MCHAKATO WA KATIBA: Watanzania wako njia panda kura ya maoni

Inashangaza sana kusema kuwa  mchakato wa Mabadiliko ya Katiba unaosubiri Kura ya Maoni miezi mitatu ijayo, umeacha mvurugano na mgawanyiko kuliko hapo awali. Muda ndiyo utakaothibitisha ukweli huu na hii haimaanishi hata kidogo kuidharau Katiba Inayopendekezwa.
Hata hivyo, utata wa kisheria ulionekana katika mchakato mzima umeacha maswali mengi yaliyotakiwa kutafutiwa majibu. Kuna mambo mengi ya kisheria yahusianayo na kura ya maoni ambayo yametuacha katika wakati mgumu kutokana na mgongano wa masuala ya kisheria yanayotegemeana.
Ukichunguza kwa makini mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, bila shaka utaungana nami kuwa kuna mtego na tupo katika wakati mgumu usio wa kawaida. Kabla sijaeleza mtego upo wapi, napenda nieleze maana ya mtego au kipindi cha wakati mgumu kwa Kiingereza “catch 22 situation”.
Nyaraka mbalimbali zinabainisha kuwa Joseph Heller alitumia neno hilo katika riwaya yake mwaka 1961 iliyoitwa “A catch 22.”   Hali hii hutokea pale mtu anapokuwa hawezi kuikimbia kutokana na taratibu au kanuni zinazokinzana.
Catch 22 mara nyingi huzaliwa kutoka katika sheria, kanuni, au taratibu ambazo mtu anatakiwa kuzifuata, lakini hana uwezo wa kudhibiti au kuziongoza kwa sababu kupingana nazo ndiko kukubaliana nazo.
Kwa mujibu wa kifungu cha 36(5) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba namba 83 ambacho naomba nikitengeneze upya, iwapo kura nyingi zilizopigwa zikasema ‘Hapana’  katika Kura ya Maoni ya Katiba Inaopendekezwa  basi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 itaendelea kutumika.
Kwa maana hiyo, kupitia sheria hii iwapo watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watapigia Katiba Inayopendekezwa kura ya hapana basi tutalazimishwa moja kwa moja kurudi katika Katiba ya mwaka 1977.
Kinachovutia zaidi kama kura zote zitasema ‘Ndiyo’ basi matokeo ya kura zilizopigwa yatakuwa yameamuliwa kwa misingi ya asilimia 50 ya jumla ya kura zilizopigwa Tanzania Bara na zaidi ya asilimia 50 Zanzibar na Katiba Mpya itakuwa imekubaliwa. Lakini kuna tofauti gani baina ya Katiba Inayopendekezwa na ile ya Mwaka 1977?
Swali hili ni la msingi siyo tu katika kuonyesha mtego ulipo, lakini pia kupitia misingi isiyokubaliwa na wengi na chama kama Katiba Inayopendekezwa ilivyopitishwa kwa mvutano mzito ambao baadaye ulileta mgawanyiko uliosababisha baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba kususia Bunge hilo.
Kwa maoni yangu huu ulikuwa ushahidi tosha wa mgawanyiko siyo tu kwa Wajumbe wa Bunge la Katiba, bali kwa nchi nzima kutokana na hoja kuwa wajumbe hao walikuwa wakiwakilisha wananchi wa Jamhuri ya Muungano. Mungu atuepushie mbali!
Hata hivyo, ukweli ni kwamba Katiba Inayopendekezwa imeongeza kitita cha vipengele vipya hususan vinavyohusiana na haki za binadamu katika rasimu ya mwisho na vipo katika Katiba ya mwaka 1977 kwa kufanyiwa mabadiliko kidogo.
Kwa maana hiyo, machaguo yaliyowekwa mezani kwa ajili ya watu kupigia kura wakati wa Kura ya Maoni ni kwamba aidha upigie ‘Ndiyo’ ili tuishie na maboresho ya Katiba ya mwaka 1977 au upigie ‘Hapana’  ili twende kwenye Katiba ya mwaka 1977 bila mabadiliko yoyote. Huu ni mtego.

Post a Comment

Previous Post Next Post