Dk. Mokiwa: Watanzania wachague viongozi wasing'ang'anie vyama

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk. Valentane Mokiwa akiongea wakati wa kuadhimisha Jubilee ya miaka 50 ya Dayosisis hiyo jijini Dar es Salaam jana.
Watanzania wametakiwa kuchagua Rais na wabunge watakaotatua matatizo yanayowakabili pamoja na taifa badala ya kung’ang’ania vyama vya siasa ambavyo hutaka kuingia madarakani hata kwa udanganyifu.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk. Valentane Mokiwa, alisema jana jijini Dar es Salaam  wakati akizungumzia jubilee ya miaka 50 ya dayosisi hiyo.

Aidha, alisema katika suala la kutafuta kiongozi wasiangalie vyama kinachotakiwa kutizamwa ni uwezo wa mtu katika kushughulikia changamoto zinazoikabili taifa.

“Wakati wa Watanzania kudanganywa na viongozi umekwisha,” alisema na kuongeza kuwa kuna udanganyifu mwingi wakati wa uchaguzi mkuu lakini si mikakati inayotekelezeka ya kutatua matatizo ya nchi.

“Tusikubali kudanganywa na hao viongozi,msiangalie chama mtizameni mgombea atayekabili matatizo ya msingi yanayolikabili taifa” alisisitiza.

Askofu Mokiwa alisema:”Kiongozi ni yule ambaye anaweka mahitaji ya nchi mbele hivyo usibatize uso wa mtu angalia changamoto za Tanzania tuwapime kwa matatizo kwani tumechoka kudanganywa tubadilike ,”

Aliyataja baadhi ya matatizo kuwa afya duni na kuendelea kuona wagonjwa wanapelekwa nje kutibiwa.

Aliongezea “Taasisi za afya zisihujumiwe, hivyo akipatikana kiongozi atakayeshughulikia changamoto hizi ndiye tutakayemchagua kwa sasa bado hatujamjua Rais ajaye na hatutaangalia chama,” alisema Askofu Mokiwa

Alitaja elimu kuwa nayo inahitaji kuboreshwa,miundombinu iliyochakaa, kukosekana ulinzi wa kutosha mipakani na kusababisha wahalifu na bidhaa kupita na kuhatarisha amani na uchumi pia.

 “Tumezoea wanatudanganya eti nikishinda nitaweka maji nitajenga shule hizo ni sera za kisiasa suala la maji ama shule ni haki za watu na serikali ni wajibu wake kutekeleza na siyo mtudanganye,’ alisema Askofu Mokiwa



Akizungumzia jubilee hiyo itakayofanyika kesho katika Kanisa la Mtakatifu Albano alisema siku hiyo itakuwa na matukio mbalimbali pamoja na makongamano kwa vijana.

Alisema vijana wataelimishwa masuala mbalimbali ikiwamo kufahamu umuhimu wa kujiajiri pamoja na kujihami na mambo ya ngono.

 “Tutasherekea miaka 50 kwa kuonyesha jinsi ambavyo kanisa  limewekeza na kuendesha shughuli za kiuchumi na kijamii bila ubaguzi wa rangi ama dini,” alisema Askofu Mokiwa

Alisema mikakati ya miaka 50 ijayo itajikita zaidi katika utoaji wa elimu bora kuanzia hatua za awali, msingi, sekondari hadi elimu ya juu.

“Moja ya mikakati ni kukuza elimu na mawasiliamo itakuwa ni kuandaa mpango wa kukusanya fedha za kuinua kiwango cha elimu na kuanzisha kitengo cha mawasiliano kwa nia ya redio na gazeti na baadaye tutaanzisha televisheni,” alisema Askofu Mokiwa.

Alisema watatilia mkazo katika kuanzisha mafunzo ya ufundi stadi kwa watakaokosa kujiunga na elimu ya sekondari ikiwa ni sehemu ya kuongeza ajira kwa vijana.

Mbali na hilo alisema Kanisa linajenga kituo kwa ajili ya kuwajengea maisha watoto ambao hawana wazazi na kwamba  litawajibika katika kuwasaidia kupata huduma zote za msingi.
 

Pia aliwataka wananchi wasikubali kurubuniwa kwa rushwa katika kuwachagua viongozi waongo kwani wataipeleka nchi pabaya.

Post a Comment

Previous Post Next Post