Songea. Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe amesema kuwa Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa
itakayonufaika na mradi wa ujenzi wa reli ya Mtwara Corridor utakaoanza
mwakani na utakamilika mwaka 2018.
Dk Mwakyembe aliyasema hayo jana wakati alipokuwa
akizungumza na wadau mbalimbali wa usafirishaji katika Halmashauri ya
Manispaa ya Songea kwenye ukumbi wa mikutano wa Ikulu ndogo mara baada
ya kufanya ziara ya siku moja kutembelea Uwanja wa Ndege wa Songea
mkoani Ruvuma na kukagua miundombinu katika uwanja huo.
Alisema kuwa lengo kubwa la ujenzi wa mradi huo
ambao utaanza kujengwa katika Mkoa wa Mtwara kupitia Ruvuma hadi Njombe
utagharimu kiasi cha Dola 3.5 bilioni ikiwa ni mkopo kutoka Benki ya
Dunia na kujengwa na kampuni ya kichina lengo likiwa kusaidia
kusafirisha mizigo mikubwa ikiwamo chuma na makaa ya mawe kwa njia ya
reli.
Dk Mwakyembe alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo
kutasaidia kuepusha uharibifu mkubwa wa barabara kutokana na kupitisha
mizigo mikubwa na mizito na kuisababishia Serikali kuingia gharama kubwa
ya kuzifanyia matengenezo jambo ambalo alidai kuwa linarudisha nyuma
uchumi wa Taifa.
Katika hatua nyingine, Dk Mwakyembe alisema kuwa
katika mwaka wa fedha wa Julai 2015, Serikali ina mpango wa kuboresha
viwanja vya ndege 11 vya mikoa kikiwamo cha Songea mkoani Ruvuma ambacho
kinatakiwa kupanuliwa ukubwa wa mita 100, kufunga taa ili kiweze
kufanya kazi saa 24 pamoja na kuboresha miundombinu mingine ikwemo njia
za kurukia ndege.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق