HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI
WA BARAZA LA MAPINDUZI, MHE. DK. ALI MOHAMED SHEIN, KATIKA SHEREHE ZA
MAADHIMISHO YA MIAKA 51 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR, AMAAN STADIUM TAREHE
12 JANUARI, 2015
Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dk. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar;
Mheshimiwa Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dk. Salmin Amour Juma, Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume, Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Viongozi Wakuu Wastaafu Mliohudhuria;
Waheshimiwa Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar;
Mheshimiwa Mama Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar;
Mheshimiwa Othman Chande Mohamed, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Mheshimiwa Abdalla Mwinyi, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi;
Waheshimiwa Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa;
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Assalaam Alaikum,
Namshukuru Mwenyezi Mungu Muumba wa
Mbingu na Ardhi na Mwenye uwezo wa kila kitu kwa kutujaalia uhai na
uzima wa afya, tukaweza kukusanyika hapa leo kwa kusherehekea miaka 51
ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, ya tarehe 12 Januari, 1964. Namuomba
Mwenyezi Mungu aibariki shughuli yetu hii iwe ya mafanikio.
Pili, natoa shukurani zangu na za
wananchi wa Zanzibar kwako Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuja kuungana nasi katika
sherehe zetu hizi adhimu na muhimu.
Shukurani zetu vile vile zije kwenu
viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, mliopo madarakani na mliostaafu, Mabalozi wa nchi
mbali mbali, Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Viongozi wa dini na
vyama vya siasa na wananchi wote, kwa kuhudhuria kwa wingi kwenye
sherehe hizi.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Mwaka jana, katika tarehe kama ya leo
tuliadhimisha sherehe za kutimiza miaka 50 tangu tulipojikomboa, tarehe
12 Januari, 1964. Nawapongeza wale waliozifanikisha sherehe hizo pamoja
na wananchi wote kwa mahudhurio yenu katika hatua zote za maadhimisho
hayo.
Leo tunaadhimisha miaka 51 ya Mapinduzi
na tumefurahi sana kwa mafanikio tuliyoyapata katika kutekeleza dhamira
za Mapinduzi hayo Matukufu. Ni dhahiri kwetu sote kwamba Mapinduzi
ndiyo yaliyotukomboa wanyonge na kusimamisha utawala wa haki na usawa.
Tutaendelea kuwakumbuka wazee wetu Waasisi wa Chama cha Afro Shirazi
walioongozwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, kwa ushujaa wao na
jitihada zao za kupigania haki, kuleta usawa na maelewano na kuondoa
kila pingamizi walizokuwa wakizipata wananchi wa Unguja na Pemba.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Pamoja na ufanisi wa utekelezaji wa
dhamira ya Mapinduzi, ambayo nitaielezea baadae, tunaona fahari kubwa
kwamba mwaka uliopita, tulisherehekea kutimia miaka 50 ya Muungano wa
nchi zetu mbili zilizokuwa huru na kuanzishwa kwa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Tutaendelea kuutunza, kuuheshimu na kuuenzi Muungano huu
ambao ndio chombo kikubwa cha amani; umoja na mshikamano wa wananchi na
maendeleo yetu.Vile vile, sherehe zetu za leo zinajumuisha kumalizika
miaka minne ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, yenye
muundo wa Umoja wa Kitaifa. Kwa hakika, tumefanikiwa kufanya mengi
katika miaka minne hiyo, yakiwemo maendeleo ya uchumi wetu na maendeleo
ya jamii, pamoja na kudumisha amani, utulivu na mshikamano. Nawapongeza
viongozi na wananchi wote walioshiriki katika kuleta mafanikio haya.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Sasa nitaelezea baadhi ya mafanikio
yaliyopatikana baada ya Utekelezaji wa Dira 2020, MKUZA II, Ilani ya
Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2010-2015 na Malengo ya Milenia. Miongoni
mwa mafanikio muhimu yaliyopatikana ni kuwepo kwa amani, umoja na
mshikamano wa Wazanzibari na Watanzania wote kwa jumla, mambo ambayo
yamechangia sana kuongeza kasi yetu ya maendeleo.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika kutekeleza matakwa ya Katiba,
Serikali imeifanyia marekebisho Sheria Nam. 5 ya Tume ya Mipango na
kutunga Sheria Nam. 3 ya mwaka 2012. Tume ya Mipango ni chombo cha juu
cha kupanga, kuratibu na kusimamia mipango ya kiuchumi na ya
kijamii.Katika kipindi hiki cha miaka minne, Tume imesimamia utekelezaji
wa miaka mitano ya MKUZA na imesimamia utekelezaji wa maazimio
yaliyopitishwa kwa ajili ya utekelezaji wa “Matokeo kwa Ustawi” (Results
for Prosperity) katika Utalii, Mazingira na Utafutaji wa Fedha. Vile
vile, Tume imekamilisha vipaumbele vya utafiti kwa Zanzibar, imefanya
uchambuzi wa uchumi na jamii na kutoa muelekeo. Kadhalika imetoa
vipaumbele vya Zanzibar katika matayarisho ya Bajeti na Mpango wa
Maendeleo, imesimamia tafiti za Utumishi na imeandaa vipaumbele vya
mafunzo kwa ajili ya mahitaji ya wataalamu mbali mbali.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Uchumi wetu umekuwa ukikua mwaka hadi
mwaka kuanzia mwaka 2010 hadi 2014. Pato la Taifa limeongezeka kutoka
TZS bilioni 942.3 mwaka 2010 hadi kufikia TZS bilioni 1,442.8 katika
mwaka 2013, sawa na ongezeko la asilimia 53. Uchumi wetu umekua kutoka
asilimia 6.4 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 7.4 mwaka 2013. Pato la
Mtu Binafsi limeongezeka kwa wastani wa asilimia 38, kutoka TZS
778,000 (USD 558) mwaka 2010 na kufikia TZS milioni 1.077 (USD 667)
mwaka 2013.Kwa mwaka 2014, kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa na huduma
(mfumko wa bei) ilibaki katika wastani wa tarakimu moja, asilimia 5.6,
ikilinganishwa na asilimia 6.1 kwa mwaka 2010. Katika mwaka 2015 uchumi
wetu unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 7.8 na Pato la Taifa
litaongezeka hadi kufikia TZS bilioni 1,555.1.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kufuatia utaratibu unaokubalika duniani
kote wa kubadilisha mwaka wa kuanzia hesabu za makadirio ya takwimu za
Pato la Taifa kwa lengo la kuziimarisha takwimu ili zilingane na
