‘Mikikimikiki ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa’

Dar es Salaam. Wanachama 11 wa Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya kujeruhi, kuwatishia na kuwazuia maofisa wa polisi kutekeleza majukumu yao.
Watu hao wanadaiwa kufanya vurugu kwa nyakati tofauti wakati wa uapishwaji wa wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika wilaya ya Kinondoni uolifanyika Januari 6, mwaka huu katika Hoteli ya Landmark iliyopo Ubungo, Dar es Salaam, wakipinga kuwa baadhi ya waliokuwa wakiapishwa hawakustahili.
Hali hiyo ilisababisha polisi kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya.
Akisoma hati ya mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumain Kweka alidai jana kuwa washtakiwa Sunday Urio (20), Kizito Damian (35), Joseph Samky (30), Christant Luhilila (24), Karim Ally (40), Wilfred Ngowi (30) na Kinyaiya Siriri (35) waliwatishia na kuwazuia maofisa wa Polisi kutekeleza majukumu yao.
Kweka alidai, Januari 6, 2015 katika eneo la Ubungo RiverSide, Wilaya ya Kinondoni, washtakiwa hao kwa pamoja waliwatishia na kuwazuia maofisa wa polisi wasitekeleze majukumu yao.
Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka hayo, waliyakana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekwisha kamilika na wakaomba ipangwe tarehe kwa washtakiwa kusomewa maelezo ya awali (PH).
Hakimu Mkazi, Devotha Kisoka aliwaambia washtakiwa hao dhamana ipo wazi na kuwataka kila mshtakiwa kusaini hati ya dhamana ya maneno ya Sh5 milioni pamoja na kuwa na wadhamini wawili.
Katika kesi nyingine, iliyosomwa mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda washtakiwa Abdul Hamis (67), Mwanaharusi Salum (42), Kizito Damian (35), Joseph Samky(30), Sunday Urio (30), Sandro Carlos na Karim Ally wanakabiliwa na shtaka la kumjeruhi Juma Salum na kumsababisha maumivu na majeraha. Wakili Kweka akishirikiana na Wakili wa Serikali, Janeth Kitali walidai kuwa Januari 6, katika Hoteli ya Landmark Wilaya ya Kinondoni walimjeruhi Juma Salum.
Ilidaiwa kuwa siku hiyo ya tukio washtakiwa hao kwa pamoja walimpiga kwa kumrushia mawe na kumsababishia majeraha Salum na kipigo hicho kilisababisha mkono wake wa kushoto kuvunjika.
Baada ya kusomewa shtaka linalowakabili, washtakiwa wote walikana na Hakimu Kaluyenda aliwataka kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao kila mmoja wao alitakiwa kusaini hati ya dhamana ya maneno yenye thamani ya Sh1 milioni pamoja na washtakiwa wenyewe.
Hata hivyo, Hakimu Kaluyenda aliiahirisha kesi hiyo hadi Januari 21, 2015 na kuwaachilia huru washtakiwa watatu.
Mhadhiri CBE kizimbani

Post a Comment

أحدث أقدم