Jeshi
la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania linapenda kutoa taarifa kwa wananchi
na Vyombo vya Habari kuhusu mgogoro wa eneo la TONDORONI lililopo katika
Wilaya ya Kisarawe kama ilivyokaririwa na baadhi ya Vyombo vya Habari
hapa nchini.
Taarifa
zilizotolewa na kukaririwa na baadhi ya Vyombo vya Habari kwamba
Wanajeshi wametumia nguvu kuwatoa wananchi eneo la TONDORONI na baadhi
yao kudai kupotelewa na mali zao siyo za kweli na ni za kuwapotosha
wananchi kwa sababu wananchi hao walitaarifiwa kuondoka kupitia uongozi
wa Wilaya na uongozi wa Vijiji vya MLOGANZILA na KILUVYA B. Aidha,
walipewa muda wa kutoa vitu vyao na wao kuondoka.
JWTZ
linapenda kuwahakikishia wananchi kuwa hatua ya kuwaondoa wananchi
wavamizi kutoka katika eneo la kambi ya Jeshi kwa uangalifu, umakini na
kulikuwa na usimamizi wa hali ya juu na hakuna mali ya mwananchi
iliyoporwa kama ilivyodaiwa.
Ifahamike
kwamba; Jeshi linaona ni bora lilaumiwe kwa kuwaondoa wananchi
waliovamia maeneo hatarishi ya jeshi ambayo hutumika katika mafunzo
yanayohusisha risasi za moto, zana hatari za kijeshi na mabomu ambayo
wakati mwingine hulipuka baada ya muda fulani kupita badala ya kuwaacha
wakae katika maeneo hayo kutokana na sababu za kisiasa au ushabiki
mwingineo na hivyo kuwa katika hatari ya kuweza kuumia vibaya au
kupoteza maisha yao na mali zao.
Pia ni vema tukajua historia ya tatizo hili.
Mnamo
mwaka 1978 eneo linalojumuisha vijiji vyaMLOGANZILA na KILUVYA B na
kilichokuwa kijiji chaTONDORONI lilichukuliwa na Serikali kwa ajili ya
matumizi yaJWTZ. Baada ya maamuzi hayo Kikosi cha JWTZ
kilihamiaTONDORONI mwaka 1981na kukalia eneo la hekta 4197.
Serikali ililipima eneo la TONDORONI kisheria mwaka 1984 na eneo lote liliwekewa mawe ya mipaka.
Baada
ya hapo, Serikali ilifanya tathimini ya malipo kwa awamu mbili. Awamu
ya kwanza ilikuwa mwaka 1987/88na wakati huo kulikuwa na wananchi
wapatao 1,508. Awamu ya pili ilifanyika 1992/93 ambayo ilijumuisha
tathmini ya nyumba na majengo ambapo wananchi wengine 955 walifanyiwa
tathimini.
Kufuatia tathimini iliyofanyika malipo yalikuwa kama ifuatavyo:
Mwaka 1996 malipo yalifanyika kwa barua kumbukumbu Na. FE 98/371/01/73 ya tarehe 11 Juni 2003.
Malipo
mengine yalifanyika mwaka 2002 na 2006. Baada ya Malipo hayo, mengine
tena yalifanyika mwaka 2012 kutokana na kesi ya madai Na. 144/1996. Kwa
hiyo madai ya msingi ya wananchi yalishalipwa na sheria ya uchukuaji
ardhi imetekelezwa kikamilifu.
Hata
hivyo, mwaka 2005 baadhi ya wananchi wachache walifungua kesi Na.
78/2005 ambayo baadae ilifutwa na mahakama. Tarehe 10 Dec 2013 M/kiti
wa kamati ya Ulinzi ya Wilaya Kisarawe alikwenda eneo la
TONDORONIkuwasomea wananchi maamuzi ya mahakama akiandamana na
mwanasheria wa Wilaya ya Kisarawe.
Pamoja
na taarifa hizo kupitia uongozi wa Wilaya na uongozi wa Vijiji vya
MLOGANZILA na KILUVYA B. wananchi wachache wameendelea na kazi
zinazochangia kuharibu mazingira hasa ukataji wa miti, uchomaji wa mkaa
na kuwasha moto mara kwa mara hali inayotishia usalama wa kambi na wa
wananchi wenyewe ikizingatiwa kwamba hili ni eneo la mafunzo ambapo
risasi za moto hutumika sambamba na zana zingine hatari za kijeshi
katika eneo hilo.
Wananchi
waliowengi wanajua ukweli kuwa eneo laTONDORONI linamilikiwa kihalali
na JWTZ, lakini wapo wananchi wachache wamekuwa wakiingia kinyemela
katika eneo hilo na kufanya ujenzi mpya usiku licha ya jitihada
mbalimbali zinazofanyika kuwaelimisha na kuwashauri kuwa waache tabia
hiyo ya kulivamia eneo hilo la Jeshi, jambo ambalo hugunduliwa na
kuzuiliwa uendelezaji wa ujenzi huo.
Jeshi
linawataka wananchi wachache wanaovamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya
matumizi ya kijeshi; kutambua kuwa kufanya hivyo ni kosa la kisheria
lakini pia kwa mara nyingine tena kuendelea kuwakumbusha wananchi kuhusu
madhara yanayoweza kuwapata wananchi wanaovamia maeneo ya Jeshi na
kujenga katika maeneo hayo.
Jeshi
litaendelea kushirikiana na wananchi wema na kuheshimu mipaka iliyopo
baina ya makambi yake na maeneo ya wananchi lakini pia litaendelea
kuwaondoa wale wachache wanaojenga katika maeneo yake kinyume cha
utaratibu.
Imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Mahusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
S.L.P 9203, Dar es Salaam, Tanzania.
Kwa Mawasiliano zaidi: 0783-309963
Post a Comment