Okwi atua Dar, aifuata Simba Zenji

Kiungo mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi.

KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, jana alitarajiwa kutua nchini akitokea nyumbani kwao alipokwenda kwenye mapumziko ya wiki mbili.Okwi, raia wa Uganda, alirejea nyumbani kwao mara baada ya mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar iliyomalizika kwa timu hiyo kufungwa bao 1-0, kwa ajili ya fungate.

Awali, kulikuwepo na tetesi za kiungo huyo kuwepo Dar es Salaam akifanya mambo yake huku kukiwepo na taarifa za kwenda kwao katika mapumziko mafupi.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Katibu Mkuu wa Simba, Stephene Ally, alisema Okwi anatarajiwa kutua Dar saa 11:00 jioni na ndege aina ya Rwanda Airways inayopitia Uwanja wa Entebbe, Uganda.
Stephene alisema, kiungo huyo mara baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, ataunganisha kwa kupanda ndege nyingine kwenda kujiunga na wenzake Zanzibar.
“Okwi tayari tumemtumia tiketi na leo (jana) saa 11:00 jioni anatarajiwa kutua Dar akitokea kwao Uganda, atatua nchini kwa ndege ya Rwanda Airways (Rwandair) na moja kwa moja ataelekea Zanzibar.
“Ataelekea huko tayari kwa ajili ya kambi ya pamoja ya kujiandaa na Ligi Kuu Bara na nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi tutakayoicheza kesho (leo) huko Zanzibar,” alisema Stephene.

Post a Comment

Previous Post Next Post