mabadiliko ya kiuchumi yanayotokea, mwaka 2014, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya mapitio hayo. Ofisi hio
imerekebisha mwaka wa kuanzia hesabu za Pato la Taifa kutoka bei za
mwaka 2001 na sasa zitatumiwa takwimu za bei za mwaka 2007. Kwa msingi
huo, thamani ya Pato la Taifa imeongezeka kutoka TZS bilioni 1,442.8
mwaka 2013 kwa bei za mwaka 2001 mpaka TZS bilioni 1,859 kwa bei za
mwaka 2007. Kadhalika, ongezeko hilo la thamani la Pato la Taifa
limeongeza wastani wa Pato la kila Mzanzibari kutoka TZS Milioni 1.077
(US$656) kwa bei za mwaka 2001 hadi kufikia TZS Milioni 1.39 (US$ 870)
kwa bei za mwaka 2007.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imeongeza juhudi na kuimarisha ukusanyaji wa mapato pamoja na kupanua
wigo wa vianzio vya mapato hayo. Katika kipindi cha miaka minne,
2006/2007 hadi 2009/2010 Serikali ilikusanya mapato ya TZS bilioni 484;
ikilinganishwa na TZS. bilioni 997 zilizokusanywa katika kipindi cha
2010/2011 mpaka 2013/2014. Takwimu hizi zinaonesha ongezeko la asilimia
106. Natoa pongezi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania na Bodi ya Mapato
Zanzibar kwa kazi nzuri waliyoifanya.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
inaendelea kuimarisha mazingira ya biashara kwa kushirikiana na sekta
binafsi. Juhudi hizo zimeiwezesha Zanzibar kusafirisha bidhaa zenye
thamani ya TZS milioni 94,235.8 kwa mwaka 2014 kutoka bidhaa zenye
thamani ya TZS milioni 87,799.6 kwa mwaka 2013, sawa na ongezeko la
asilimia 7.3. Usafirishaji wa bidhaa kwenda Tanzania Bara umeongezeka
kutoka TZS milioni 71,396.8 mwaka 2011 hadi kufikia TZS milioni
642,110.3 mwaka 2014. Ongezeko hilo ambalo ni sawa na mara tisa,
limechangia katika kuongeza mapato ya Serikali na ajira.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kwa upande wa zao la karafuu, Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua juhudi za kulifufua zao hilo, ambapo
mpango wa miaka kumi umeandaliwa na umeanza kutekelezwa. Katika kipindi
cha miaka mitatu ya kwanza ya mpango huo; 2011/12 - 2013/2014, jumla ya
tani 11,477 za karafuu zenye thamani ya US$ milioni 130.82
zilisafirishwa na kuuzwa nje ya nchi. Kiwango hicho ni sawa na ongezeko
la tani 2,792 ambalo ni sawa na asilimia 32.1 ikilinganishwa na mwaka
2008/09 - 2010/2011.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Serikali imetimiza ahadi yake iliyoitoa
mwaka 2011 ya kuwalipa wakulima wa zao la karafuu asilimia 80 ya bei ya
karafuu ya soko la dunia. Karafuu za daraja la kwanza zinanunuliwa kwa
bei ya TZS 14,000 kwa kilo badala ya TZS 5,000 kwa kilo, bei iliyokuwepo
mwaka 2010. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 180. Kadhalika, vituo
vipya vya ununuzi na uuzaji wa karafuu vimejengwa, vituo vya zamani
vimekarabatiwa na huduma zote muhimu zinapatikana kwenye vituo hivyo.
Tumefanikiwa sana katika kupambana na magendo ya karafuu na wananchi
wanauza karafuu zao katika vituo vya ZSTC. Tunawashukuru Wananchi na
Vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama kwa kazi nzuri walioifanya ya
kushirikiana na Serikali katika kupambana na magendo ya karafuu.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kuhusu uwekezaji, katika kipindi cha
2010-2014 jumla ya miradi 141 imeidhinishwa na kuwekezwa nchini kupitia
Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA). Miradi hiyo itakapomalizika
itaingiza jumla ya mtaji wa US$ milioni 1,469 na kutoa nafasi za ajira
5,969.Kupitia ZIPA, Serikali imo katika hatua ya utekelezaji wa Mpango
wa uendelezaji wa mji mpya wa kisasa katika Maeneo Huru ya Uchumi ya
Fumba ili kuvutia wawekezaji. Mji huu utakuwa na mitaa ya biashara na
eneo la viwanda lenye ukubwa wa kiasi cha hekta 100. Mipango yetu
imejumuisha kujenga kituo cha kisasa cha mikutano cha kimataifa na
maeneo ya kupumzikia wananchi na wageni. Tayari shughuli za uwekezaji
wa miundombinu ya barabara, maji na umeme zimeanza. Natoa wito wananchi
washirikiane na Serikali katika kuziunga mkono jitihada hizi.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Serikali imeweka mkazo maalum wa
kuiendeleza sekta ya utalii ikiwa ni sekta kiongozi katika kukuza
uchumi wetu. Katika kutekeleza Mpango wa Utalii kwa Wote, idadi ya
watalii wanaokuja kutembelea Zanzibar imeongezeka kutoka watalii 132,836
mwaka 2010 na kufikia watalii 274,619 mwaka 2014. Hili ni ongezeko la
asilimia 107.Hivi sasa, inaandaliwa Sera ya Urithi wa Utamaduni
itakayotoa muongozo wa matumizi bora ya maeneo ya urithi ili kuimarisha
shughuli za utalii. Aidha, maeneo ya historia, mambo ya kale na urithi
wa utamaduni yaliyopo Mangapwani, Kuumbi Jambiani na Kwa Bi. Khole kwa
upande wa Unguja na Chwaka - Tumbe kwa Pemba yanaendelea kuimarishwa.
Wito wangu kwa wananchi wote wazitumie fursa hizo kujifunza masuala
mbali mbali yanayohusu utamaduni na urithi wetu wa kimaumbile.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kuhusu sekta ya elimu, Serikali
imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuiimarisha na kuiiendeleza
elimu. Katika kipindi hiki cha miaka minne, tumepata mafanikio makubwa
kuanzia kwenye skuli za maandalizi, msingi, sekondari hadi elimu ya
juu. Tumeweza kupunguza tatizo la upungufu wa walimu, maabara, vitabu
vya kusomea na uhaba wa madarasa na samani.Aidha, tumeweza kuajiri
walimu 1,781 wa ngazi mbali mbali. Idadi hii ni sawa na asilimia 74 ya
mahitaji. Hata hivyo, bado walimu 627 wanahitajika, sawa na asilimia
26. Aidha, idadi ya skuli za maandalizi imeongezeka kutoka skuli 238
mwaka 2010 hadi 279 mwaka 2014, ongezeko hili ni sawa na asilimia 17.
Skuli za msingi zimeongezeka kutoka 299 mwaka 2010 hadi skuli 359 mwaka
2014. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 20. Ingawa skuli za msingi
zimeongezeka katika mwaka 2014, lakini bado kuna upungufu wa skuli
hizo. Kwa hivyo, Serikali ina mpango wa kujenga skuli za msingi 10,
katika Wilaya zenye upungufu wa skuli za msingi. Jumla ya US$ milioni
kumi zimepatikana kutoka Shirika la Mafuta Duniani (OPEC) kwa ajili ya
ujenzi wa skuli hizo.
