Ruvuma nayo kuunganishwa kwa reli ya Mtwara Corridor

Songea. Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesema kuwa Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa itakayonufaika na mradi wa ujenzi wa reli ya Mtwara Corridor utakaoanza mwakani na utakamilika mwaka 2018.
Dk Mwakyembe aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na wadau mbalimbali wa usafirishaji katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwenye ukumbi wa mikutano wa Ikulu ndogo mara baada ya kufanya ziara ya siku moja kutembelea Uwanja wa Ndege wa Songea mkoani Ruvuma na kukagua miundombinu katika uwanja huo.
Alisema kuwa lengo kubwa la ujenzi wa mradi huo ambao utaanza kujengwa katika Mkoa wa Mtwara kupitia Ruvuma hadi Njombe utagharimu kiasi cha Dola 3.5 bilioni ikiwa ni mkopo kutoka Benki ya Dunia na kujengwa na kampuni ya kichina lengo likiwa kusaidia kusafirisha mizigo mikubwa ikiwamo chuma na makaa ya mawe kwa njia ya reli.
Dk Mwakyembe alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuepusha uharibifu mkubwa wa barabara kutokana na kupitisha mizigo mikubwa na mizito na kuisababishia Serikali kuingia gharama kubwa ya kuzifanyia matengenezo jambo ambalo alidai kuwa linarudisha nyuma uchumi wa Taifa.
Katika hatua nyingine, Dk Mwakyembe alisema kuwa katika mwaka wa fedha wa Julai 2015, Serikali ina mpango wa kuboresha viwanja vya ndege 11 vya mikoa kikiwamo cha Songea mkoani Ruvuma ambacho kinatakiwa kupanuliwa ukubwa wa mita 100, kufunga taa ili kiweze kufanya kazi saa 24 pamoja na kuboresha miundombinu mingine ikwemo njia za kurukia ndege.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post