MTOTO WA HOUSEGIRL

Leo ni kumbukumbu ya aliyekuwa Rais wa Cuba kwa takriban miongo minne, Fidel Alejandro Castro Ruz maarufu kama Fidel Castro. Ni Rais anayependwa zaidi na wanaharakati za kimapinduzi.
Moja ya vitu vinavyompa sifa katika ulimwengu huu ni ujasiri wake wa kutoafikiana na Taifa kubwa duniani, Marekani kiasi cha kuandamwa na kutengenezewa mitego au majaribio mbalimbali ya kumwangamiza pasipo mafanikio.
Miongoni mwa vitu vingi ambavyo havijulikani miongoni mwa wengi ni historia yake. Huyu jamaa alizaliwa nje ya ndoa. Ni ‘mwanaharamu’ halisi, kama unaweza kumuita hivyo kwa lugha sanifu ya Kiswahili.
Baba yake Castro aliyejulikana kama Angel Castro Argíz alikuwa ni Mhispania aliyehamia Cuba wakati wa harakati za uhuru wa nchi hiyo katika kipindi kati ya mwaka 1895 na 1898. Mkewe ni Maria Luisa Argota.
Angel alikuwa ni mkulima wa miwa wa kipato cha kati aliyeishi katika Kitongoji cha Biran, mashariki mwa nchi hiyo pamoja na familia yake iliyokuwa na kijakazi aliyeitwa Lina Ruz Gonzalez.
Kijakazi huyo alikuja kughilibiwa na Angel kuwa na uhusiano wa kimapenzi na ndiyo uliyosababisha kuzaliwa kwa Castro.
Katika muda wote wa ndoa ya Angel na Maria hawakufanikiwa kupata mtoto mpaka Agosti 13, 1926 baba huyo alipompa ujauzito binti huyo wa kazi za ndani (housegirl).
Baada ya kuzaliwa kwa Castro, Angel alilazimika kuivunja ndoa yake na Maria na kuamua kuishi na Lina ambaye alizaa nae watoto watano.
Castro alionekana kuwa na akili nyingi huku akiwika katika michezo hasa ule wa magongo. Kutokana na uelewa wa haraka aliokuwa nao tangu akiwa shule ya msingi, alisomea sheria katika Chuo Kikuu cha Havana.
Akiwa hapo alivutiwa na siasa hivyo kujiunga na chama cha Orthodox, kilichokuwa kinapinga masuala ya ufisadi serikalini.
Mara tu alipohitimu, mwaka 1950 alifanyakazi ya uwakili akivutiwa zaidi za kesi za kisiasa.
Kutokana na mapenzi yake katika siasa, alikuwa ni mgombea wa ubunge katika Uchaguzi Mkuu uliotarajiwa kufanyika Juni, 1952.
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم