*Ni kuhusu sakata la Akaunti ya Escrow
OFISI ya Katibu Mkuu Kiogonzi (KMK), imeanza kazi ya uchuguzi dhidi
ya Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Eliakim Maswi aliyesimamishwa
Desemba 23, mwaka jana kupisha uchuguzi dhidi yake, kama ilivyoelekezwa
na Rais Jakaya kikwete.
Taarifa iliyopatikana Ikulu jana, imesema tayari watu walioteuliwa na
Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, wameanza kazi hiyo Januari 6, mwaka
huu na wanatarajia kumaliza kazi hiyo mapema iwezekanavyo.
“Ni kweli uchuguzi ulianza Januari 6, mwaka huu ukiwa na lengo la
kujiridhisha kama kuna mahali Katibu Mkuu huyo alihusika katika utendaji
wake,” alisema Katibu Mkuu Kiogozi, alipozungumza na mwandishi wa
habari hizi ofisini kwake, jana.
Ombeni alisema jukumu hilo ni la kujiridhisha kama kweli mtumishi
huyo wa umma alihusika katika kufanikisha utoaji fedha za la Akaunti ya
Escrow, kama ilivyopendekezwa na Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Bunge
(PAC), mwaka jana.
Alisema kisheria,pamoja na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Frederick
Werema, kukiri ndani ya Bunge kuwa, jambo lililotokea abebeshwe yeye,
lakini kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, lazima ufanyike
uchuguzi na kujiridhisha.
Alisema kutokana na katibu huyo kuwajibika kwake, ni vema suala hilo
likawekwa wazi zaidi, kuliko kukurupuka kutoa uamuzi ambao baadaye
unaweza kubainika kuwa si sahihi.
“Naomba watu walioteuliwa tuwaache wafanye kazi yao na wakituletea
ripoti yao, tukiipitia na kubaini ukweli ndani yake, tutatoa uamuzi,”
alisisitiza.
Alipoulizwa kama uchuguzi uliofanywa na Bunge kama haukutosheleza
kumchukulia uamuzi, Ombeni alisema kiutaratibu mihimili hiyo ni tofauti,
hivyo Bunge pekee haliwezi kuhukumu au kumchukulia hatua bila upande
mwingine kujiridhisha makosa yake.
“Upande wa Serikali una taratibu zake kwa watumishi wa umma, kama
vile maadili kwa viongozi na pindi wanapobainika na makosa, ndipo adhabu
hufuata,” alisema.
Balozi Sefue alichukua hatua hiyo kwa mujibu wa Kifungu 4(3) (d) cha
Sheria ya Utumishi wa Umma, Na. 8 ya mwaka 2002 (kama
ilivyorekebishwa),ambapo ndiye mamlaka ya nidhamu kwa watumishi wa umma
wanaoteuliwa na rais, wakiwemo makatibu wakuu.
Badala yake, Balozi Sefue alimkaimisha kwa muda Naibu Katibu Mkuu,
Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava, nafasi ya Katibu
Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, hadi uchunguzi dhidi ya Maswi
utakapokamilika.
“Kuhusu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa vile ni
mtumishi wa umma, anatawaliwa na sheria na kanuni za utumishi wa umma,
hivyo nimeelekeza mamlaka kuchunguza tuhuma zake, na ikibainika ana
makosa hatua za kinidhamu zitachukuliwa.”
Maswi, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Werema, Waziri wa Nishati na
Madini, Sospeter Muhongo na aliyekuwa wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Anna Tibaijuka, walituhumiwa wakati wa kikao cha Bunge
kilichopita kuhusika Akaunti ya Tegeta Escrow.

Post a Comment