Dar es Salaam. Wakati joto la kisiasa
likiendelea kupanda kila siku, makundi mbalimbali ya wanawake
yanaendesha kampeni za chinichini nchi nzima kuhakikisha kuwa
anapatikana rais mwanamke katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba
mwaka huu.
Makundi hayo yanayoongozwa na wanawake wasomi na
wanasiasa yamo katika kinyang’anyiro hicho ambacho hatima yake ni Oktoba
mwaka huu.
Kampeni zinazofanyika sasa, ni kuhakikisha jina la mwanamke linapitishwa na wanawake wote bila kujali itikadi, kumpigia kura.
Umoja wa Wanawake Wanasiasa nchini (Ulingo),
Mtandao wa Wanawake na Katiba, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC) na wadau wengine ndiyo walio mstari wa mbele kuhakikisha kuwa
azma hiyo inafikiwa.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema kuwa walikwisha kuanza kampeni
hizo tangu Septemba 2014 kupitia mradi wa ‘Wanawake na Uchaguzi’ huku
wakiwa tayari wamefika kwenye mikoa 15.
“Uzoefu wetu unaonyesha kuwa mwaka huu wa uchaguzi una nafasi kubwa kwa mwanamke ikilinganishwa na 2005/10,” alisema Bisimba.
Dk Bisimba alitaja mikoa waliyofanikiwa kuendesha
mradi huo kuwa ni Mtwara, Mwanza, Dar es Salaam, Mara na Ruvuma.
Aliongeza kuwa mwaka 2000, CCM iliwakatisha tamaa wanawake walioonyesha
nia ya kuwania urais.
“Mwaka huu ngoja tuangalie, maana kuna wanawake
wengi wenye uwezo kama tulivyoshuhudia kwenye utendaji wao, uadilifu,
uzoefu na busara za kuongoza hata taifa hili,” alisema Dk Bisimba na
kuongeza:
“Kwa hivyo tunaratajia kuona vyama vikubwa vikitoa nafasi sawa kwa wanawake bila upendeleo au kuendekeza rushwa.”
Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia
Tanzania (TGNP), Usu Mallya alisema atakuwa tayari kuendesha kampeni
hizo kwa mwanamke yeyote atakayejitokeza bila kujali itikadi za chama
anachotokea.
Naye Mwenyekiti wa Ulingo, Anna Abdallah
alimwambia mwandishi wa gazeti hili kuwa, umoja huo umeshajiandaa
kuendesha kampeni ya pamoja na kwamba unasubiri kupulizwa rasmi kwa
kipenga cha kampeni.
Mama Anna alisema katika uchaguzi huo, wanawake
hawatakuwa tayari kuendelea kubakia kwenye majukwaa kuwapigia kampeni
wanasiasa wanaume peke yao, badala yake wameamua kuchukua hatua hiyo
kutokana na uwezo na utashi wa wanawake uliopo hivi sasa.

Post a Comment