MREMBO
mmoja aliyefahamika kwa jina la Regina Thobias (29) amenaswa akitapeli
watu kwa kuwachangisha fedha akidai kuuguliwa na mgonjwa katika
Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa, kitu ambacho siyo kweli.
Tukio hilo lilitokea Ijumaa baada ya mrembo huyo anayeishi eneo la
Frelimo mjini hapa, kutaka kumtapeli dereva wa halmashauri ya mji,
akiomba asaidiwe fedha ili akalipie hela za matibabu kwa shangazi yake
aliye hoi hospitalini hapo.
Hata hivyo dereva huyo hakuweza kutoa fedha hizo baada ya
kumshuku kuwa tapeli, lakini wakati akitafakari, ghafla binti huyo
aliondoka na kwenda kupanga foleni kama mtu anayetaka kuchukua fedha
katika mashine za ATM ya benki moja iliyopo eneo hilo.
Lakini kama ilivyo kawaida za mwizi ni 40, baadhi ya watu
waliopata kutapeliwa na mrembo huyo walianza kumhoji kwa kitendo chake
cha kupanga foleni katika ATM kwani kwa wanavyomjua, asingeweza kuwa
na akaunti. Hata walipomtaka kuonyesha kadi yake alishindwa.
Wakizungumza eneo la tukio, baadhi ya waliopata kutapeliwa naye
walisema mrembo huyo amekuwa na tabia ya kutapeli watu mbalimbali kwa
kuwadanganya kuwa ana mgonjwa Hospitalini na yeye anaishi Ilula,
kwamba ameporwa pesa zake na vibaka.
Akijitetea, binti huyo alikiri kufanya vitendo hivyo kutokana na hali
ngumu ya maisha. Akaomba kusamehewa, wakamwachia kwa sharti kuwa
asirudie tena tabia hiyo
إرسال تعليق