Mgomo wa wafanyakazi Tazara yafaa sasa utafutiwe ufumbuzi

Kwa takribani wiki moja sasa, vyombo vya habari vya hapa nchini, vimetawaliwa na mgomo wa wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara).
Hadi kufikia jana, mgomo huo ulikuwa umeingia siku ya tano huku kukiwa na matumaini madogo ya madai ya wafanyakazi hao kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Wafanyakazi hao wanadai malimbikizo ya mishahara yao ya miezi mitano mfululizo.

Hali hiyo imewafanya watumishi hao wagome na zipo taarifa kwamba jana walikuwa wamesitisha kutoa huduma zote muhimu ukiwamo usafiri wa treni kutoka Dar es Salaam hadi Zambia.

Juzi, wafanyakazi hao kupitia Chama chao cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (Trawu), waliipa menejimenti ya Tazara siku saba kuhakikisha kwamba wanalipa madai hayo.

Mgomo huo umekuja baada ya makubaliano ya pamoja katika mkutano baina yao na uongozi Trawu Taifa na kumuomba Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kuzungumza nao ili kutoa tamko la hatma ya Tazara.

Mwenyekiti wa Trawu Mkoa wa Dar es Salaam, Yassin Mleke, aliliambia NIPASHE kuwa hakuna huduma yoyote inayoendelea katika mamlaka hiyo inayomilikiwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na ya Zambia kwa kuwa tatizo hilo limekuwa sugu.

Hii si mara ya kwanza kwa wafanyakazi hao kugoma kwani wamekuwa wakifanya hivyo mara kwa mara na chanzo kikubwa kikiwa ni kutolipwa mishahara yao kwa wakati.

Hakuna asiyefahamu umuhimu wa chombo hicho kwa uchumi wa taifa letu la Tanzania na kwa msingi huo, matatizo yake yanatakiwa yatafutiwe majawabu ya haraka.

Sisi tunapata huzuni kubwa tunapoona kwamba hadi jana mgomo huo ulikuwa ukiendelea na hivyo kuzidi kutishia uchumi wa Tanzania.

Tunajua kwamba kwa vyovyote vile, serikali inakuna kichwa kuhakikisha kwamba suala hilo linapatiwa ufumbuzi ili wafanyakazi hao wa Tazara, warejee kazini na kuendelea kulisukuma mbele gurudumu la maendeleo.

Hata hivyo, tunachoshangaa ni ukimya wa serikali kuhusiana na suala hilo kiasi cha kuwatia wasiwasi wafanyakazi wa mamlaka hiyo na hivyo kuendelea kugoma hali inayozidi kuzorotesha shughuli za shirika.

Msemaji wa Tazara, Conrad Simuchile, alisema menejimenti inaendelea kutafuta uwezekano wa kulipa malimbikizo ya wafanyakazi hao na ikiwezekana mishahara yote ya miezi mitano.

Kauli hii kwa hakika ni ya kutia moyo, lakini tulipenda kusikia serikali inasema nini kuhusiana na hili hasa kutokana na umuhimu wa mamlaka hii kwa uchumi wa Taifa.

Katika siku za nyuma ilipotokea migomo ya namna hii, mara kwa mara, tulimsikia Waziri wa Uchukuzi, Dk. Mwakyembe, akiingilia kati haraka na kutolea tamko la serikali.

Amekuwa akifanya hivyo akiwa jijini Dar es Salaam na wakati mwingine akiwa katika vikao vya Bunge mjini Dodoma.

Kwa kufanya hivyo ni dhahiri kwamba husaidia kuwapa wafanyakazi matumaini ya kuwa serikali yao inashughulikia matatizo yao.

Wafanyakazi wametoa siku saba ambazo zitaishia kesho kuhakikisha kwamba serikali inawalipa malimbikizo ya mishahara yao ya miezi mitano.

Tumewasikia wafanyakazi hao wakilalamika jinsi wanavyoishi maisha magumu kutokana na kutolipwa mishahara yao ya miezi mitano.

Tunaishauri na kuiomba serikali ilitazame tatizo la wafanyakazi hawa kwa jicho la huruma kwani kuishi na familia zao kwa miezi mitano bila mishahara, si jambo jema hata kidogo.

Kinachotakiwa kwa serikali, ni kuketi pamoja na wafanyakazi hao na kuzungumza nao ikibidi, waelezwe hali halisi ya shirika lao lakini pia wahakikishiwe njia mwafaka itakayotumika kuwalipa madai yao hayo.

Ni matarajio yetu kwamba serikali itafanya kila liwezekano kumaliza kero hii ya wafanyakazi ili warejee kazini na kuendelea kufanya kazi kwa maslahi ya Taifa.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم