Dar es Salaam. Wanachama 11 wa Chama cha
Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
wakikabiliwa na kesi ya kujeruhi, kuwatishia na kuwazuia maofisa wa
polisi kutekeleza majukumu yao.
Watu hao wanadaiwa kufanya vurugu kwa nyakati
tofauti wakati wa uapishwaji wa wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika
wilaya ya Kinondoni uolifanyika Januari 6, mwaka huu katika Hoteli ya
Landmark iliyopo Ubungo, Dar es Salaam, wakipinga kuwa baadhi ya
waliokuwa wakiapishwa hawakustahili.
Hali hiyo ilisababisha polisi kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya.
Akisoma hati ya mashtaka yanayowakabili washtakiwa
hao, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumain Kweka alidai jana kuwa
washtakiwa Sunday Urio (20), Kizito Damian (35), Joseph Samky (30),
Christant Luhilila (24), Karim Ally (40), Wilfred Ngowi (30) na Kinyaiya
Siriri (35) waliwatishia na kuwazuia maofisa wa Polisi kutekeleza
majukumu yao.
Kweka alidai, Januari 6, 2015 katika eneo la
Ubungo RiverSide, Wilaya ya Kinondoni, washtakiwa hao kwa pamoja
waliwatishia na kuwazuia maofisa wa polisi wasitekeleze majukumu yao.
Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka hayo,
waliyakana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo
umekwisha kamilika na wakaomba ipangwe tarehe kwa washtakiwa kusomewa
maelezo ya awali (PH).
Hakimu Mkazi, Devotha Kisoka aliwaambia washtakiwa
hao dhamana ipo wazi na kuwataka kila mshtakiwa kusaini hati ya dhamana
ya maneno ya Sh5 milioni pamoja na kuwa na wadhamini wawili.
Katika kesi nyingine, iliyosomwa mbele ya Hakimu
Mkazi, Janeth Kaluyenda washtakiwa Abdul Hamis (67), Mwanaharusi Salum
(42), Kizito Damian (35), Joseph Samky(30), Sunday Urio (30), Sandro
Carlos na Karim Ally wanakabiliwa na shtaka la kumjeruhi Juma Salum na
kumsababisha maumivu na majeraha. Wakili Kweka akishirikiana na Wakili
wa Serikali, Janeth Kitali walidai kuwa Januari 6, katika Hoteli ya
Landmark Wilaya ya Kinondoni walimjeruhi Juma Salum.
Ilidaiwa kuwa siku hiyo ya tukio washtakiwa hao
kwa pamoja walimpiga kwa kumrushia mawe na kumsababishia majeraha Salum
na kipigo hicho kilisababisha mkono wake wa kushoto kuvunjika.
Baada ya kusomewa shtaka linalowakabili,
washtakiwa wote walikana na Hakimu Kaluyenda aliwataka kuwa na wadhamini
wawili wanaoaminika ambao kila mmoja wao alitakiwa kusaini hati ya
dhamana ya maneno yenye thamani ya Sh1 milioni pamoja na washtakiwa
wenyewe.
Hata hivyo, Hakimu Kaluyenda aliiahirisha kesi hiyo hadi Januari 21, 2015 na kuwaachilia huru washtakiwa watatu.
Mhadhiri CBE kizimbani

Post a Comment