza taifa
akiwa na umri wa miaka 39, aliacha uongozi akiwa na umri wa miaka 63
alifariki akiwa na umri wa miaka 77.
Katika kizazi hicho hicho cha kwanza alitoka Rais
wa Pili wa Jamhuri Ali Hassan Mwinyi ambaye alizaliwa mwaka 1925,
alipata uongozi kama Rais wa nchi akiwa na miaka 60 na alimaliza akiwa
na umri wa miaka miaka 70.

Post a Comment