MKE, HAWARA MBARONI WIZI WA GARI

MWANAMKE mmoja mke wa mtu anayejulikana kwa jina la Latifa Ally, hivi karibuni alikamatwa akiwa na hawara yake aitwaye Mose Kessy, wakidaiwa kuiba gari aina ya Toyota Opa lenye namba za usajili T 818 BHG la John Alex, mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro, Risasi Jumamosi lina mkanda mzima.
Alex ambaye ni mume wa Latifa wakiwa na miaka nane katika ndoa yao, ambaye ni mfanyabiashara wa usafirishaji mizigo, anadaiwa kumnunulia gari hilo mkewe kama zawadi.
Inadaiwa kuwa baada ya kupewa gari hilo, Latifa alisubiri kwa muda hadi mumewe aliposafiri kikazi, ndipo alipoondoka na hawara wake huyo, wakitanua sehemu mbalimbali nchini, ikiwemo Dar es Salaam, Morogoro na Tanga.
Akizungumza na mwandishi wetu, Alex alisema alisafiri kikazi kuanzia Desemba 10-12 mwaka jana, lakini aliporudi alikuta mkewe akiwa ameondoka na gari lake pamoja na Mose Kessy.
“Baada ya kurudi safari sikumkuta mke wangu kitu ambacho si kawaida yake, nilianza kufuatilia mawasiliano yake  na kubaini kuwa ana mtu anawasiliana naye kwa Instagram yuko jijini Dar es Salaam na alitambulika kwa jina la Mose Kessy.”
Kufuatia jambo hilo, Alex alifungua malalamiko katika kituo cha Polisi Moshi na Jalada lake lilisomeka; MOS/RB/4669/2014 WIZI WA GARI na kwa kushirikiana na jeshi la polisi, walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
“Tuliwakamata wakiwa kwa mganga wa kienyeji, sikujua lengo lao kuwa hapo ni nini, sheria itachukua mkondo wake,” alisema Alex. Kwa upande wa Latifa alipohojiwa kuhusiana na tukio hilo, alikiri kukamatwa mkoani Tanga akiwa na Mose  na kudai alikuwa na mpango wa kuuza gari hilo kisha akafungue biashara.
“Wazo langu lilikuwa ni kuuza lile gari maana mume wangu alishanipa mpaka na kadi yake, hivyo ninaamini nilikuwa nikiuza mali yangu, yule ni rafiki yangu na sina mpango naye tena,” alisema Latifa.
Akizungumzia suala la kukamatiwa kwa Sangoma,  Latifa alisema aliyeenda ni Mose  ambaye  walikuwa wote na lengo lake  lilikuwa ni masuala yake ya muziki na si vinginevyo maana ni msanii.

Post a Comment

Previous Post Next Post