MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Kazi imewataka wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kurudi kazini, huku ikiagiza mamlaka hiyo kutowakata fedha wafanyakazi hao katika kipindi chote cha mgomo.
Licha
ya Mahakama hiyo kutoa huku ya kuwataka kurudi kazini, wafanyakazi hao
wamesema hawatarudi kazini mpaka watakapolipwa mishahara yao yote pamoja
na kuonana na Waziri wa Uchukuzi Dk Harisson Mwakyembe ili kujadiliana
naye kuhusu hatma ya Tazara pamoja na maisha ya wafanyakazi wake, kwa
madai kuwa wamechoshwa na kufedheheshwa.
Hukumu
hiyo ya kesi namba mbili ya mwaka huu ilitolewa juzi usiku na Jaji wa
Mahakama hiyo, Iman Aboud, baada ya wafanyakazi hao kusota siku nzima
kusubiri hukumu hiyo.
Jaji
Aboud alisema kwa mujibu wa kifungu namba 94 (1) (f) cha sheria ya
Ajira na Mahusiano Kazini mgomo huo ni batili, hivyo kutoa amri kwa
wafanyakazi hao kurudi kazini.
“Mahakama imezuia moja kwa moja kwa wafanyakazi kufanya migomo iliyo kinyume cha sheria,” alisema Jaji Aboud.
Aidha,
Mahakama imemtaka mwajiri kutokata fedha yoyote katika kipindi chote
cha mgomo wa wafanyakazi hao kutokana na kitendo cha kukaa miezi mitano
bila kuwa na mshahara kimetosha.
Kesi
hiyo ilifunguliwa na Menejimenti ya Tazara kuiomba Mahakama hiyo kutoa
amri kuwa mgomo huo ulioungwa mkono na Katibu Mkuu wa Trawu, kuwa ni
batili na pia kuzuia moja kwa moja migomo inayofanywa na wafanyakazi hao
kinyume cha sheria.
Tamko
la wafanyakazi hao la kutorudi kazini, lilitolewa na Kaimu Mwenyekiti
wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli nchini (Trawu) Kanda ya Dar es Salaam,
Yassin Mleke ambapo alisema, uamuzi huo ni wafanyakazi wote kuanzia Dar
hadi Tunduma, mkoani Mbeya.
Kwa
mujibu wa Katibu Mkuu wa Trawu, Erasto Kihwele chama hicho kinasikitika
kuona watu ambao ‘wamekufa’ wanatakiwa kurudi kufanya kazi.
“Mwajiri
alimshitaki Katibu Mkuu kwa kuhamasisha mgomo ambao haujafuata sheria
na tunaamriwa watu ambao tayari tumekufa kurudi kazini. “Mheshimiwa Jaji
kwa mamlaka aliyopewa ametuamuru turudi kazini kuanzia leo Januari 16,
mwaka 2015 (jana) kwa sababu mgomo wetu sio halali,” alisema Kihwele.
Awali
akizungumza na wafanyakazi hao waliokusanyika kusikiliza kilichojiri,
Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Hezron
Kaaya alisema, kuwa wafanyakazi hao wamekuwa wavumilivu lakini
wanaonekana kuvunja sheria kwa kudai haki yao.
Hata
hivyo alitaka wafanyakazi hao kutotishika kwa kuwa shirikisho hilo
limeshachukua jambo hilo, huku akieleza kuwa siku saba walizotoa awali
zimeisha wametoa siku tano nyingine ambapo baada ya siku hizo watatoa
tamko la kutikisa nchi.
Mwenyekiti
wa Trawu Taifa, Mussa Kalala alisema, mpaka sasa barua iliyopelekwa kwa
Waziri kwa ajili ya kumuomba aje kukutana na wafanyakazi hao haijapata
majibu, pia kusisitiza chama hicho hakina kauli binafsi bali kina kauli
ya wafanyakazi.
Jana abiria wengine waliokuwa wasafiri kwa treni hiyo kwenda Bara walishindwa kusafiri na kuishia kurudishiwa nauli zao.
Wakati
huo huo Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), limelaani
kitendo cha wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia
(TAZARA) kutolipwa mishahara yao kwa muda wa miezi sita na kutoa siku
tano kwa menejimenti ya mamlaka hiyo kuhakikisha inawalipa wafanyakazi
hao mishahara yao.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa
TUCTA, Hezron Kaaya alisema kutokana na wafanyakazi hao kutolipwa
mishahara yao walishindwa kwenda kazini kwa sababu hawakuwa na nauli
lakini kitendo hicho kikatafsiriwa kuwa ni mgomo.
Alisema
tatizo hilo la mishahara katika mamlaka hiyo limedumu kwa miaka kumi
sasa hivyo linatakiwa kufikia mwisho na kuwataka wafanyakazi wote
waungane katika hilo.
إرسال تعليق