Mrithi wa Werema: Ofisi ya AG ina changamoto kubwa

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, amesema anaingia katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, kukiwa na changamoto kubwa ya wananchi kutoielewa serikali yao.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuapishwa Ikulu jijini Dar es Salaam, alisema serikali ina nia njema kwa wananchi wake hivyo ni vyema kiongozi anapoeleza jambo aaminiwe.

“Kama Taifa tunahitaji kuwa wamoja ili amani na mshikamano viendelee kuwapo nchini ambavyo ni muhimu sana kwa maendeleo endelevu,” alisema.

Masaju ambaye amesema anataka kutambulika kama Mtumishi badala ya mheshimiwa, alisema amekuwa mzoefu katika kuishauri serikali na Mahakama na kwamba kwa sasa ameongezewa wajibu wa kulishauri Bunge katika masuala ya kisheria.

Hata hivyo, alishindwa kukidhi kiu ya waandishi wa habari waliotaka kujua suala la uwazi katika mikataba ya madini na gesi na kusema kuwa bado ni mgeni na hajafika ofisini na kuwataka waandishi kwenda ofisini kwake kwa ufafanuzi zaidi.

Alisema ipo mikataba inastahili kuwa wazi na mingine haistahili, na kwamba atakapoanza kazi atazungumza na waandishi wa habari juu ya suala hilo na mengine.

Mwansheria huyo aliteuliwa baada ya aliyekuwa Mwansheria Mkuu wa Serikali, Fredirick Werema, kujiuzulu Desemba 16, 2014 kutokana na ushauri alioutoa katika fedha za akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
 

Post a Comment

أحدث أقدم