Dar es Salaam. Meneja Misamaha ya Kodi TRA, Kyabukoba Leonard
Mutabingwa , Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco, Steven Roman Urassa
na Mkurugenzi wa fedha BOT , Julius Rutta Angello wamefikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya kuomba na
kupokea rushwa ya mamilioni ya fedha kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.
Watuhumiwa hao wanafanya idadi ya waliofikishwa
mahakamani kwa kashfa ya miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow kufikia
watano baada ya watumishi wengine wawili wa umma kufikishwa mahakamani
hapo Jumatano iliyopita.
Waliofikishwa mahakamani hapo ni Mkurugenzi wa
Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Rugonzibwa Mujunangoma aliwekewa kiasi cha Sh323 milioni kupitia akaunti
yake namba 00120102602001.
Mwingine ni Mhandisi Mkuu wa Wakala wa Umeme
Vijijini (Rea), Wizara ya Nishati na Madini, Theophillo Bwakea
aliyepokea rushwa ya Sh161,700,000 kupitia akaunti yake namba
004101102643901.
Mahakama ya Kisutu leo
Washtakiwa hao wanaokabiliwa na mashtaka ya kuomba
na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15 (1)(a) cha sheria ya
kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2015, walifikishwa kwa mahakimu
wawili tofauti, Hakimu Mkazi Janeth Kaluyenda na Hakimu Mkazi, Devotha
Kisoka.
Akisoma hati ya mashtaka katika kesi namba 16 ya
2015 inayomkabili Kyabukoba, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai alidai mbele ya Hakimu
Kaluyenda kuwa Januari 27, 2014 katika Benki ya Mkombozi wilaya ya
Ilala , alipokea Sh1.6 bilioni kupitia akaunti namba 00110202613801.
Swai alidai kuwa mshtakiwa huyo akiwa katika
Benki ya Mkombozi alijipatia kiasi hicho cha fedha ambacho ni sehemu
ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow na kwamba alizipokea kutoka kwa
James Burchard Rugemalira ambaye ni Mshauri huru wa Kitaalam,
Mkurugenzi wa VIP Engineering na Mkurugenzi wa zamani wa IPTL kama tuzo
kwa kuiwakilisha kampuni ya Mabibo Beer Wines and Spirits ambayo ni
mali ya Rugemalira mahakamani kitu ambacho ni kinyume cha sheria.
Alidai kuwa Julai 15, 2015, mshtakiwa huyo
Kyabukoba akiwa katika benki hiyo ya Mkombozi alipokea rushwa ya
Sh161.7 milioni, Agosti 26,2014 alipokea tena rushwa ya Sh 161.7 milioni
na Novemba 14, 2014 alijipatia rushwa ya kiasi kingine cha fedha cha
Sh161.7 milioni kupitia kwenye akaunti hiyo, kama tuzo kwa kuiwakilisha
kampuni hiyo ya Rugemalira mahakamani kitu ambacho ni kinyume cha
sheria na kwamba fedha zote hizo ni sehemu ya fedha za Akaunti ya
Tegeta Escrow.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Kyabukoba
aliyakana na upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo umekwisha
kamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya mshtakiwa huyo
kusomewa maelezo ya awali (PH).
إرسال تعليق