Kuhusu skuli za sekondari kuanzia Kidatu
cha Kwanza hadi cha Sita nazo zimeongezeka kutoka 194 mwaka 2010 hadi
skuli 210 mwaka 2014. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 8.Kwa lengo la
kukabiliana na tatizo la uhaba wa madarasa Serikali imekamilisha ujenzi
wa madarasa 513 kati ya madarasa 600 kwa mujibu wa lengo la mpango mkuu
wa elimu, ifikapo mwaka 2016. Idadi hii ni sawa na asilimia 85.5 ya
malengo. Serikali itafanya kila jitihada ili tuweze kulifikia lengo
hili.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika kipindi chote cha miaka minne,
Serikali imefanikiwa kuwaandikisha wanafunzi wote waliotarajiwa kuanza
darasa la kwanza. Jumla ya watoto 35,535 wameanza darasa la kwanza
mwaka 2014, ikiwa ni sawa na asilimia 100 ya uandikishaji. Idadi hii ni
sawa na ongezeko la asilimia nane ikilinganishwa na wanafunzi 32,983
walioandikishwa mwaka 2010. Jitihada hizo zinakwenda sambamba na
utekelezaji wa MKUZA II na Malengo ya Milenia.Kuhusu mafunzo ya elimu ya
amali, idadi ya vijana wanaojiunga na vituo vya mafunzo hayo
yanayotolewa katika kituo kilichopo Mkokotoni Unguja na Vitongoji Pemba,
imeongezeka kutoka wanafunzi 449 mwaka 2010 hadi kufikia wanafunzi 580
mwaka 2014. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 29. Hivi sasa Serikali
inatayarisha ujenzi wa skuli nyengine ya mafunzo ya amali huko
Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja na Mtambwe katika Mkoa wa Kaskazini
Pemba.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Vile vile, Serikali imechukua hatua ya
kuimarisha fursa za elimu ya juu. Idadi ya wanafunzi katika vyuo vikuu
vitatu vya Zanzibar imeongezeka kutoka 3,624 mwaka 2010 hadi 6,038 mwaka
2014. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 67. Sambamba na ongezeko la
wanafunzi, idadi ya masomo katika viwango vya shahada mbali mbali katika
vyuo vikuu vyote vitatu imeongezeka. Aidha, masomo ya udaktari (Doctor
of Medicine), yaliyoanzishwa mwaka 2013 yanaendelea vizuri na wanafunzi
99 wanaendelea na masomo yao ya mwaka wa kwanza na wa pili. Kadhalika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kutoa mikopo na hadi
kufikia Disemba, 2014 imetoa mkopo kwa wanafunzi 4,678 yenye jumla ya
TZS bilioni 19.4.kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya juu.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Huduma katika Hospitali ya Mnazi mmoja
zimeimarishwa, ili ifikie lengo la kuwa Hospitali ya Rufaa. Vifaa vya
kisasa vipya vimewekwa kwenye chumba cha upasuaji, maabara ya uchunguzi
wa maradhi, wodi mpya ya wagonjwa mahututi, wodi ya wazazi na chumba cha
wagonjwa wa dharura. Kadhalika, kituo cha meno cha tabasam, (smiling
centre) kinachowahudumia watu wenye matatizo ya midomo
kimeanzishwa.Jengo jipya la utoaji wa huduma za upasuaji wa kichwa na
uti wa mgongo, limezinduliwa rasmi tarehe 9 Januari mwaka huu. Huduma
zinazotolewa kwenye kitengo hiki, ambacho kimeanzishwa kwa msaada wa NED
ya Hispania ni cha kwanza kuwepo katika eneo la Afrika ya Mashariki na
Kati. Mradi wa huduma za mama na watoto, ujenzi wa jengo jipya la watoto
na huduma za wagonjwa wa maradhi ya figo, imeanza kutekelezwa. Vile
vile, kitengo cha uchunguzi wa maradhi ya mfumo wa chakula kimeanzishwa
na wodi mpya ya wagonjwa mahututi imefunguliwa rasmi tarehe 10 Januari,
2015.
Huduma kwenye hospitali ya Wete
zimeimarishwa ambapo wodi mpya ya wazazi, wodi ya wagonjwa wa akili na
chumba cha upasuaji vimejengwa. Vile vile, huduma katika hospitali ya
Chake Chake zimeimarishwa baada ya kuzipanua huduma za uchunguzi wa
maradhi kwa kuifanyia matengenezo makubwa maabara yake na kuwa maabara
ya kisasa, mashine mpya ya x-ray kufungwa, wagonjwa kupatiwa huduma za
damu salama na kitengo cha mazoezi ya viungo kufanyiwa
matengenezo.Katika kuziimarisha huduma za afya katika hospitali ya
Abdalla Mzee, ili ifikie daraja la hospitali ya Mkoa, hospitali ya
Abdalla Mzee ya Mkoani imeanza kujengwa upya kwa msaada wa Jamhuri ya
Watu wa China. Hospitali hii inatarajiwa kumalizika katika kipindi cha
miaka miwili ijayo.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika kipindi cha miaka minne
iliyopita, idadi ya madaktari na wataalamu mbali mbali wa afya
imeongezeka kutoka 3,634 mwaka 2010 hadi kufikia 4,618 mwaka 2014.
Ongezeko hili ni sawa na asilimia 26.Idadi ya madaktari wazalendo
walioajiriwa sasa imefikia 102. Idadi hii imefikiwa baada ya kuajiriwa
madaktari wazalendo 37 katika mwezi wa Novemba, 2014. Hivi sasa
Zanzibar wapo madaktari 40 wa kigeni. Kwa hivyo, idadi ya madaktari wote
wanaotoa huduma Zanzibar, sasa imefikia 142. Kwa idadi hii ya
madaktari na idadi ya watu wa Zanzibar, kwa mujibu wa sensa ya 2012,
daktari mmoja anatoa huduma kwa watu 9,708 hivi sasa. Kiwango hiki cha
madaktari kimesaidia sana katika kutoa huduma za afya kwa Unguja na
Pemba. Hata hivyo, jitihada za kuwasomesha madaktari na watalaamu
wengine wa afya zinaendelezwa.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Elimu ya Afya kwa umma inaendelea
kutolewa kwa njia mbali mbali ikiwemo Radio, TV, kupitia ZBC na
vipeperushi. Mkazo zaidi umewekwa kuwaelimisha wananchi kuhusu maradhi
ya kuambukiza na yasio ya kuambukiza. Serikali ilifanya jitihada maalum
juu ya kinga na tahadhari kuhusu maradhi ya Ebola. Mafanikio ya kutia
moyo yamepatikana kwenye huduma za mama na mtoto pamoja na chanjo
zinazotolewa dhidi ya maradhi mbali mbali na kwenye kampeni ya kitaifa
ya chanjo, ambapo asilimia 96.75 ya watoto walichanjwa Unguja na Pemba.
Kwa lengo la kupunguza vifo vya mama
wajawazito, Serikali inahimiza utekelezaji wa uamuzi wake uliotolewa
mwezi wa Mei, 2012 kwamba kinamama wajawazito wakajifungue kwenye vituo
vya afya na hospitali za Serikali bila ya malipo yo yote. Kwa hivyo,
nawataka wafanyakazi wa vituo vya afya na wodi za wazazi za Serikali,
wasiwatoze wazazi fedha zozote wanapokwenda kujifungua kwa njia ya
kawaida au ya upasuaji. Huduma hizi zinapaswa zitolewe bure.Kuhusu
UKIMWI, kiwango cha maambukizo kinaendelea kubakia kuwa asilimia 0.6 na
idadi ya wagonjwa wanaopata huduma ya ARVs imeongezeka kutoka wagonjwa
2,341 mwaka 2010 hadi 4,669 mwaka 2014. Ongezeko la idadi hii ni sawa
na asilimia 99. Jitihada zetu za kupambana na UKIMWI zimepata
mafanikio ya kuridhisha na wanaoishi na virusi vya UKIMWI ambao
wanatumia ARVs afya zao zimeimarika.
Naendelea kuwanasihi wananchi waendelee kupima afya zao, kwani tatizo la UKIMWI bado lipo.
Serikali inaendelea kuwahamasisha
wananchi kuchangia damu ili kuimarisha upatikanaji wa damu salama kwa
mahitaji ya wagonjwa wetu kupitia kitengo cha damu salama. Katika mwaka
2010/2011, kitengo hiki kililenga kukusanya “units” 6,000 za damu na
kufanikiwa kukusanya “units” 7,965. Ongezeko hili ni sawa na asilimia
33. Katika mwaka 2013/2014, mahitaji yaliongezeka na kufikia units
10,000 kwa mwaka ambapo makusanyo yalifikia asilimia 95 ya lengo.
