LIWALE JIMBO LENYE MATATIZO LUKUKI


Liwale ni moja kati ya wilaya 6 za Mkoa wa Lindi Kusini mwa Tanzania. Upande wa Kaskazini inapakana na Mkoa wa Pwani, Mashariki inapakana na Wilaya ya Kilwa, Kusini inapakana na Wilaya ya Ruangwa na Magharibi inapakana na Mkoa wa Morogoro.
Mbunge wa Liwale Faith Mitambo kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Pia Liwale ni jimbo la uchaguzi linaloongozwa na Mbunge Faith Mitambo kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Siku kadhaa zilizopita, Uwazi lilichanja mbunga mpaka kwenye jimbo hilo ambalo linafikika kwa tabu kutokana na miundombinu mibovu ya barabara.
Uwazi lilifanikiwa kuzungumza na baadhi ya wananchi wa Kata za Barikiwa, Kiang’ara, Kibutuka, Liwale Mjini, Mkata, Mangirikiti, Liwale ‘B’, Mpigamiti, Ngongowele, Mlwembwe na Mkutano ambazo wakazi wake wengi ni wa kabila la Wangindo na makabila mengine.
MATATIZO YA WANANCHI
1. Miundombinu mibovu
Said Makubi, mfanyabiashara wa Liwale Mjini, alikuwa na haya ya kusema: “Barabara za kuja huku Liwale ni mbaya sana, kama sisi wafanyabiashara tunapata sana shida kwa sababu tunalazimika kufuata bidhaa mbali, nyingi zinaharibikia njiani kutokana na ubovu wa barabara.
“Pia mahali ambapo ungeweza kusafiri kwa muda mfupi, unashinda kutwa nzima barabarani, nauli zinakuwa kubwa yaani ni kero tupu. Tunaomba mbunge atimize ahadi zake za kutujengea barabara nzuri.”
2. Bei ndogo ya korosho
Wakazi wengi wa Liwale wanategemea zao la korosho kuendesha maisha yao, hata hivyo, malalamiko ya wengi ni kwamba bei ya zao hilo inazidi kuporomoka kila kukicha, huku vyama vya ushirika navyo vikizidi kuwadidimiza.
“Kila mwaka bei ya korosho inazidi kushuka, tena afadhali tungekuwa tunalipwa fedha zote kwa mkupuo lakini tunalipwa kwa awamu, mara ya kwanza mnapewa kidogo na kupeleka korosho ghalani, zikiuzwa ndiyo mnamaliziwa tena fedha zilizobaki. Mwaka 2013 wakulima walikasirika kutokana na unyonyaji huu wa bei mpaka wakamchomea mbunge nyumba yake. Tunamuomba mheshimiwa atusaidie, tulimchagua ili atusemee matatizo yetu, mbona anatusahau?” Abdallah Mwera, mkazi wa Liwale B aliliambia Uwazi.
3. Huduma mbovu za kijamii
Hamduni Nangwale, mkazi wa Liwale, naye alifunguka: “Huduma za kijamii huku kwetu ni mbaya sana, yaani utafikiri tunaishi kisiwani. Dawa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Liwale hakuna, ukienda unaambiwa ukanunue kwenye maduka ya watu binafsi na kama huna fedha unaweza kufa hata kwa malaria.
Serikali yetu mbona imetusahau? Mbunge mbona hashughulikii matatizo yetu?”
Naye Mwantumu au mama wawili, mkazi wa Barikiwa, alilalamikia ukosefu wa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya kila siku, na kueleza kuwa wakati mwingine wanalazimika kunywa na kupikia maji machafu kutokana na kukosekana kwa maji ya bomba.
“Tunaomba mbunge atimize ahadi ya kutuletea maji na kutuchimbia visima kama alivyoahidi wakati akiomba kura.”4. Mila na desturi za kizamaniAnord Maliyela ambaye ni mwalimu wa shule moja ya msingi jimboni humo, yeye alilalamikia wakazi wa Liwale kuendekeza mila zilizopitwa na wakati.
“Unakuta wazazi wanawatoa watoto shuleni na kuwapeleka kuchezwa ngoma za unyago wakati wenzao wakiendelea na masomo. Wakiwa huko wanafundishwa mambo ya kikubwa kiasi kwamba hata wakirudi shuleni, akili zao zinakuwa zinawaza kuolewa tu hivyo wanashindwa kuzingatia masomo. Naomba serikali iingilie kati suala hili,” alisema.
Matatizo mengine yaliyobainishwa ni uhaba wa walimu hasa wa masomo ya sayansi, uhaba wa wauguzi katika sekta ya afya, uhaba wa madawati na madarasa, umaskini uliokithiri na ukosefu wa ajira kwa vijana.
MBUNGE APIGA CHENGA KUTOA MAJIBU
Katika hali isiyo ya kawaida, mbunge wa jimbo hilo, Faith Mitambo, kwa nyakati tofauti alipotafutwa na Uwazi kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa kero za wananchi, alikuwa akitoa sababu mbalimbali.
“Sipo jimboni, nipo Arusha kwenye mkutano, nitakupigia baadaye,” alisema mbunge huyo alipotafutwa kwa mara ya kwanza. Hata alipotafutwa tena baadaye, hakupokea simu yake. Kesho yake alipopigiwa, alipokea na kumwambia mwandishi kwamba atampigia baadaye ingawa hakufanya hivyo.
Siku mbili baadaye, mbunge huyo alitafutwa tena lakini majibu yake yalikuwa yaleyale: “Nitakupigia baadaye” au “nipo kwenye kikao.” Mpaka Uwazi linakwenda mitamboni, bado mbunge huyo aliendelea kukataa kutoa ushirikiano.Uwazi linaendelea kumtafuta mbunge huyo na atakapopatikana, atatolea ufafanuzi kero zilizoelezwa na wananchi waliomchagua.
*  *  *
Wiki kadhaa zilizopita, Gazeti hili lilichapisha kero za wananchi wa Jimbo la Temeke lakini mbunge wa jimbo hilo, Abbas Mtemvu hakuweza kupatikana kuzijibu. Jitihada za kumtafuta zinaendelea na atakapopatikana, atatoa majibu kupitia ukurasa huu- Mhariri

Post a Comment

أحدث أقدم