Ivo: Nilibeba ‘zigo’ la lawama

Dar es Salaam. Kipa wa Simba, Ivo Mapunda amesema kocha Goran Kopunovic alimpa jukumu zito la kumtaka akadake penalti kama angeshindwa angebebeshwa lawama zaidi.
Ivo hivi karibuni alitangaza kutokata golini katika mchezo wowote wa timu hiyo, lakini juzi Jumanne alijikuta akiingia kuchukuwa nafasi ya kipa Peter Manyika katika dakika ya 90, na kufanikiwa kuibuka shujaa baada ya kupangua penalti ya mwisho ya Mtibwa Sugar na kuipa Simba ushindi wa penalti 4-3 uliowapa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi juzi kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Ivo alisema ulikuwa ni uamuzi mgumu kwake kwani angeshindwa kufanya vizuri angebebeshwa lawama zaidi, lakini alishindwa kumkatalia kocha kwani lilikuwa ni jambo la ghafla.

“Nashukuru nimewathibitishia uwezo wangu, Manyika ni kipa mzuri na amedaka vizuri na ataendelea kuwa bora, ni kweli sitaki kupangwa nataka nikae benchi ila kwa sasa sitaki kuzungumza zaidi,” alisema Ivo.

“Kocha alinipa jukumu zito sana, kila mmoja alikuwa akiniangalia mimi nitafanya nini, nililitambua hilo tangu kocha aliponiambia nijiandae kuingia hivyo sikutaka kumwangusha,” alisema Ivo.

Alisema hakutaka kufanya makosa katika mchezo huo kwani alitambua madhara yake yatakuwaje baadae kama angeshindwa kufanya kile timu ilikihitaji hivyo aliingia uwanjani akijiamini na kuwa tayari kwa lolote.

“Namshukuru Mungu nimeweza kufanya kile kilichotarajiwa na timu na mashabiki wetu, niwapongeze pia wachezaji wenzangu kwa jitihada walizofanya dakika zote 90 katika mechi ile ngumu na hatimaye tumetwaa kombe hili,” alisema Ivo.
Akizungumzia juu ya kushindwa kumpa mpira kiungo wa Mtibwa Sugar, Ibrahim Rajabu ‘Jeba’, Ivo alisema kuwa “mpira una mambo mengi hasa unapotaka ushindi, nilifanya makusudi kwa lengo la kumtoa mchezoni na kweli alikubali kutoka mchezoni ndio maana alipiga mpira uliogonga kwenye mwamba vinginevyo angefunga, yote hiyo ni kuifanya Simba ishinde,”.

Ukiachana na Jeba wengine waliopiga penalti kutoka Mtibwa Sugar ni Vicent Barnabas ambaye mpira wake ulidakwa wakati Ally Lundenga, Shaaban Nditi na Ramadhan Kichuya wakipata.
Penalti za Simba zilipigwa na Awadhi Juma, Hassan Kessy, Hassan Isihaka, na Dan Sserunkuma huku Shaaban Kisiga akikosa.

Post a Comment

Previous Post Next Post