Kutokana na mafanikio haya yaliyopatikana, nawapongeza wale wote
wanaochangia damu kwa imani yao ya kuwasaidia wagonjwa wote. Ili
kuhakikisha upatikanaji wa damu salama ya kutosha, natoa wito kwa
wananchi wote wajitokeze kuchangia damu ambayo inahitajika katika
hospitali zetu za Unguja na Pemba katika wodi ya wazazi, watoto upasuaji
na wodi za dharura.
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kuhusu malaria, baada ya kasi ya malaria
kupungua, baada ya jitihada zilizochukuliwa na Serikali, mikakati mbali
mbali ya ziada ya kupambana na malaria imeongezwa. Hivi sasa, bado
kiwango cha malaria kipo chini ya asilimia 1. Katika mwaka 2013, shehia
71 hazikuwa na mgonjwa hata mmoja wa malaria, lakini wagonjwa wachache
wamebainika katika Wilaya ya Magharibi, Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja
na Wilaya ya Micheweni kwa Pemba.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa
Awamu zote za uongozi ndani ya kipindi cha miaka 51, imetekeleza mipango
mbali mbali ya kuwapatia wananchi huduma ya maji safi na salama kwa
kuamini kuwa maji ni uhai. Vile vile, suala hili limepewa kipaumbele
katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2010 - 2015, ambapo
Serikali imetakiwa kusambaza huduma ya maji safi na salama kutoka
asilimia 75 hadi asilimia 95 kwa mijini na kutoka asilimia 60 hadi
asilimia 80 kwa vijijini ifikapo mwaka 2015. Ili kufikia lengo hilo,
Serikali kwa kushirikiana na Washirika mbali mbali wa Maendeleo
imetekeleza miradi kumi, program mbili na mpango wa kulinda vyanzo vya
maji.
Katika kipindi cha miaka minne, jumla ya
visima 106 vimechimbwa, matangi 31 yenye viwango tofauti yamejengwa na
mabomba yenye urefu wa km. 371.65 yamelazwa katika maeneo mbali mbali ya
Mikoa yote ya Unguja na Pemba. Katika jitihada hizi, uzalishaji maji
wa jumla ya lita milioni 17.6 umefikiwa na idadi ya watu 175,873
wameongezeka katika kupatiwa huduma za maji katika kipindi hiki. Hadi
kufikia Disemba, 2014, mahitaji halisi ya maji kwa Unguja na Pemba, ni
lita milioni 214.6 na uzalishaji uliofanyika katika kipindi hiki ni lita
milioni 163. Kiwango hiki ni sawa na asilimia 76 ya mahitaji na
kiwango cha upungufu ni asilimia 24.
Katika takwimu hizi Mkoa wa Mjini
Magharibi, kiwango cha upatikanaji wa maji kimefikia asilimia 87.7 ya
mahitaji halisi, Mkoa wa Kaskazini Unguja asilimia 71.68, Mkoa wa Kusini
Unguja asilimia 76.45, Mkoa wa Kaskazini Pemba asilimia 56.42 na Mkoa
wa Kusini Pemba asilimia 74.08.Juhudi hizi, ni kielelezo cha jinsi
Serikali inavyozingatia umuhimu wa kuwapatia wananchi huduma ya maji
safi na salama kulingana na MKUZA II na Ilani ya CCM ya Uchaguzi ya
mwaka 2010-2015. Natoa wito kwenu wananchi muendelee kuwa na subira na
mshirikiane na Serikali katika kuvitunza vianzo vyote vya maji.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika kipindi hiki cha miaka minne,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, ilikamilisha kazi za
ujenzi wa barabara 11 zenye urefu wa km 102 za mikoa miwili ya Pemba na
barabara nne zenye urefu wa km. 34.85 za mikoa mitatu ya Unguja
zilizoanzwa kujengwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya
Sita. Barabara zote hizo zilizinduliwa katika sherehe za Mapinduzi za
mwaka 2014 na 2015. Kukamilika kwa barabara hizi kumerahisisha usafiri
wa abiria, usafirishaji wa mazao ya wakulima, shughuli za kijamii,
kukuza uchumi na kuimarisha mtandao wa barabara zetu.Ujenzi wa barabara
mpya ya Jendele-Cheju hadi Kaebona yenye urefu wa km 11.7 na barabara
ya Koani hadi Jumbi yenye urefu wa km 6.3 umeanza na kazi inaendelea
vizuri.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Ujenzi wa barabara ya Wete hadi Gando
(km 15) na barabara ya Wete hadi Konde (km 15) umefikia hatua ya utiaji
lami na kukabidhiwa katika kipindi kifupi kijacho. Aidha, maandalizi
ya ujenzi wa barabara kutoka Ole hadi Kengeja yenye urefu wa km 35
yameanza. Ujenzi wa barabara ya Chake Chake hadi Wete yenye urefu wa km
22.1 utaanza baada ya kukamilika kwa barabara ya Wete hadi Gando na Wete
hadi Konde. Ujenzi wa barabara hizo unafadhiliwa kwa pamoja kati ya
Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kiarabu (BADEA) na Serikali ya Saudi
Arabia (SAUDI FUND) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Natoa
shukurani kwa Shirika la MCC la Marekani, Benki ya BADEA na Serikali ya
Saud Arabia kwa kushirikiana nasi katika ujenzi wa barabara saba za Mkoa
wa Kaskazini Pemba na kwa Serikali ya Norway kwa msaada wao katika
ujenzi wa barabara za Mkoa wa Kusini Pemba.Natoa wito wangu kwa wananchi
wazitunze barabara hizi ili zidumu kwa muda mrefu kwa madhumuni ya
kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi yetu.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika uimarishaji wa miundombinu ya
bandari, Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya Azam Marine imejenga
majengo mapya ya kupumzikia abiria katika Bandari ya Malindi. Aidha,
Serikali imenunua mashine na vifaa mbali mbali kwa ajili ya kuimarisha
shughuli za kazi bandarini. Jitihada zinafanywa ili kuziongeza mashine
na vifaa vyengine. Katika jitihada za kuziimarisha huduma za bandari
kutokana na shughuli nyingi ziliopo katika bandari ya Malindi, na
uchache wa nafasi, Serikali imeamua kujenga bandari mpya huko
Mpigaduri. Upembuzi yakinifu umekamilika na jitihada za kuanza ujenzi
zinafanywa.
Kadhalika, Mamlaka ya Usafiri Baharini
imeimarisha ukaguzi wa vyombo vya baharini kwa kushirikiana na SUMATRA,
hatua ambayo imepelekea kupungua kwa ajali za vyombo vya baharini kwa
kiasi kikubwa. Katika kuimarisha usafiri wa abiria baharini, Serikali
iliamua kununua meli mpya kwa ajili ya kupunguza tatizo la usafiri wa
abiria na mizigo yao. Meli hiyo yenye uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na
mizigo tani 200 inatarajiwa kufika nchini mwezi wa Juni, 2015.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kwa upande wa usafiri wa anga, ujenzi wa
maegesho ya ndege na njia ya kupitia ndege unaojengwa kwa ajili ya
kukiimarisha kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume
umekamilika na tarehe 3 Januari, 2015 umezinduliwa. Ujenzi wa jengo
jipya la abiria bado unaendelea na unatarajiwa kumalizika mwezi Oktoba
2015. Kazi ya kuweka taa katika Kiwanja cha Ndege cha Pemba inatarajiwa
kuanza hivi karibuni na kumalizika mnamo mwezi wa Juni mwaka huu.
Kumalizika kwa kazi hizo, kutaimarisha usafiri wa ndege na kuimarisha
utalii na biashara.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu
ya Saba, imesimamia na kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi.
Serikali imetayarisha sera mpya ya ardhi ambayo imezingatia mabadiliko
na maendeleo ya kijamii na kiuchumi tuliyofikia hivi sasa pamoja na
mwelekeo wetu wa miaka ijayo.
