Tanga. Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban Bin Simba
amewataka Watanzania kutoichezea amani iliyopo na kusema wengi hawaioni
thamani yake kwa kuwa wamezaliwa na kuikuta.
Aidha, amewataka wasikubali kufarakana kama baadhi
ya mataifa ya Magharibi yanavyotaka kwa kubuni mbinu za kuwagombanisha
ili yafanye biashara ya silaha.
Akihutubia kwenye mkesha wa Maulid ya kuadhimisha
kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Shule
ya Msingi Mazoezi, Korogwe, Mufti aliwaasa Waislamu kumuenzi kiongozi
huyo kwa kuimarisha mshikamano na amani.
Alisema Mtume Mohammad (S.A.W) alipozaliwa alikuta
dunia ikiwa imevurugika kwa kukosa amani na hakukuwa na utaratibu
maalumu, lakini alitumia juhudi kubwa kuleta amani kwa kujenga ustaarabu
kwa kuyakutanisha makundi yaliyokuwa yakigombana na kuyasuluhisha.
“Mtume Mohammad (S.A.W) alisawazisha sera za watu
ambao kazi yao kubwa ilikuwa kuwagombanisha wanadamu, pia aliwakutanisha
mahasimu ndipo amani ikapatikana,” alisema Mufti Simba.
Alisema njia pekee ya kudumisha siku ya kuzaliwa
kwa Mtume Mohammad (S.A.W) ni kwa Waislamu kuepuka mbinu chafu za
kufarakanishwa ili waonekane wavurugaji wa amani wakati ukweli ni
kinyume chake.
Mufti Simba aliwataka waumini hao kujenga moyo wa
kujitolea kifedha kwa ajili ya kueneza dini yao pia aliwataka kuchangia
elimu akisema hakuna ya bure kuanzia ile ya dunia hadi ya dini.
Makamba
Akihutubia katika Maulid hayo, Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba aliwataka Watanzania
wasifanye majaribio kwa kumchagua rais anayetoa fedha kusaka wadhifa
huo.
“Kiongozi wa namna hiyo, hataongoza kwa haki, watu
wanaotoa fedha nyingi kusaka uongozi na wanaotumia makundi kamwe
hawataongoza kwa haki. Tuwakatae viongozi wa namna hii,” alisema Makamba
ambaye tayari ametangaza nia ya kuwania urais, huku akisisitiza kuwa
Watanzania watafanya kosa la mwaka kumchagua rais ambaye atakuwa amepita
kwa kutoa fedha nyingi katika kusaka wadhifa huo.
Akihutubia umati mkubwa wa waumini wa Kiislamu
Makamba alisema: “Msikubali kuwachagua hawa wanaotumia fedha na mbinu
nyingine za kuwagawa kwa makundi, kwani hao si viongozi wanaohitajika
kuliongoza Taifa la Tanzania,” aliongeza: “Tanzania inahitaji kiongozi
atakayewaunganisha wananchi wote kuwa kitu kimoja, mwenye busara na
subira lakini si anayeutaka uongozi kwa njia yoyote hata kama ni
kuwagawa kwa makundi au kutumia fedha ili mradi aweze kuchaguliwa.
إرسال تعليق