Phiri atoa ya moyoni Simba

Kocha Patrick Phiri amesema Simba haiwezi kufika popote kama wataendelea na tabia ya kufukuza makocha kila mara. Phiri (pichani) ameondoka nchini jana asubuhi kurudi kwao Zambia baada ya viongozi wa Simba kusitisha ajira baada ya kuifundisha timu hiyo kwa miezi minne.
Phiri alisema hapingani na uamuzi uliochukuliwa na viongozi wake juu ya kusitisha mkataba wake, lakini siyo sahihi kufukuza kocha wakati ligi inaendelea kwani kwa kufanya hivyo ni kuivuruga timu.
Phiri alisema kuwa inasikitisha kuona timu moja inafundishwa na makocha watatu kwa msimu mmoja na kuongeza kuwa ni hatari na kumtaka Rais wa Simba, Evans Aveva kuwa makini katika kufanya uamuzi juu ya hilo.
“Kama mfumo wa Simba utaendelea kuwa hivi kwa kufukuza makocha na makundi kwa wachezaji, basi hawawezi kufika popote, watakuwa wanapiga hatua moja mbele wanarudi hatua tatu nyuma, nimeikuta Simba ikiwa mpya kwa maana wachezaji wengi walikuwa wageni, lakini walianza kuelewana.
“Simba hii naamini itakuwa nzuri hapo baadaye, lakini kubadilisha makocha kwa upande mwingine siyo vizuri kwani ataanza kuwafundisha upya, wale walioanza kuelewana wanaweza kupotea kabisa, kutengeneza timu kunatakiwa kuwepo na uvumilivu kwani inachukua muda mrefu timu kukaa sawa,” alisema Phiri.
Alisema kuwa awali viongozi hao walisita kumwambia ukweli juu ya ajira yake baada ya kumleta kocha mpya Mserbia Goran Kopunovic kwa kile walichodai kuwa yeye bado ni mwajiriwa wa klabu hiyo.
“Niliposikia juu ya kufukuzwa kwangu niliwauliza, lakini  hawakuwa wawazi kwangu ndipo nilipomwambia Rais Aveva kwani ni rafiki yangu mkubwa kwamba aniruhusu  nirudi kwetu kwa mapumziko, lakini baadaye Aveva nilikutana naye na kuzungumza juu ya hilo, kikubwa nawatakia kila la heri ili wafanye vizuri kwenye mechi zilizobaki, inawezekana wameanza vibaya na wakamaliza vizuri japokuwa simfahamu huyu kocha ila naamini makocha wa kanda hiyo ni wazuri,” alisema Phiri.
Akizungumzia soka la Tanzania kwa jumla, Phiri alisema “Soka la Tanzania linaweza kupanda endapo tu kutakuwa na misingi mizuri kuanzia kwenye klabu, mfumo wa klabu za hapa nchini ni mbovu, soka la Tanzania kwa sasa linafanywa kisiasa zaidi, hilo ni tatizo na linarudisha nyuma maendeleo ya soka, viongozi wa soka wanatakiwa kuwa wanamichezo, wenye uchungu na soka.”

Post a Comment

Previous Post Next Post