Vile vile, kazi ya usajili na utambuzi
wa ardhi inaendelea. Hadi hivi sasa, shehia 20 za Unguja na Pemba
zishasajiliwa na 13 nyengine zinaendelea na zoezi la utambuzi. Zoezi la
utoaji wa Hati za Matumizi ya Ardhi mpya pamoja na kuzibadilisha hati
za zamani, linaendelea. Napenda niwahimize wananchi, wauitikie wito wa
usajili wa ardhi, ili zoezi hili liweze kufanyika kwa haraka kama
ilivyopangwa kwenye MKUZA II la kusajili asilimia 50 ya ardhi mwaka huu
wa 2015.
Katika kipindi hiki cha miaka minne,
katika sekta ya ardhi jumla ya mikataba 223 imesainiwa na kukabidhiwa
wawekezaji sambamba na utoaji wa hati 1,310 za matumizi mbali mbali ya
ardhi. Vile vile, jumla ya viwanja 1,691 vimepimwa Unguja na Pemba kwa
matumizi mbali mbali ikiwemo nyumba za makaazi za wananchi.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Hivi sasa wakati tunasherehekea miaka 51
ya Mapinduzi ya 12 Januari, 1964, mafanikio makubwa yamepatikana ya
kuwa na umeme wa MW 100 kwa Unguja na MW 20 kwa Kisiwa cha Pemba.Kazi
kubwa imefanyika katika kuusambaza umeme huu kwa Unguja na Pemba, kwa
mijini na vijijini. Hivi sasa huduma za umeme zinapatikana katika miji
yote na huduma hizi zimefikishwa katika vijiji 129 badala ya 123
vilivyokisiwa awali. Hili ni ongezeko la asilimia 4.9. Ahadi ya
Serikali ya kupeleka umeme kwenye visiwa vidogo vidogo imeanza
kutekelezwa. Tayari kazi ya kupeleka umeme Kisiwa Panza, Makoongwe na
Shamiani huko Pemba, imeanza na inatarajiwa kukamilika mwaka huu, 2015.
Nawanasihi wananchi wa Kisiwa Panza, Makoongwe na Shamiani, waendelee
kuwa na subira huku Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) likifanya bidii
kubwa ya kuikamilisha kazi hiyo.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Serikali inafanya jitihada mbali mbali
katika kuendeleza Mapinduzi ya Kilimo ili kuongeza uzalishaji, kuwa na
uhakika wa chakula na lishe. Kwa lengo la kuwasaidia wakulima hasa wa
mpunga, Serikali inaendeleza programu iliyoanzishwa mwaka 2011 ya kuwapa
ruzuku wakulima ya asilimia 75 ya gharama za bei ya mbolea, mbegu, dawa
ya kuulia magugu na huduma za matrekta. Katika kipindi hiki, zana,
vifaa na nyenzo mbali mbali zilinunuliwa. Jumla ya wakulima 61,500 wa
kilimo cha kutegemea mvua na kilimo cha umwagiliaji maji walifaidika.
Vile vile, mavuno ya zao la mpunga kwa
jumla, yaliongezeka kutoka tani 21,014 mwaka 2010 hadi tani 33,655
mwaka 2013. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 60. Juhudi za Serikali
za kutoa ruzuku zimesaidia sana kupatikana mafanikio haya na juhudi hizi
zitaendelezwa katika miaka ijayo.
Kadhalika, jitihada za kuendeleza
miundombinu ya umwagiliaji maji wa hekta 2,200 katika mabonde ya Cheju,
Kibokwa na Kilombero kwa Unguja na Mlemele na Makwararani kwa Pemba
zinaendelea. Kazi iliopo hivi sasa ni kuanza ujenzi wa miundombinu hio
baada ya kazi ya usanifu (design) kukamilika. Fedha za miradi hii
tayari zimepatikana kutoka Exim Bank ya Jamhuri ya Korea na Benki ya
Dunia.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika kuendeleza utafiti, kwa lengo la
kuimarisha kilimo Serikali imeanzisha Taasisi ya Utafiti ya Kizimbani na
inashirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania (COSTECH) katika kuendeleza utafiti. Jumla ya mbegu 43
zimefanyiwa utafiti kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa zao la
mpunga wa kimataifa (IRRI). Kwa upande wa utafiti wa mbegu za mazao ya
mizizi, Taasisi ya Utafiti imeweza kutoa mbegu zinazostahamili maradhi
na kunawiri katika mazingira ya Zanzibar.
Katika kipindi cha miaka minne
iliyopita, mwaka 2014 ulikuwa ni mwaka wa mafanikio kwa watu wa Zanzibar
ambapo uzalishaji wa mazao muhimu ya chakula ulifikia tani 674,334.
Kiwango hiki ni ongezeko la asilimia 95 la tani 346,535 zilizovunwa
mwaka 2013.Aidha, katika kipindi cha miaka minne, jitihada za kuotesha
na kupanda miti zilichukuliwa ambapo jumla ya miti milioni 5 ya misitu
ilioteshwa katika vitalu vya Serikali na miche milioni 8 katika vitalu
vya watu binafsi.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kuhusu sekta ya mifugo, Serikali
imefanya juhudi kubwa ya kuwaendeleza wafugaji kupitia programu ya
Uimarishaji wa Huduma za Mifugo (ASDP-L) yenye kutoa taaluma ya ufugaji
bora. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, wafugaji 54,567
wametembelewa na kupewa ushauri wa kitaalamu.Vituo vya kutolea huduma za
utibabu na uzalishaji wa mifugo pamoja na huduma za utafiti na utibabu
wa wanyama ziliimarishwa. Vile vile, matengenezo makubwa ya maabara ya
Maruhubi, Unguja na ya Chake Chake, Pemba yamefanywa.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika kipindi hiki cha miaka minne
sekta ya uvuvi imeimarika ambapo mchango wa sekta hii katika Pato la
Taifa umefikia asilimia 7.2. Tani 148,535 za samaki walivuliwa wenye
thamani ya TZS bilioni 527.5. Jumla ya wavuvi 2,320, walifundishwa
taaluma na mbinu bora za uvuvi na ufugaji wa samaki unaozingatia hifadhi
ya mazingira. Vikundi 100 vya ufugaji samaki vimeundwa na mabwawa sita
ya kufugia samaki yameanzishwa Unguja na Pemba.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Ukulima wa zao la mwani umeimarishwa,
ambapo wananchi wengi, hasa wanawake, wanajishughulisha na uzalishaji wa
zao hili hivi sasa. Kiasi cha tani 51,687 za mwani mkavu zenye thamani
ya TZS bilioni 18.7 zilisafirishwa kwa kipindi cha miaka minne
iliyopita.Nawasisitiza sana wananchi waendelee kupinga vitendo vya uvuvi
haramu ili kazi ya uvuvi iwe endelevu na yenye tija. Aidha, Serikali
itaendelea kuwahamasisha wawekezaji wawekeze kwenye uvuvi wa bahari kuu
ili kuongeza mchango wa sekta hii katika uchumi na kutoa fursa za ajira
kwa vijana.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Zanzibar kama ilivyo nchi nyingi
duniani, inakabiliwa na changamoto za kimazingira ikiwa ni pamoja na
uharibifu wa misitu, utupaji mbaya wa taka na umwagaji wa maji machafu,
uchimbaji wa mawe, mchanga na kifusi.Katika kukabiliana na hali hiyo,
Serikali inaitumia Sera mpya ya Mazingira ya mwaka 2013 kwa ajili ya
kuzishughulikia changamoto za kimazingira pamoja na kutayarisha mpango
wa usimamizi wa mazingira. Kadhalika, Serikali imeandaa na kuzindua
Mkakati wa Zanzibar wa Mabadiliko ya Tabianchi ambao una shabaha ya
kuihami Zanzibar dhidi ya athari hizo. Vile vile, sheria mpya ya
mazingira yenye lengo la kulinda na kusimamia mazingira imeandaliwa na
inatarajiwa kupelekwa katika Baraza la Wawakilishi kwenye vikao vijavyo.
Hadi kufikia mwezi wa Septemba, 2014,
jumla ya tani 4.0 za mifuko ya plastiki zimekamatwa mafanikio haya
yamepatikana kutokana na utekelezaji na usimamizi wa kanuni za mwaka
2011. Natoa wito kwa kila mmoja wetu ashiriki katika kuyalinda na
kuyahifadhi mazingira yetu, ambayo ni muhimu katika maendeleo yetu.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Serikali imeendelea kufanya jitihada
mbali mbali za kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutekeleza mipango
yenye lengo la kuinua kipato cha wananchi na kukabiliana na tatizo la
ukosefu wa ajira hasa kwa kinamama na vijana.Tarehe 21 Disemba, 2013,
Serikali ilizindua Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ili kukabiliana
na tatizo la ajira na kuinua uchumi wa wananchi.
Mfuko huu hivi sasa una jumla ya TZS
bilioni 2.313.Hadi tarehe 31 Disemba, jumla ya mikopo 706 imeidhinishwa
kwa Unguja na Pemba na jumla ya TZS milioni 795.55 zimekopeshwa kwa
wananchi. Katika mikopo iliyotolewa, ajira za moja kwa moja 1,384 na
ajira zisizo za moja kwa moja 4,000 zimepatikana. Jumla ya TZS milioni
146.95 tayari zimerejeshwa kuanzia Julai hadi Novemba, 2014. Mfuko huu
umetoa mikopo katika sekta muhimu za kiuchumi.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
inatekeleza vyema wajibu wake wa kuielimisha jamii na kuipa habari za
ndani na nje ya nchi. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Shirika
la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) limesimamia mfumo wa utangazaji, kutoka
“Analogue” kwenda “Digital” kwa mafanikio makubwa. Matangazo ya Radio
na TV yanaendelea kwa saa 24 tangu yalipoanzishwa pamoja na chaneli ya
pili ya ZBC (ZBC2) imeanzishwa ili kuimarisha huduma zake. Vifaa vipya
kwa ajili ya studio ya Karume House na studio ya Pemba vimenunuliwa na
wafanyakazi wa ZBC wamepewa mafunzo kwa ajili ya kuwawezesha kufanya
kazi kwa ufanisi zaidi.
Aidha, Serikali imetekeleza ahadi yake
ya kuwajengea wasanii Studio ya kisasa ya kurekodia nyimbo na michezo ya
kuigiza kwenye jengo la zamani la Utangazaji la Sauti ya Tanzania
Zanzibar, baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa. Vifaa vipya kwa ajili
ya Studio vinatarajiwa kununuliwa hivi karibuni.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Utamaduni ni kielelezo cha utambulisho
wa jamii. Kwa kuzingatia umuhimu huo, Serikali imeendelea kusimamia na
kuuendeleza utamaduni wetu, silka na desturi zetu. Katika kipindi cha
miaka minne iliyopita, Zanzibar imeendelea kuandaa matamasha mbali mbali
ambayo yamesaidia sana kuendeleza na kuhifadhi utamaduni wa mambo ya
asili, kuchangia uchumi wetu na kutoa ajira kwa vijana. Nawanasihi
wananchi wote tuendeleze utamaduni wetu na mila zetu kwa manufaa yetu
na kizazi kijacho.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Serikali imetekeleza mambo mbali mbali
katika kuimarisha sekta ya michezo. Miongoni mwa mambo hayo ni
kuandaliwa kwa sera mpya ya michezo ya Zanzibar itakayoimarisha na
kuiendeleza michezo yote. Serikali imeanzisha mashindano ya riadha ya
Wilaya, kwa Wilaya zote kumi za Zanzibar na ilitoa vifaa vya michezo
kwa wanariadha 250 ili kurejesha vugu vugu la michezo ya riadha.
Utaratibu wa kutoa vifaa kwa wanamichezo utaendelezwa. Vile vile,
Serikali imewahamasisha wananchi waendeleze michezo ili wajenge afya zao
kwa kufanya mazoezi ya viungo kila siku na washiriki kwenye tamasha la
mazoezi ya viungo linalofanyika litakalofanyika tarehe 1 Januari ya kila
mwaka.
Kadhalika, katika kuhakikisha watoto
wetu wanapata maeneo ya kucheza na kufurahi, Serikali kupitia Mfuko wa
Hifadhi ya Jamii imekijenga upya Kiwanja cha Kufurahishia Watoto cha
Uhuru kiliopo Kariakoo kwa TZS bilioni 15. Kiwanja hicho kimefunguliwa
tarehe 8 Januari, 2015 katika shamrashamra za miaka 51 ya Mapinduzi na
kina aina nyingi ya michezo ambayo watoto wataifurahia sana. Ujenzi wa
Kiwanja cha Kufurahishia Watoto cha Tibirinzi Pemba, utakamilika hivi
karibuni.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kwa lengo la kutekeleza azma ya Serikali
ya kukifufua Kiwanda cha Upigaji Chapa na Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa
Serikali ili kurudisha hadhi yake na kuinua kiwango cha uzalishaji,
jumla ya TZS milioni 5,532.40 zimetumika kwa matengenezo ya majengo
yaliyokuwa kiwanda cha sigara Maruhubi pamoja na ununuzi wa mashine mpya
za kisasa za uchapishaji za kiwanda hicho.
Hivi sasa kiwanda hiki kina uwezo wa kuchapisha vitabu na nyaraka za aina mbali mbali. Serikali ina lengo la kukiimarisha zaidi ili kiweze kuchapisha magazeti, vitabu vikubwa na kadhalika. Ni dhahiri kukamilika kwa kiwanda hiki kumeipunguzia mzigo Serikali na kitaiwezesha kutoa huduma zenye ubora wa kiwango kikubwa zaidi.
Hivi sasa kiwanda hiki kina uwezo wa kuchapisha vitabu na nyaraka za aina mbali mbali. Serikali ina lengo la kukiimarisha zaidi ili kiweze kuchapisha magazeti, vitabu vikubwa na kadhalika. Ni dhahiri kukamilika kwa kiwanda hiki kumeipunguzia mzigo Serikali na kitaiwezesha kutoa huduma zenye ubora wa kiwango kikubwa zaidi.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Miongoni mwa malengo ya Mapinduzi ya
tarehe 12 Januari, 1964 ni kuwahudhumia na kuwatunza wazee. Katika
kutekeleza azma hii Serikali imeendelea kuwatunza na kuwahudumia ambapo
huduma zote muhimu zimeimarishwa na zinapatikana kwa ajili ya maisha
yao ya kila siku.
