Unahitaji kutanguliza maombi na dua kujihakikishia usalama
unaposafiri kwa njia ya Reli ya Kati. Usafiri huo unadaiwa kuwa ni ‘nusu
ya kifo’ kwa watumiaji wake.
Katika harakati za kudhibiti hali mbaya katika
Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), hivi karibuni, Waziri wa Uchukuzi, Dk
Harrison Mwakyembe aliwatimua kazi watumishi sita kutokana na kitendo
cha kuihujumu kampuni hiyo.
Alichukua uamuzi huo kwa lengo la kuimarisha upya
TRL katika utoaji wa huduma zake kupitia maboresho yanayoendelea ikiwamo
vifaa na mabehewa mapya.
Pamoja na hatua hiyo, wachambuzi wa masuala ya
kiuchumi wanasema endapo usafiri wa njia ya reli utawekezwa ipasavyo,
utakuwa nyenzo pekee inayorahisisha kasi ya ukuaji wa uchumi na
maendeleo ya wananchi.
Akizungumzia umuhimu wa sekta hiyo, Profesa
Hamphrey Moshi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, anataja mambo kadhaa muhimu ya
kuimarishwa katika sekta hiyo ya reli kwa manufaa ya nchi.
Anafafanua kuwa reli ya kati itakapoboreshwa
itasaidia kupunguza msongamano wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam
ambayo inatumika kupitishia mizigo inayokwenda nchi jirani na mikoani.
“Wafanyabiashara wamekuwa wakilalamikia msongamano
wa mizigo kwa sababu maroli hayana kasi ya kusafirisha mizigo hiyo,
wanahamia katika bandari nyingine, lakini njia hiyo ya reli ingekuwa
imara tungeongeza mapato ya bandari na kulinda wateja,” anasema.
Kwa mujibu wa TRL, kupitia mpango wake mpya wa
biashara unaoonyesha licha ya vikwazo vilivyopo, abiria wake
wameongezeka hadi kufikia milioni moja na zaidi mwaka uliopita.
Kutokana na hatua hiyo, Profesa Moshi anasema
kuimarika kwa njia ya reli kutasaidia kupunguza mfumuko wa bei. Anasema
mfumuko huo unaathiri maisha na uchumi wa Watanzania kutokana na ukosefu
wa mahitaji ya kutosha kwa mikoani.
Anasema kila wakati Serikali inatumia gharama
kubwa kujenga miundombinu ya barabara, lakini usafiri wa malori umekuwa
ukiiharibu hatua inayoathiri mgawanyo wa bajeti.
“Uzoefu unaonyesha malori yanachangia ongezeko la
ajali za barabani. Treni moja ni sawa na malori 75, ambayo yanaharibu
mazingira ya hali ya hewa,” anasema na kuongeza:
“Lakini tukiimarisha njia ya reli, Serikali
itaokoa fedha za matengenezo ya dharura kwa barabara, ajali zitapungua,
makali ya maisha pia yatapungua.”
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment