Tarehe 13/01/2015 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa
chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake wa Taifa Dr. Jakaya Mrisho Kikwete
ilifanya kikao chake cha kawaida cha siku moja Kisiwandui Mjini
Zanzibar. Pamoja na mambo mengine baadhi ya mambo yaliyojadiliwa na
Kamati Kuu ni pamoja na:-
1. SAKATA LA AKAUNTI YA ESCROW
Chama Cha
Mapinduzi kimesikitishwa sana na sakata hili. Baada ya kulijadili kwa
muda mrefu na kwa kina Kamati Kuu imeamua yafuatayo:-,
i).Pamoja na yale ambayo yameshatekelezwa na serikali, Kamati Kuu
imeitaka serikali na vyombo vinavyohusika kuendelea kutekeleza maazimio
ya bunge juu ya swala hilo.
ii). Kamati Kuu imewataka wote wanaopewa dhamana wajenge utamaduni wa
kuwajibika kwa dhamana zao,na wasipowajibika waliowapa dhamana wachukue
hatua za kuwawajibisha.
iii).Aidha Kamati Kuu imeiagiza Kamati Ndogo ya Maadili kuchukua
hatua za kimaadili kwa wale wote waliohusika na ukiukwaji wa maadili
kwenye sakata la Escrow na wako kwenye vikao vya maamuzi vya Chama.
Kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili kitafanyika tarehe 19/01/2015 kwa
ajili ya utekelezaji wa agizo hilo.
2. WALIOPEWA ADHABU KWA KUKIUKA MAADILI YA CHAMA
Itakumbukwa kuna makada sita wa CCM walipewa adhabu kwa kuhusishwa na
ukiukwaji wa maadili kwenye mchakato wa kutaka kuteuliwa na CCM kugombea
urais, watamaliza muda wa adhabu zao mwezi wa pili mwaka 2015.
Baada ya muda wa adhabu zao kuisha, itafanyika tathimini kuona kama
walizingatia mashariti ya adhabu zao. Na kama kuna ambao watakutwa
hawakuzingatia mashariti ya adhabu zao wataongezewa adhabu.
3. SOKO LA MAHINDI
Kamati Kuu imepokea taarifa
ya mwenendo wa soko la mahindi nchini. Baada ya tathimini na uchambuzi,
pamoja na kazi iliyofanywa na serikali, Kamati Kuu imeiagiza serikali
kuangalia upya mfumo unaotumiwa na Hifadhi ya Taifa ya Chakula
(NFRA)katika ununuzi wa mahindi, ili unufaishe zaidi wakulima badala ya
utaratibu wa sasa ambao kwa kiasi kikubwa unanufaisha zaidi mawakala
badala ya wakulima moja kwa moja.
4. RATIBA YA VIKAO VYA CHAMA
Kamati Kuu
imepitisha ratiba ya shughuli mbalimbali za Chama kwa mwaka 2015.Aidha
ratiba ya mchakato wa kuwapata wagombea wa CCM ndani ya dola utapangwa
na vikao vijavyo vya Chama.
Nape Moses Nnauye
CCM Secretary for Ideology & Publicity
Post a Comment