Dar es Salaam. Kuna njia mmoja tu ya kupambana
na vijana waliokata tamaa ya maisha maarufu kama Panya Road waliopo
katika jiji la Dar es Salaam.
Ni rahisi kuwadharau vijana hao, lakini makundi
yote makubwa ya kigaidi au yale ambayo yanasumbua nchi mbalimbali
duniani yalianza kimasihara hivihivi kama walivyo Panya Road wa Dar es
Salaam.
Hawa ni vijana ambao wamekataa tamaa na jinsi
mambo yanavyoendeshwa nchini. Wamefika katika hatua ya ‘alienation’ au
kwa lugha nyepesi unaweza kusema wamejikataa au kudhani dunia
imewakataa.
Kisaikolojia, ‘alienation’ ni hatua ya mwisho
kabisa kabla ya mtu kuamua kujiua. Ndiyo maana watu wanaodhani vijana
hawa ni wahuni wanakosea, badala yake wanapaswa kujua sababu kuu
inayowafanya wafanye vurugu na si kuwalaumu tu.
Vijana hawa wamejikataa na ndiyo maana hawataki
kujiita majina ya binadamu, badala yake wamejipachika majina ya wanyama
kama ‘panya’ au watoto wa mbwa mwitu. Kwa hatua waliyofika, huwezi
kuwadharau tena kama viongozi wetu wanavyofanya sasa kwa kutoa lugha ya
vitisho.
Ni rahisi kwa Serikali kusema ‘tutawadhibiti’,
lakini kuna njia moja kubwa ya kuwadhibiti ambayo itakuwa ni suluhisho
la kudumu na si kutumia nguvu kama dola inavyofanya.
Hawa vijana wamekata tamaa ya maisha, hawana kazi,
wamekuwa wakiishi kwa mfumo wa uchumi unaoitwa ‘hand to mouth’ yaani
‘mkono kwa mdomo’, kila wanachokipata kwa siku kinakwenda mdomoni,
hawana akiba yoyote.
Hawawezi kuweka akiba yoyote, kila wanachokipata
wanakitumia leo na hawana uhakika wa kesho. Hayo ndiyo maisha yao ya
kila siku. Kwao hakuna maisha bora kwa kila Mtanzania ila kuna bora
maisha kwa kila Mtanzania.
Inapofikia hali hiyo, binadamu huwa anakataa tamaa
na inapofika hatua hiyo mtu huwa hajui sababu inayomtia hasira na ndiyo
maana ukiwauliza vijana hao wa Panya Road kwa nini wanapora mali za
watu watakwambia kwa sababu mwenzao kauawa, kapigwa au kakamatwa na
polisi. Huwa hawajui sababu ya msingi kwa kuwa imejificha.
Wanachokieleza huwa si sababu ya msingi, bali
kichocheo tu cha sababu ya wao kuibuka barabarani na kupora mali za watu
na kuwaacha wengi wakiwa na maumivu kutokana na vipigo.
Sababu kubwa za kuibuka makundi kama haya ni
kwamba rasilimali nyingi za nchi zimeshikiliwa na watu wachache na
kwamba hakuna mgawanyo sawa wa rasilimali hizo kwa watu wote. Kuna
wachache wanachukua kila kitu wakati wapo wengi ambao hawapati kabisa.
Unapoambiwa nchi hii ina madini, ina mbuga za
wanyama, bahari, Mlima Kilimanjaro, mito, maziwa, misitu na rasilimali
nyinginezo unashangaa kuona kuna kundi kubwa la watu wakiishi maisha
ambayo hayana uhakika wa kesho.

Post a Comment