MPENZI WA MBALI UKISEMA KATULIA, HAKUSALITI, UNAJIPA MOYO TU!


Mchezo wa wapenzi kusalitiana umeshamiri sana kwenye jamii yetu. Ni kitu kinachouma sana lakini cha kushangaza imefika mahali watu wanaona ni cha kawaida kwa kuwa ni vigumu kumzuia mtu asikusaliti akiwa ameamua kufanya hivyo.
Kamchezo haka kapo kwa jinsi zote lakini leo niwazungumzie wasichana ambao baadhi wamezidisha na kuwaogopesha wanaume wengi kujiingiza kwenye mapenzi.
Tabia ya msichana kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja hasa kimjinimjini imekuwa ni kama fasheni. Unaweza kusema wewe uko peke yako kwa huyo uliyenaye lakini kumbe unajidanganya.Hii ni kwa sababu wengi wanasaliti kwa umakini mkubwa bila ya wanaume kushitukia huku tamaa ya fedha na vitu vya thamani vikiwa ndiyo chanzo.
Matokeo yake sasa unakuta binti anakuwa na mwanaume wa kumlipia kodi ya nyumba, wa kumfanyia ‘shopping’ na wa kumlisha.
Wenye tabia hiyo wengi wao ni wale wasichana wazuri ambao wakikatiza mbele za wanaume ni lazima wapate usumbufu wa hapa na pale. Hawa wanapokosa msimamo wa kusema ‘no’ kwa wanaume wanaowatokea, matokeo yake ndiyo hayo ya kuwapanga foleni wanaume.
Kinachoniuma sasa ni kwamba, kuna wanaume ambao wao wanatafuta wanawake wa kuoa na wanapokutana na wasichana hawa, hujikuta wakiwekeza ile mbaya wakidhani wamebahatika kupata wasichana wazuri kumbe wameingia ‘vyoo vya kike’.
Ukitaka kujua ni kwa jinsi gani wanaume wengi tunasalitiwa na wapenzi wetu, msikilize kijana huyu ambaye ni mmoja wa waathirika wa tabia hii ya wasichana kujimilikisha wanaume zaidi ya mmoja.Anasema: “Katika maisha yangu nimekuwa na ndoto za kuwa na mke mzuri, niliamini nikiwa na kazi nzuri na mke mzuri, maisha yangu yatakuwa ya furaha sana.
“Mungu akanijaalia nilipomaliza chuo nikapata kazi na siku moja nikakutana na msichana ambaye hakika alikuwa chaguo la moyo wangu. Umbo lake lilinivutia sana ila hofu yangu ikawa kwenye tabia.
“Sikutaka kumkosa, nikajiaminisha kwamba atakuwa mzuri pia kitabia. Nilipomtokea na kummwagia sera zangu, naye alionesha kunipenda na hapo ndipo tulipoanzisha uhusiano wetu.
“Siku za mwanzo alionesha kunipenda na kuniheshimu sana. Sikuona dalili za kusalitiwa licha ya kwamba alipokuwa mbali na mimi nilihisi mapedeshee wangeweza kuniibia. Uzuri alikuwa akinipa moyo kwamba, amepita kwa wengi lakini kwangu amefika na wala nisifikirie kuna siku atanisaliti.
“Siku moja tukiwa chumbani kwangu, aliumwa ghafla. Hali yake ikawa mbaya, nikawapigia simu ndugu zake na kuamua kumpeleka hospitalini. Kutokana na kuumwa kule, simu yake ilibidi nimshikie.“Mara ikaingia simu kutoka kwa mtu aliyeseviwa kwa jina la Mche Mungu. Sikupokea, ikaita mpaka ikakatika. Baadaye ikaingia sms iliyoandkwa hivi; Vipi baby, mbona hupokei?”
“Ujumbe huo ulinishangaza sana, nikagundua kuna mwanaume mwingine anapendwa. Niliumia sana. Baada ya mchumba wangu kupata nafuu na kumkabidhi simu yake, alionekana kukosa amani zaidi hasa baada ya kugundua kuwa niliona sms aliyotumiwa.”
Ushuhuda wa kaka huyu unatupa fundisho kubwa sana. Wasichana wengi wa mjini ni wazuri na wanayajua mapenzi kweli lakini wengi wao wametawaliwa na utapeli tena wa kisiri sana.
Unaweza kutokea kumpenda sana lakini kumbe yeye ana lake jambo, anakuchukulia kama wa kukuchuna tu na nyuma yako unachagia penzi na wenzako kibao.Kikubwa ni kwamba, unapoingia kwenye uhusiano na msichana yeyote na ukaona anafaa kuwa mkeo hata kama utabaini kuwa ni mapepe, fanya haraka umuoe.
Ukishamuoa angalau unaweza kuwa na imani kwamba hawezi kutoa ‘sukari’ yako kwa mtu mwingine licha ya kwamba, hata ukimuoa akiamua kukusaliti anaweza.Kinachosaidia ukishamuoa ni kwamba, atatakiwa kufanya kazi ya ziada sana kukusaliti bila ya wewe kujua na hata akikusaliti haitakuwa kwa kiwango kikubwa.
Wapo ambao wanaishi mbali na wapenzi wao, ikifika saa tatu usiku anamuaga mpenzi wake tena kwa maneno matamu kisha anasema anazima simu. Akishazima simu anakwenda kwenye mishemishe zake. Wewe uko mbali na unajua mwenzako kalala, kumbe yawezekana kaenda kwa mwanaume mwingine.
Mimi nadhani ni suala la kuaminiana tu lakini kiukweli kabisa mke au mume ni rahisi sana kumkontroo lakini mpenzi tena ambaye mnaishi mbalimbali, ukijiaminisha kwamba hakusaliti, unajipa moyo tu.

Post a Comment

Previous Post Next Post