Kadhalika, Serikali imefanya jitihada
mbali mbali ili kuwasaidia watu wenye ulemavu. Mfuko Maalum wa Watu
Wenye Ulemavu umeanzishwa na uliozinduliwa mwaka 2012. Mfuko huu una
jumla ya TZS milioni 167.6 ambazo zitatumika kwa mahitaji mbali mbali ya
watu wenye ulemavu. Vile vile usajili wa watu wenye ulemavu uliofanywa
kwenye Wilaya zote za Unguja na Pemba sasa umekamilika, na umesaidia
sana kuwatambua ili kurahisisha upangaji na utekelezaji wa mipango yao
ya maendeleo.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Vitendo vya unyanyasaji wa wanawake na
watoto bado vinaendelea kuwepo. Tarehe 6 Disemba 2014, Serikali
ilizindua rasmi Kampeni ya kupinga vitendo vya udhalilishaji wa wanawake
na watoto. Mpango wa miaka miwili tayari umeandaliwa na utatekelezwa
na taasisi zote za Serikali na za kiraia kwa kushirikiana na Washirika
wa Maendeleo. Sote tuseme kwa kauli moja na tuoneshe kwa vitendo, kwamba
udhalilishaji wa wanawake na watoto sasa basi. Hii ni imani yangu na
bila ya shaka hii itakuwa ni imani ya wananchi wote wa Zanzibar.
Tunapaswa tuchukue hatua sasa, kwa pamoja tutafanikiwa.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Serikali inaendeleza jitihada za
kuhakikisha kwamba watumishi wa umma wanatekeleza wajibu wao ipasavyo
kwa kuwatumikia wananchi bila ya ubaguzi wowote. Katika kipindi hiki,
viwango vya utendaji kazi vimeongezeka na haya yamedhihirika kutokana na
mafanikio yaliyopatikana. Ingawa bado zipo changamoto zinazotukabili,
lakini jitihada zinaendelea kuchukuliwa ili kuziondoa changamoto hizo
hatua kwa hatua.
Katika kipindi cha miaka minne
iliyopita, jumla ya wananchi 19,758 walipatiwa ajira. Watumishi
walioajiriwa Serikalini na kwenye mashirika ya umma ni 5,667. Wananchi
7,256 walipatiwa ajira katika sekta binafsi na wananchi 6,835 walipatiwa
ajira katika vyama vya ushirika. Vile vile, wapo wananchi waliojiajiri
wenyewe baada ya kupata mikopo ambao ni 3,400 na wananchi 4,000
wamepata ajira zisizokuwa za moja kwa moja.
Kwa upande wa maslahi ya wafanyakazi,
Serikali ililishughulikia suala hili kwa kuwaongezea mishahara na posho
wafanyakazi wote wa Serikali katika mwaka wa fedha 2011/2012 na
2013/2014. Marekebisho hayo, yalizingatia mambo mbali mbali ya sheria ya
Utumishi wa Umma na Kanuni zake.Serikali itahakikisha kuwa maslahi ya
watumishi wa umma yanaimarishwa kutokana na utendaji wao wa kazi, ili
yawe bora zaidi, kwa kuwaongezea mishahara na stahili nyengine kadri
hali ya uchumi wetu inavyoimarika na kwa kuzingatia miundo ya utumishi
mipya ambayo sasa iko tayari kutumika.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kwa lengo la kuziimarisha huduma za
mawasiliano Serikalini, Serikali ilianzisha mradi wa “e-government”
uliozinduliwa mwaka 2013. Hadi hivi sasa, jumla ya majengo 86 ya
Serikali yameunganishwa katika mtandao wa Serikali (e-government) na
tayari yameanza kupata huduma ya intaneti bila ya malipo. Awamu ya
kwanza ya mradi huu inaendelea vizuri na maandalizi ya awamu ya pili
yamekamilika.Kupitia mradi wa “e-government”, maeneo yote ya visiwa vya
Zanzibar yanaunganishwa na baadae Zanzibar itaunganishwa na Tanzania
Bara kupitia mkonga wa Taifa na itaunganishwa na mkonga wa mawasiliano
wa Kimataifa wa “EASSy” na “SEACOM”.
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika utekelezaji wa dhamira ya
Serikali ya kuimarisha Utawala Bora, Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu
wa Uchumi imeanzishwa baada ya kutungwa Sheria Namba 1 ya mwaka 2012.
Taasisi hii imeanza kazi zake baada ya kupatiwa nyenzo, vifaa vya kazi
na wafanyakazi na inaendelea vizuri. Vile vile, sheria ya maadili ya
viongozi tayari imeandaliwa na inatarajiwa kupelekwa kwenye Baraza la
Wawakilishi kwenye kikao kijacho.Aidha, katika kipindi hiki, Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amewasilisha Serikalini Ripoti ya
Ukaguzi ya mwaka 2010/2011 hadi 2012/2013 na Serikali iliziwasilisha
kwenye Baraza la Wawakilishi, kama Katiba ya Zanzibar ya 1984
inavyoelekeza na baadae Serikali ilizifanyia kazi.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Baraza la Wawakilishi la Zanzibar la
Nane lililoanza kazi zake mwezi Novemba 2010, limetekeleza shughuli zake
kwa ufanisi mkubwa. Hadi kufikia Disemba, 2014 jumla ya mikutano 17
imefanywa na Baraza hilo. Aidha, jumla ya miswada 53 imepitishwa kuwa
sheria na hoja binafsi tatu za wajumbe zilipokelewa na kufanyiwa kazi.
Kadhalika, wajumbe na watumishi wa Baraza walipatiwa mafunzo ndani na
nje ya nchi ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.
Katika kipindi hiki cha miaka minne,
Serikali imechukua juhudi mbali mbali za kuziimarisha mahakama ili
ziweze kutekeleza kazi zake kwa ufanisi. Idadi ya majaji imeongezeka
kutoka majaji wawili mwaka 2011 hadi sita mwaka 2014; wakiwemo wanawake
wawili. Kadhalika, idadi ya mahakimu katika ngazi mbali mbali
imeongezeka kutoka 43 mwaka 2010 hadi 69 mwaka 2014. Ongezeko hili ni
sawa na asilimia 60. Jumla ya kesi 29,786 zilifunguliwa katika mahakama
zote za Unguja na Pemba ambapo kesi 19,952 ziliweza kutolewa maamuzi,
sawa na asilimia 51.7.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika hotuba yangu niliyoitoa katika
Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 49 ya Mapinduzi, nilielezea uamuzi wa
Serikali wa kuleta mageuzi kwenye mfumo wetu wa kiutawala kwa kuzipa
uwezo zaidi Serikali za Mitaa. Nilielezea kuwa Serikali iliandaa Sera
ya Serikali za Mitaa pamoja na Mpango wa Utekelezaji. Ili kuipa nguvu
Sera hio na Mpango wake, Serikali imefanyia marekebisho Sheria Namba 3
na 4 ya mwaka 1995 na Sheria Namba 1 ya mwaka 1998 na tayari imeandaa
sheria mpya ya Tawala za Mikoa na Sheria mpya ya Serikali za Mitaa za
mwaka 2014. Ninatarajia kwamba wananchi wataendelea kutuunga mkono
katika mabadiliko haya tunayokusudia kuyatekeleza.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika kukabiliana na changamoto mbali
mbali za kimazingira zinazoikabili Manispaa ya Zanzibar pamoja na miji
ya Chake Chake, Wete na Mkoani, Serikali ilianzisha Mradi wa Huduma za
Jamii (ZUSP) mwaka 2011. Lengo kuu la mradi huu ni kuimarisha
upatikanaji wa huduma za mji Unguja na miji ya Pemba na kuhifadhi eneo
la urithi wa Mji Mkongwe.Katika kipindi hiki cha miaka minne, gari 19
zimenunuliwa, vizimba vinaendelea kujengwa, jengo la Manispaa
linafanyiwa ukarabati, taa za barabarani zimeanza kuwekwa na ujenzi
unaendelea katika maeneo mbali mbali ya miradi.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kama nilivyosema hapo awali, maelezo
niliyoyatoa yalikuwa ni muhtasari tu wa mafanikio ya kisiasa, kiuchumi
na kijamii, tuliyoyapata wakati tunapoadhimisha miaka 51 ya Mapinduzi ya
tarehe 12 Januari, 1964. Ni wajibu wetu tuyaendeleze mafanikio haya na
tufanye kila jitihada, ili nchi yetu iweze kupata mafanikio zaidi.
Jukumu kubwa tulilonalo ni lazima tuhakikishe kwamba amani na utulivu
inatunzwa, inaimarishwa na inaendelezwa wakati wote. Bila ya shaka
yoyote, hali hio tutaifikia tu, ikiwa tutaendeleza umoja, mshikamano
wetu na mapenzi baina yetu.
Sote tuna wajibu wa kuzitii sheria ikiwa
ni hatua moja muhimu katika kuitekeleza mipango yetu ya maendeleo na
kuzitatua changamoto mbali mbali zilizotukabili. Ni wajibu wa viongozi
wote wa Serikali, wanasiasa, viongozi wa dini na viongozi wengine katika
jami, sote kwa pamoja tutekeleze wajibu wetu huo kwa kuhakikisha kuwa
amani na utulivu inadumishwa, inaendelezwa na sheria za nchi
zinafuatwa. Mapinduzi yetu na Muungano wetu ndizo nguzo zetu kubwa za
maendeleo yetu na ndivyo vilivyotufikisha hapa tulipo hivi leo na ndivyo
vitakavyotufikisha kule dira zetu za maendeleo zinavyotuelekeza tufike
hapo baadae.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kwa kuzingatia umuhimu wa Muungano wetu,
katika kipindi cha miaka minne hii, nchi yetu ilikabiliwa na mambo
kadhaa muhimu ya kuuimarisha Muungano wetu. Miongoni mwa mambo hayo ni
kuanza kwa mchakato wa kupata Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, ulioanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, na kupelekea kutungwa kwa Sheria
ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba Namba 8 ya Mwaka 2011.Bunge Maalum la
Katiba la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilikamilisha kazi yake muhimu
ya kutunga Katiba Mpya na kuikabidhi Katiba inayopendekezwa kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na kwangu,
tarehe 8 Oktoba, 2014 huko Dodoma.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Mwaka huu tumekabiliwa na kuipigia kura
ya maoni Katiba inayopendekezwa, ifikapo tarehe 30 Aprili, 2015 kama
ilivyotangazwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya
Mrisho Kikwete. Vile vile, kama nyote mjuavyo, mwaka huu tunakabiliwa
na Uchaguzi Mkuu wa nchi yetu ambao hufanyika kila baada ya miaka
mitano.Chaguzi hizi mbili tutakazozifanya ni kielelezo cha kukua kwa
demokrasia nchini na ni wajibu wetu tuendelee kuzitii sheria zetu katika
kusimamia maslahi ya nchi yetu na tufanye jitihada za pamoja za kulinda
amani na utulivu nchini. Serikali zetu mbili zitaendelea kutimiza
wajibu wake wa kuilinda nchi yetu na zitahakikisha kuwa wakati wote
zinakabiliana na vitendo vyo vyote vya uvunjaji wa amani na sheria.
Nchi yetu iko salama na Mwenyezi Mungu ataijaalia kuwa salama wakati
wote. Vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama viko imara katika kuilinda
nchi yetu na mipaka yake.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika hotuba zangu za Maadhimisho ya
Sherehe za Mapinduzi ya miaka 47 mwaka 2011 na miaka 48 mwaka 2012,
nilielezea jinsi Serikali ya Mapinduzi ya Awamu ya Saba yenye Muundo wa
Umoja wa Kitaifa ilivyoanza kazi zake na ilivyokuwa ikiendelea
kuwatumikia wananchi.Leo baada ya kukamilisha miaka minne na kuuanza
mwaka wa tano wa kuiongoza Serikali hii, napenda nielezee furaha kubwa
niliyonayo kutokana na mafanikio tuliyoyapata. Maelezo niliyoyatoa ya
kila sekta na mengine ambayo sikuweza kuyaelezea kwa sababu ya muda,
tunayatekeleza kwa ufanisi kwa kuzingatia mpango wetu wa Dira ya
Maendeleo ya Mwaka 2020, MKUZA II, Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya
mwaka 2010/2015 na Malengo ya Milenia.
Napenda niitumie nafasi hii niwashukuru
na niwapongeze Makamu wa Rais wote wawili, ambao ndio Wasaidizi na
Washauri wangu wakuu; Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa
Kwanza wa Rais na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa
Rais. Ninakushukuruni sana kwa ushauri wenu mnaonipa na mnavyonisaidia.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Namalizia hotuba yangu kwa kutoa
shukurani zangu tena kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, viongozi mbali mbali mliohudhuria, wageni
wetu wote na Mabalozi wa Nchi za Nje. Vile vile, natoa shukurani zetu
za dhati kwa Washirika wetu wa Maendeleo wa ndani na nje ya nchi
wakiwemo nchi rafiki, jumuiya za kimataifa, Asasi za kiraia na sekta
binafsi kwa michango yao muhimu katika maendeleo yetu. Kwa hakika
michango yenu ni kichocheo kikubwa cha utekelezaji wa mipango yetu ya
maendeleo.
Kadhalika, natoa shukurani zangu kwa
wananchi wote kwa mahudhurio makubwa katika Sherehe za Miaka 51 ya
Mapinduzi Matukufu zilizofana sana. Shukurani zangu vile vile, nazitoa
kwa kwa vikosi vyote vilivyoshiriki kuandaa gwaride la kuvutia,
wanafunzi waliofanya halaiki ya kupendeza, waandishi wa habari
walivyofanya kazi kubwa ya kuzitangaza sherehe hizi. Vile vile,
shukrani zangu nazito kwa vikundi vya utamaduni vilivyotuburudisha na
wananchi wote walioshiriki kuzifanikisha sherehe zetu za kuadhimisha
Miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964.
Aidha, natoa pongezi kwa Kamati ya
Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa inayoongozwa na Makamu
wa Pili wa Rais, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi kwa kazi nzuri ya walioifanya
ya kuandaa na hatimae kuzifanikisha sherehe za leo na zile
zilizotangulia kwa mafanikio makubwa. Hongereni Sana.
Ndugu wananchi
Leo nataka kutangaza rasmi kwamba
kuanzia mwaka ujao wa fedha 2015-2016 unaoanza Julai mwaka huu
uchangiaji katika elimu ya msingi utaondoshwa wazee na wazazi
hawatatakiwa tena watoe mchango wowote. Fedha hizo sasa zitachangiwa na
kutolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa hivyo elimu ya msingi
itakuwa bila ya malipo. Uwamuzi huu una lengo la uwamuzi wa Serikali wa
kutoa elimu bure kama ilivyotangazwa na Marehemu Mzee Abeid Amani
Karume mnamo tarehe 23 Septemba mwaka 1964. Kuhusu elimu ya Sekondari,
Serikali itaendelea kugharamia mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne
pamoja na mitihani ya Kidato cha Sita, wazee hamtatakiwa kugharamia hata
senti moja. Mambo mengine yanayohusu gharama za elimu ya Sekondari
tutayatangaza hapo baadae
Nakutakieni viongozi, wageni waalikwa na
wananchi nyote kheri na baraka ya mwaka mpya wa 2015. Namuomba
Mwenyezi Mungu aturudishe sote nyumbani salama.
MAPINDUZI DAIMA
MUNGU IBARIKI ZANZIBAR
MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRIKA
MUNGU IBARIKI ZANZIBAR
MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRIKA
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Post a Comment