Iringa. Wengi huisikia dhahabu, sifa zake na thamani yake. wenye
fedha zao hununua vidani vya madini hayo adimu ulimwenguni na
kujirembesha, lakini wale maskini kujikuta wakivaa vidani yaliyotiwa tu
nakshi ya madini hayo, huku asilimia kubwa vikiwa vimetengenzwa kwa
bati.
Mbali ya wenye fedha kidogo, wapo baadhi ambao
maisha yao yote hutegemea ‘kupiga roba’ watu waliovaa vidani hivyo ili
kujinakshi wao pia, lakini wengi hufanya uhalifu huu kwa lengo la
kuviuza na kujipatia fedha kwa njia hii isiyo halali.
Mlolongo wa matukio yote hayo unatokana na kasi
ya ongezeko la thamani ya dhahabu nchini na ulimwenguni kwa ujumla
katika miaka karibuni. Mahitaji makubwa ya madini ya dhahabu yameongeza
msukumo katika uzalishaji wa dhahabu kwa ujumla wake.
Uzalishaji wa dhahabu hufanywa katika migodi
mikubwa inayomilikiwa na kampuni kubwa za kimataifa, pia migodi
midogomidogo inayoendeshwa na wachimbaji wadogo pia hutoa mchango mkubwa
na madini wanayoyachimba ndiyo ambayo hutumiwa sana na masonara wa
ndani kuzalishia vidani kama pete, hereni, bangili na vinginevyo.
Kinachotafutwa katika machimbo madogo huwa na
thamani kubwa ya kifedha na wapo waliotajirika na kubadilika kimaisha
kutokana na mafanikio walioyapata katika uchimbaji wao. Hata hivyo,
maisha katika migodi mingi ya wachimbaji wadogo siyo ya kawaida.
Hali ya maisha katika maeneo haya siyo kama
inavyofikiriwa kwani haiakisi uhalisia wa thamani ya madini. Mgodi wa
machimbo ya dhahabu wa Ihanzutwa ni mfano halisi wa aina ya maisha
waishiyo wachimbaji wadogo katika maeneo mengine nchini.
Kama yalivyo machimbo mengine ya dhahabu hapa
nchini ni dhahiri kwamba Ihanzutwa nayo inachangia uchumi wa nchi,
upatikanaji wa ajira na biashara ya dhahabu. Hata hivyo, matukio ya
uhalifu katika eneo la mgodi huu yanatishia maisha ya watu na mali zao.
Kwa ujumla mazingira siyo salama.
Mgodi huu uliopo kilometa zipatazo 65 kutoka Mji
wa Mafinga katika wilaya ya Mufindi mkoani Iringa umegubikwa na matukio
ya wizi, ngono zembe, biashara ya bangi na dawa za kulevya aina ya
heroine na cocain. Biashara ya dawa za kulevya inafanywa wazi wazi
pasina kificho na wahusika hawaogopi kwani hakuna usimamizi wa sheria.
Ngono yaitwa ‘show time’
Wachimbaji wengi hutumia fedha zao katika kununua
ngono kutoka kwa wanawake waliojaa katika machimbo hayo. Wanawake wengi,
wakiwamo mabinti wadogo wenye wastani wa umri wa miaka 17 na 18
wamejazana eneo hilo kutafuta soko la wachimbaji hao ambao kiasi kidogo
cha malipo kwa huduma ni Sh10,000.
Asilimia kubwa ya wanawake hao wanafanya kazi
katika vilabu vya pombe na kuendesha biashara ya ngono kwa saa maarufu
kama ‘show time’ na kurudi kuendelea kuuza pombe. Wapo pia baadhi
wanaojitegemea bila ya kufanya kazi katika kilabu chochote cha pombe
- Mwananchi

Post a Comment