MWANDISHI Richard Manyota/UWAZI UNAPOZUNGUMZIA
ulinzi katika nchi zilizoendelea ni jukumu la kila mtu, lakini kwa hapa
nyumbani ni kazi ya polisi hata kama ukweli uko wazi kwamba, uwiano wa
polisi na raia umepishana kwa kiwango kikubwa.
Ulipotokea mtikisiko wa kundi la uasi la Panya Road jijini Dar es
Salaam, hivi karibuni yamesemwa mengi; machache nataka kuyajengea hoja
katika kushibisha makala haya niliyoyapa kichwa cha habari hapo juu.
KWANZA; polisi wetu walivyolishughulikia tatizo. Nilikuwa miongoni
mwa watu waliotaharuki mno siku ya tukio la hofu ya Panya Road. Katika
hali ya kawaida ukubwa wa hofu haukulingana hata kidogo na tukio husika.
Mahali nilipokuwepo watu walitawanyika huku wakitelekeza simu za
thamani mezani kwa mayowe tu ya “Panya Road.” Lakini miongoni mwetu
hakuna aliyemuona siyo Panya Road hata mende njiani hawakuwepo kabisa.
Kwa kutambua umuhimu wa utulivu, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Suleiman Kova alitoa ufafanuzi kupitia vyombo vya habari usiku
ule akiwaambia wananchi kuwa tatizo siyo kubwa kwa kiwango hicho;
alisema lipo lakini limedhibitiwa na dola.
Kwangu mimi, taarifa hiyo ilikuwa muhimu kwa sababu ilirejesha
utulivu. Mahali ambapo wanawake hawakuchagua pa kujificha au kukimbilia
na hatimaye kufanyiwa vitendo vibaya na watovu wa nidhamu (siyo Panya
Road) walipata ahuweni na kuzitumia fahamu zao kujilinda. Nia ya
kurejesha utulivu ilitimia; pongezi kwa polisi.
Natafakari KIZAZI CHA WAKOSOAJI; kasumba inayojengeka hivi sasa
miongoni mwa jamii ni uhodari wa mtu kupimwa kwa uwezo wa ukosoaji.
Tumeshuhudia baadhi ya wananchi na vyombo vya habari vikikosoa kauli ya
kamanda iliyosema tatizo halikuwa kubwa. Wanaosema hivyo kwa maana
nyingine walipenda kumsikia kamanda Kova akiwaambia wananchi tatizo ni
kubwa na hivyo waendelee kutawanyika. Ujinga mtupu!
Hii ndiyo akili ya kizazi cha ukosoaji ambayo haipaswi kupewa nafasi
kwenye nchi hii. Maana wamesikika wenye akili hizo wakihoji: “Mbona Kova
alisema Panya Road ni watu 15 sasa hao 1,000 wanaosema wamewakamata
wamewatoa wapi?”
Najiuliza mwandishi wa habari anayeweza kuhoji kitu kidogo namna hii
ufahamu wake ukoje? Wanaosomea udaktari wanaelewa ninachosema, maana ni
wazi kwenye kila ugonjwa kuna dalili. Panya Road kama ugonjwa huwezi
kuutibu bila kuangalia dalili.
Watu 1,000 wanaotangazwa kukamatwa ni namna ya daktari kushughulika
na dalili ya Panya Road. Ugumu wa kuelewa uko wapi kwenye jambo hili.
Nimetembea zaidi ya vituo 14 vya polisi hapa Dar es Salaam, cha mwisho
ni Urafiki lengo likiwa ni kujielimisha juu ya sakata hili.
Kila nilipofika wakuu wa vituo waliniambia wamewakamata vijana wengi
(hao wanaotajwa kwa idadi ya 1,000) wenye dalili za Panya Road. Miongoni
mwao ni wapiga debe, wavuta bangi, wazururaji, wauza madawa ya kulevya
na kadhalika.
Lengo la polisi ni kutambua dalili za tatizo kuelekea kwenye tiba ya
Panya Road. Cha kushangaza pamoja na kazi nzuri ya polisi kizazi cha
kupinga hakitaki kukubaliana na hilo kwa sababu siku hizi uhodari wa mtu
ni kupinga. Aibu kubwa kwa watu wanaojiita wasomi nao kushindwa
kupambanua mambo.
Miaka nenda rudi tumekuwa na tatizo la vibaka. Sote tunajua sheria
zetu hazikidhi kuwafunga lakini tunawafahamu. Kamanda mmoja aliniambia,
vijiwe vya wabwia unga wanavijua na wahusika wanajulikana. Lakini
kukamata ‘mateja’ vijiweni na kuwalaza vituoni wataishia kuharisha
mahabusu mwisho wa siku hawatafungwa kwa kuwa vidhibiti hakuna.
Tuache siasa; PANYA ROAD ni watoto wetu na ndugu zetu ambao
tumeshindwa kuwalea kama wazazi na taifa limekosa kuwapa fursa ya kuweza
kuishi kwa kuwapatia ajira na elimu. Tusiwalaumu polisi, tujilaumu sisi
pia kwa kushindwa kuwajibika juu ya ulinzi wetu na makengeza ya sheria
zetu! Nachochea tu!
Post a Comment