MABINGWA mara mbili wa Tanzania, 1999 na 2000, Mtibwa Sugar wamewatoa
kileleni mwa msimamo mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara, Azam
fc baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na wenyeji JKT Ruvu katika mchezo
uliomalizika jioni hii uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es salaam.
Azam
walirejea kileleni jana baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Stand
United uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga, ambapo walifikisha pointi 17
na magoli 11 ya kufunga kufuatia kushuka dimbani mara 9.
Kutokana
na Mtibwa Sugar kuvuna pointi moja, wamefikisha pointi 17 sawa na Azam,
lakini wamewazidi wakali hao wa Chamazi kwa magoli ya kufunga kwani sasa
wametikisa nyavu mara 12 katika mechi 9 walizokipiga.
JKT Ruvu nao wamefikisha pointi 17 katika nafasi ya tatu kutokana na kuwa na magoli 11 katika mechi 11 walizocheza.
Katika
mechi ya leo, JKT Ruvu waliandika bao la kuongoza katika dakika ya 7’
kupitia kwa mshambuliaji mwenye uchu wa magoli, Samuel Kamuntu
akimalizia mpira uliotemwa na kipa Said Mohammed.
Mtibwa
walishindwa kutumia nafasi nzuri waliyopata katika dakika ya 13’ ambapo
Musa Hassan Mgosi alipata pasi kutoka kwa Ame Ally katika eneo la hatari
na kuingiza krosi nzuri, lakini Ally Shomari alipaisha mpira juu ya
lango.
Coastal Union wametoka suluhu dhidi ya Polisi Morogoro uwanja wa CCM Mkwakwani
JKT Ruvu
waliendelea kufika langoni kwa Mtibwa kutokana na nidhamu ndogo ya
walinzi wa Wakata Miwa na katika dakika ya 25’ iliingizwa kona maridadi
na ikatokea piga nikupige langoni mwa vijana wa Manungu na Ally Bilal
akazamisha mpira nyavuni, lakini mwamuzi alipuliza kipyenga kuashiri
ameotea.
Mpaka
dakika hiyo tayari JKT Ruvu walikuwa wamepata kona tatu wakati Mtibwa
hawakupata kona yoyote, kitendo kilichodhihirisha kuwa wenyeji walifika
zaidi langoni kwa mpinzani wao.
Bilal
alipata nafasi nzuri katika dakika ya 32’ kufuatia mabeki wa Mtibvwa
kudhani ameotea, akapiga shuti lililopanguliwa na kipa Mohammed.
Mtibwa
waliendelea kucheza chini ya kiwango hususani safu ya ulinzi na dakika
ya 33’, kocha Mecky Mexime akalazimika kumtoa Dickson Daudi na nafasi
yake kuchukuliwa na Ramadhani Kichuya.
Dakika ya
37’ David Charles Luhende aliingiza kona kutoka winga ya kushoto, Ame
Ally alipiga kichwa baada ya kuwachekecha mabeki wa JKT Ruvu na
kuzamisha mpira nyavuni akiisawazishia Mtibwa.
Mbali ya goli hilo, mashuti ambayo yalilenga lango mpaka dakika 40’ yalikuwa matatu kwa JKT Ruvu na mawili kwa Mtibwa Sugar.
Dakika ya
44’ iliingizwa kona na Luhende, Ibrahim Rajab ‘Jeba’ alitumbukiza gozi
kimiani kwa mkono na mwamuzi Aman Paul kutoka Musoma Mara akamuonesha
kadi ya njano.
Mpaka dakika 45’ zinakamilika, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
JKT Ruvu walimiliki mpira kwa 52% dhidi ya 48% za Mtibwa Sugar.
Kipindi
cha pili kilianza kwa timu zote kucheza mpira wa taratibu na
kushambuliana kwa zamu, lakini Mtibwa Sugar walipata nafasi nyingi za
kufunga, ingawa washambuliaji wake Mudathiri Yasini, Ibrahim Rajab
‘Jeba’ na Ame Ally hawakuwa makini.
Dakika ya
72’ kama kawaida, Mgosi alikwenda benchi na nafasi yake kuchukuliwa na
Vicent Barnabas. Katika mechi nyingi wachezaji hawa wawili wamekuwa
wakibadilishana nafasi.
Katika dakika ya 78’ Abdallah Juma aliingia kuchukua nafasi ya Ame Ally ‘Baba Amina’
Mpaka dakika 90’ zinamalizika timu hizo mbili zimetoka sare ya bao 1-1.
Mechi
nyingine ya ligi kuu imepigwa uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga ambapo
Wagosi wa Kaya, Coastal Union wametoka suluhu (0-0) dhidi ya Polisi
Morogoro.
Kikosi
hicho cha Mkenya James Nangwa kilicheza soka kali na la kushambulia muda
mwingi, lakini vijana wa Adolf Rishard walikuwa imara kuzuia
mashambulizi hayo.
Coastal
Union wameonesha makali kiuchezaji, lakini bado wamekuwa na tatizo
katika nafasi ya ushambuliaji, hivyo kocha anatakiwa kurekebisha tatizo.
Kwa matokeo hayo Coastal Union wamefikisha pointi 12 wakati Polisi Moro wamefikisha pointi 15.
Chanzo:mpenja blog.
Post a Comment