Onyo wanaosajili shule za umma kwa fedha

Rais Jakaya Kikwete.
Serikali imezionya shule za msingi za umma zinazosajili watoto kwa fedha, kuwatoza pesa za uji na kuwalazimisha wazazi kununua  sare zinazoshonwa shuleni kukoma mara moja.
Kadhalika imezitaka halmashauri kuwachukulia hatua walimu wakuu wanaotoza wanafunzi wa darasa la kwanza fedha hizo kabla ya kuwasajili na kuhimiza wazazi kutoa taarifa.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), anayeshughulikia elimu , Kassim Majaliwa, alisema hayo kufuatia malalamiko ya baadhi ya wazazi kuwa wanalazimishwa kuchangia michango lukiki inayokaribia Sh 100,000.

Wakati wazazi wakilalamikia michango hiyo, wiki iliyopita Rais Jakaya Kikwete, alitangaza kuwa elimu ya msingi na sekondari itatolewa bure kuanzia mwaka ujaoambapo Jumatatu wiki hii, Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, amesema SMZ itatoa elimu hizo bure .

Majaliwa alieleza kuwa kutokana na malalamiko hayo ya wazazi, serikali inasisitiza zaidi kuwa usajili wa watoto ni bure na kinachotakiwa ni kutimiza umri wa kuanza masomo.

 “Hakuna gharama ya usajili, tumewahi kupokea malalamiko wilaya ya Temeke, kwenye shule za Mbagala wazazi wenye watoto waliopo madarasani walikubaliana na kamati za shule wapeleke fedha kiasi lakini jambo hili halipo katika sera ya wala waraka wa serikali wa elimu,” aliongeza:

Pia alisema kumlazimisha mtoto kila siku kubeba Sh. 200 au zaidi za uji, ni kosa kwa sababu shule ambazo zimekubaliana na wazazi kupitia kamati zake, wazazi na walezi ndiyo wanaowasilisha  michango.

 “Kama zipo baadhi ya shule kupitia kamati zao, zimekubaliana wanafunzi wawe wanakunywa uji shuleni, tunachotaka  waamue  kiwango ambacho hakitamuumiza mzazi na fedha zipelekwe kwa wiki au mwezi na walezi au wazazi,” alisema na kuongeza:

“Jukumu la mtoto ni kusoma sio kubeba michango ya shule, tukiruhusu hili iko siku mtoto akipoteza hela inamaanisha shule itamwajibisha ,” alihoji?

Kuhusu baadhi ya shule hizo kuwalazimisha wazazi kununua sare za watoto wao mashuleni, Majaliwa alisema hilo ni kosa kwa sababu shule inatakiwa kutoa maelekezo ya rangi na mshono wa nguo si zaidi ya hapo .

“Hata kama yapo makubaliano kati ya mzazi na kamati ya shule hatuwezi kuingilia lakini kama mkuu wa shule anamlazimisha mzazi kufanya hivyo, watuletee taarifa hatua zichukuliwe,” alisisitiza.

Maelezo ya Waziri yanakuja wakati baadhi ya wazazi na walezi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Kibamba  jijini  Dar es Salaam, wanalazimika kuchangia Sh. 40,000 kusajili watoto wao kwa darasa la kwanza.

Kadhalika wanachangia Sh. 3, 000 kila mwanafunzi kulipia deni la maji kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu,  Asia Mpata, Kibamba inadawa na  mamlaka ya Maji safi na Majitaka malimbikizo ya deni la Sh milioni nne.

Waliliambia gazeti hili kuwa wanatozwa Sh 40,000 kusajili na pia unapotaka kuhamisha mtoto unalipia Sh.31,000. Si hivyo  tu, hulipia Sh. 200 za uji, 10,000 za madawati, pia wanalipia ulinzi na ujenzi wa vyoo.

Mwalimu Mkuu, Mpata akijibu malalamiko hayo ya wazazi, alisema michango hiyo imepitishwa na kamati za shule na wazazi hivyo wasilalamike.

"Wanaolalamika ni wale wasioitoa wanapaswa kupeleka malalamiko yao kwenye kamati ya shule na ofisi ya kata,fedha  hizo zinatumika kukarabati madawati na kuweka sakafu  kwani iliyopo imechakaa, tunachangamoto ya madarasa kwa sasa kila darasa wanafunzi ni  100", alisema.

Aidha, alisema shule haina vyoo na kinachotumika sasa ni hatari kwa wanafunzi na kwamba uongozi unatarajia kufunga shule hadi kukamilisha ujenzi wa vyoo.

“Vyoo ni tatizo yapo matundu sita ya shimo vinavyotumiwa na watoto 1,300 hii inakwenda kinyume na sera ya elimu. Tuna wanafunzi 100 kwa kila darasa wakati wanatakiwa kuwa 45,” alisema.

Afisa Elimu wa Wilaya ya Kinondoni, Kivule Takwimu aliungana na kauli ya waziri Majaliwa kuwa, hakuna michango ya kusajili wanafunzi.

“Serikali ilizitaka shule za msingi kuwa na kamati za shule ili kunusuru mambo muhimu ambayo wazazi wana uwezo wa kuchangia kidogo na hili linafanyika kupitia kamati na si vinginevyo,” alisema.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post