Dar es Salaam. Kamati za Kudumu za Bunge
zinatarajiwa kuanza kukutana na kutekeleza majukumu ya kibunge jijini
Dar es Salaam kuanzia Jumanne ijayo, huku ratiba zake zikionyesha kuwa
mambo yenye mvutano mkali kwa sasa yatajadiliwa.
Pia, kabla ya kuanza kwa vikao hivyo unatarajiwa
kufanyika uchaguzi wa wenyeviti wapya wa Kamati za Bajeti, Katiba,
Sheria na Utawala na Nishati na Madini baada ya waliokuwepo kutajwa
kuhusika katika sakata la ufisadi katika Akaunti ya Tegeta Escrow na
Bunge kuazimia waondolewe katika nafasi zao.
Waliotajwa katika maazimio ya Bunge, kutakiwa
kuachia nafasi zao za uwenyekiti ni Andrew Chenge (Bajeti), William
Ngeleja (Katiba) na Victor Mwabalaswa (Nishati na Madini).
Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Januari 14
itajadili hesabu za kampuni ya magazeti ya serikali, Shirika la
Utangazaji (TBC) na Januari 15 itajadili hesabu za taarifa ya Ukaguzi
Maalumu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ambayo inalalamikiwa kwa
muda mrefu.
Januari 15 kamati hiyo itajadili hesabu za Bodi ya
Sukari nchini, Bodi ya Korosho Tanzania na Mamlaka ya Uendelezaji wa
Bonde la Mto Rujifi (Rubada).
Pia Januari 19, itajadili hesabu za Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) ambayo watumishi wake saba walisimamishwa kazi
kutokana na sakata la escrow na Januari 20 itajadili taarifa ya Kamati
ndogo ya Hesabu za Serikali kuhusiana na ukusanyaji mdogo wa kodi za
ardhi unaoikabili Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Pia, itajadili hesabu za Wizara ya Kilimo, Chakula
na Ushirika na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ambalo
hivi karibuni liliingia katika mgogoro mkali na kamati hiyo na
kusababisha watendaji wake kukamatwa na polisi kutokana na kuinyima
kamati hiyo mikataba 26 ya gesi. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
za Mitaa (LAAC), Januari 13 itafanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo
katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Ukaguzi huo unafanyika
wakati tayari kamati hiyo ikiwa imefanya ziara katika Manispaa za jiji
hilo na kubaini ufisadi mkubwa. Ilala na Kinondoni zimetajwa kwenye
ufisadi huo.
Baada ya ziara hiyo, Januari 14, LAAC itakutana na
kujadiliana na mameya wa manispaa tatu za jiji hilo kuhusu hali halisi
ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali na nidhamu ya matumizi ya fedha za
umma katika maeneo yao.
Pia, itajadili taarifa ya hesabu zilizokaguliwa za Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na Karatu, Geita na Rorya
Kuanzia Januari 19 hadi 21, kamati hiyo itajadili taarifa ya hesabu za manispaa za Bukoba, Kasulu na Kwimba.
Kamati ya Bajeti itajadili taarifa za ugawaji wa
fedha na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo ya maji,
barabara, uchukuzi na Tamisemi. Kamati hiyo pia itakutana na washirika
wa maendeleo wa Mfuko Mkuu wa Bajeti (GBS).
Kamati na Nishati na Madini yenyewe itajadili hali
ya migodi ya urani iliyopo Namtumbo na Makaa ya Mawe Mchuchuma, Liganga
na Ngaka, kujadili uzalishaji na upatikanaji wa umeme nchini na hali ya
kifedha ya Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco).

Post a Comment