Msajili amwamuru Mrema kuitisha uchaguzi wa TLP

Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema.
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, imekiandikia barua chama cha Tanzania Labour (TLP), kukitaka kifanye uchaguzi  wa viongozi  na kwamba endapo  hakitafanya hivyo baada ya Aprili, mwaka huu kitafutiwa usajili.
Akizungumza na Waandishi wa habari jana, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, alisema sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 kifungu cha 9 inavitaka vyama hivyo kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano, lakini chama hicho kimepitisha muda bila kufanya uchaguzi.

Alisema ofisi ya Msajili ilipokea maombi kwa chama hicho mara tatu kikiomba kusogezewa mbele  muda wa kufanya uchaguzi huo kutokana na sababu mbalimbali.

Sababu ya kwanza ilikuwa ya Mwenyekiti wake, Augustine Mrema, kuwa nje ya nchi kwa matibabu, sababu ya pili ilikuwa kupisha Bunge Maalum la Katiba na nyingine ilikuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Nyahoza alisema sababu zote hizo zilipimwa na kuonekana za msingi ambazo zilikuwa mwaka jana, lakini hivi sasa hawana sababu nyingine ya kuwazuia kutofanya uchaguzi huo.

“Kama sheria ya vyama  vya siasa  inavyosema, kufanya uchaguzi kwa vyama  ni lazima kila baada ya miaka mitano, TLP ilitakiwa iwe imefanya hivyo mwaka jana, lakini kutokana na sababu  za msingi tuliwavumilia, mwaka huu  hawana sababu nyingine ya kujitetea, na tumeamua kuwaandikia barua kuwataka wafanye uchaguzi huo ifikapo  Aprili mwaka huu, kinyume cha hapo chama kitafutwa,” alisema.

Aidha,  Msajili amemwandikia barua Mrema kumtaka awasilishe maelezo kwa ofisi hiyo juu ya tuhuma zinazomkabili za kuendesha chama kinyume cha Katiba ya chama.

Uamuzi wa kumtaka Mrema kuwasilisha maelezo hayo umefuatia malalamiko  ya  baadhi ya wanachama kumshutumu kuendesha chama kinyume cha kanuni na taratibu za chama.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post