Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam limewaachia huru
vijana 119 wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu maarufu kama
‘panya road’ baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosha.
Kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova
amesema vijana hao walianza kukamatwa Januari 3 mwaka huu na hadi sasa
wamekamatwa watuhumiwa 1,508.
Kamanda Kova amesema watuhumiwa 119 walioachiwa
huru nyendo zao zinafuatiliwa endapo watabainika wanajihusisha na
uhalifu wa aina yeyote watakamatwa kwenye msako unaoendelea.
“Mpaka sasa tumewakamata vijana 1,508 kwa tuhuma
za wizi, kujeruhi, kujihusisha na dawa za kulevya, wapiga debe waliokuwa
wakiwabugudhi abiria, kucheza kamari, biashara ya ukahaba na
mikusanyiko isiyo ya halali katika vijiwe, tunaendelea kufanya nao
mahojiano", amesema Kamanda Kova.
Amesema pamoja na watuhumiwa hao kukamatwa hadi
sasa vijana 959 tayari wameshafikishwa katika mahakama mbalimbali za
jijini Dar es Salaam kwa mujibu wa sheria.
Aidha Kamanda Kova amesema watuhumiwa wengine 430
wameachiwa kwa dhamana wakisubiri kukamilika kwa upelelezi huku nyendo
zao zikifuatiliwa kwa ukaribu kwa kushirikiana na wazazi wao na
viongozi wa maeneo yanayowazunguka.
Kamanda Kova ametoa wito kwa raia wema
kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhakika ili
makundi yanayofanya uhalifu wa aina ya panya road na mengine yaweze
kutokomezwa .
“Raha ya jeshi la Polisi nchini ni kuona wananchi
wa jiji la Dar es Salaam na watanzania wote kwa ujumla waishi na kufanya
shughuli zao za kijamii na kiuchumi kwa amani na utulivu uliozoeleka,
hivyo tutachukua hatua stahiki ili kukabiliana na uhalifu wowote
unaoweza kuharibu amani ya nchi," amesema Kamanda Kova
Amesema jeshi hilo litaendelea kufanya msako
maeneo mbali ya Dar es Salaam na mikoa mingine ili kuhakikisha matukio,
ama makundi ya kihalifu yanamalizika kabisa.
إرسال تعليق