Dar es Salaam. Wakati Kampuni ya kufua umeme ya
Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) chini ya uongozi wa Kampuni ya
Pan African Power Solutions (T) Ltd (PAP), ikitangaza kupunguza bei ya
umeme kwa asilimia 20 baada ya kufanya marekebisho makubwa ya injini za
mtambo wake, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema halina taarifa
yoyote.
“Tunatarajia hatua za upanuzi kwenda haraka
kuhakikisha kuwa IPTL inatoa huduma bora ya uhakika na nafuu kwa Taifa
hili. Ningependa kutoa shukrani zangu kwa uongozi wa Tanesco kwa
kukubali umeme unaozalishwa na IPTL,” ilisema taarifa iliyotolewa na
Mwenyekiti Mtendaji wa IPTL, Harbinder Singh Sethi.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco,
Felchesmi Mramba aliliambia gazeti hili jana kuwa hana taarifa hizo na
kwamba kama kuna punguzo lolote, IPTL ilitakiwa kulijulisha rasmi.
“Taarifa hizi tunazisikia tu ila hatujaelezwa
rasmi. Sisi tunachokifanya sasa ni kutekeleza maazimio yaliyotolewa na
Bunge,” alisema Mramba.
Ingawa Mramba hakufafanua utekelezaji huo, katika
azimio lake la saba kati ya manane, Bunge liliazimia kwamba Serikali
iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na
kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za shirika hilo.
Hata hivyo, Serikali kwa kupitia Rais Jakaya
Kikwete imesema hilo likifanywa na Serikali pekee linaweza kuwatisha
wawekezaji kuja nchini.
Hivi karibuni baada ya Bunge kutoa maazimio yake
yaliyotokana na Ripoti ya Kamati yake ya Hesabu za Serikali (PAC), Sethi
alikaririwa na gazeti hili akisema anafikiria mara mbilimbili kuendelea
kuwekeza nchini.
Punguzo la IPTL
IPTL ilieleza kuwa ilifanya marekebisho ya mitambo
hiyo kwa saa 36,000 kazi ambayo ilikamilika mwaka jana, huku ikitangaza
pia kuwa bei yake ya umeme inatarajiwa kushuka zaidi kulingana na
kushuka kwa bei ya mafuta mazito.
IPTL pia ilisema marekebisho hayo yaliyotumia
zaidi ya Dola za Marekani 25 milioni, yameiwezesha mitambo yake kuwa
katika nafasi nzuri ya kuzalisha umeme wa uhakika kwa kufikia megawati
100 na kuingiza kwenye Gridi ya Taifa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Sethi,
kampuni hiyo imepunguza bei ya umeme wake inaoitoza Tanesco na sasa
utakuwa chini ya bei ya awali iliyokokotolewa ya senti 23 Dola za
Marekani kwa kilowati ikiwa na maana kwamba bei hiyo imepungua kwa senti
4.6 za Dola.
إرسال تعليق