Mbinga. Ofisa habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa,
Humphrey Kisika (32) ametangaza nia ya kuwania ubunge wa Jimbo la Mbinga
Mashariki mkoani Ruvuma katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari kijijini kwake
Ukata wilayani Mbinga juzi, Kisika alisema anataka kupokea kijiti kutoka
kwa mbunge wa sasa, Gaudance Kayombo.
Alisema anautambua na kuuthamini mchango alioutoa
mbunge huyo, lakini umefika muda wa yeye kupumzika na kuwaachia wengine
nao wawatumikie wakazi wa jimbo hilo.
Alisema amebaini bado kuna pengo linalodumaza
maendeleo kati ya wataalamu ambao ni watendaji wa shughuli mbalimbali za
Serikali na wananchi ambao ni wapigakura.
“Kuna manung’uniko mengi kutoka kwa wananchi
yanayochangiwa na baadhi ya watendaji ambao kwa masilahi yao binafsi au
kwa sababu ya kufanya kazi kwa mazoea, wanashindwa kuutumikia vyema umma
wa Watanzania,” alisema.
Kisiki, ambaye anataka kujaribu bahati yake kwa
kupitia CCM, alisema chama hicho kina sera nzuri zinazoshindwa kufanya
kazi kutokana na uzembe wa baadhi ya watendaji.
Akizungumzia mwonekano wa kundi kubwa la vijana
kushabikia zaidi vyama vya upinzani, alisema katika mazingira ambayo
nchi inaendeshwa kwa misingi ya demokrasia kama Tanzania, hali hiyo
lazima itajitokeza.
Hata hivyo, alisema hiyo haimaanishi kuwa vijana wote ni wafuasi wa vyama vya upinzani.
“Ombi langu kwa vijana wenzangu, ni muhimu katika
kipindi hiki cha ushindani mkubwa wa kisiasa tukafanya siasa kwa misingi
ya upendo na amani, tusikubali kutumiwa kwenye harakati za siasa chafu
zitakazohatarisha amani ya nchi hii, tunataka iendelee kuwa kisiwa cha
amani,” alisema.
إرسال تعليق