Inashangaza sana kusema kuwa mchakato wa Mabadiliko ya Katiba
unaosubiri Kura ya Maoni miezi mitatu ijayo, umeacha mvurugano na
mgawanyiko kuliko hapo awali. Muda ndiyo utakaothibitisha ukweli huu na
hii haimaanishi hata kidogo kuidharau Katiba Inayopendekezwa.
Hata hivyo, utata wa kisheria ulionekana katika
mchakato mzima umeacha maswali mengi yaliyotakiwa kutafutiwa majibu.
Kuna mambo mengi ya kisheria yahusianayo na kura ya maoni ambayo
yametuacha katika wakati mgumu kutokana na mgongano wa masuala ya
kisheria yanayotegemeana.
Ukichunguza kwa makini mchakato wa Mabadiliko ya
Katiba, bila shaka utaungana nami kuwa kuna mtego na tupo katika wakati
mgumu usio wa kawaida. Kabla sijaeleza mtego upo wapi, napenda nieleze
maana ya mtego au kipindi cha wakati mgumu kwa Kiingereza “catch 22
situation”.
Nyaraka mbalimbali zinabainisha kuwa Joseph Heller
alitumia neno hilo katika riwaya yake mwaka 1961 iliyoitwa “A catch
22.” Hali hii hutokea pale mtu anapokuwa hawezi kuikimbia kutokana na
taratibu au kanuni zinazokinzana.
Catch 22 mara nyingi huzaliwa kutoka katika
sheria, kanuni, au taratibu ambazo mtu anatakiwa kuzifuata, lakini hana
uwezo wa kudhibiti au kuziongoza kwa sababu kupingana nazo ndiko
kukubaliana nazo.
Kwa mujibu wa kifungu cha 36(5) cha Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba namba 83 ambacho naomba nikitengeneze upya, iwapo
kura nyingi zilizopigwa zikasema ‘Hapana’ katika Kura ya Maoni ya
Katiba Inaopendekezwa basi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
mwaka 1977 itaendelea kutumika.
Kwa maana hiyo, kupitia sheria hii iwapo watu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watapigia Katiba Inayopendekezwa kura ya
hapana basi tutalazimishwa moja kwa moja kurudi katika Katiba ya mwaka
1977.
Kinachovutia zaidi kama kura zote zitasema ‘Ndiyo’
basi matokeo ya kura zilizopigwa yatakuwa yameamuliwa kwa misingi ya
asilimia 50 ya jumla ya kura zilizopigwa Tanzania Bara na zaidi ya
asilimia 50 Zanzibar na Katiba Mpya itakuwa imekubaliwa. Lakini kuna
tofauti gani baina ya Katiba Inayopendekezwa na ile ya Mwaka 1977?
Swali hili ni la msingi siyo tu katika kuonyesha
mtego ulipo, lakini pia kupitia misingi isiyokubaliwa na wengi na chama
kama Katiba Inayopendekezwa ilivyopitishwa kwa mvutano mzito ambao
baadaye ulileta mgawanyiko uliosababisha baadhi ya wajumbe wa Bunge la
Katiba kususia Bunge hilo.
Kwa maoni yangu huu ulikuwa ushahidi tosha wa
mgawanyiko siyo tu kwa Wajumbe wa Bunge la Katiba, bali kwa nchi nzima
kutokana na hoja kuwa wajumbe hao walikuwa wakiwakilisha wananchi wa
Jamhuri ya Muungano. Mungu atuepushie mbali!
Hata hivyo, ukweli ni kwamba Katiba
Inayopendekezwa imeongeza kitita cha vipengele vipya hususan
vinavyohusiana na haki za binadamu katika rasimu ya mwisho na vipo
katika Katiba ya mwaka 1977 kwa kufanyiwa mabadiliko kidogo.
Kwa maana hiyo, machaguo yaliyowekwa mezani kwa
ajili ya watu kupigia kura wakati wa Kura ya Maoni ni kwamba aidha
upigie ‘Ndiyo’ ili tuishie na maboresho ya Katiba ya mwaka 1977 au
upigie ‘Hapana’ ili twende kwenye Katiba ya mwaka 1977 bila mabadiliko
yoyote. Huu ni mtego.

إرسال تعليق