Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG), George Masaju amesema ataanza kuipitia mikataba yote inayodaiwa
kuwa na utata ili aweze kutoa ufafanuzi wa kina lakini akawataka
Watanzania wampe muda.
Hata hivyo, alisema hadhani kama watu wanaosema
kuwa baadhi ya mikataba iliyoingiwa na Serikali ina utata wako sahihi na
kuwataka Watanzania kuwa na imani na Serikali iliyopo madarakani.
“Watu wanasema hivyo ila kuna jambo moja ambalo wanatakiwa kujua kuwa kuna baadhi ya mikataba ambayo ni siri,” alisema.
Masaju aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete mwishoni
mwa wiki kuchukua nafasi ya Jaji Frederick Werema ambaye alijiuzulu
kutokana na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Jaji Werema aliomba kujiuzulu kwa sababu ushauri wake kuhusu suala hilo haukueleweka na badala yake kuchafua hali ya hewa.
Kabla ya uteuzi huo, Masaju alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kuhusu uteuzi wake, alisema; “Nina furaha kwa
sababu ninalitumikia Taifa na kuteuliwa kwangu kunaonyesha kuwa Serikali
ina imani na mimi.”
Licha ya kubanwa na wanahabari kuwa kwa nafasi
aliyokuwa nayo awali anafahamu maeneo yenye matatizo, ikiwamo na
mikataba yenye utata, alisisitiza kuwa apewe muda zaidi.
Katika mkutano wa 16 na 17 wa Bunge uliohitimishwa
Novemba 28 mwaka jana, Bunge lilitoa maazimio manane, likiwamo la Jaji
Werema kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria kutokana na kuipotosha Serikali
kuhusu mabilioni ya fedha kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.
Maazimio mengine yalikuwa ni kuwajibisha baadhi ya mawaziri na bodi ya wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Kutokana na maazimio hayo, Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi amesimamishwa kazi, aliyekuwa Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka
amefukuzwa kazi na kuteuliwa kwa bodi mpya ya Tanesco
إرسال تعليق