Sasa kazi ni moja tu, kudai Tume Huru ya Uchaguzi ili haki itendeke

Tunapouanza mwaka 2015 tujue kwamba huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu kwa wabunge, madiwani pamoja na rais.
Kisiasa ni mwaka wa kihistoria kwa sababu Katiba Inayopendekezwa inapaswa kupigiwa kura ya “Ndiyo” au “Hapana” mwezi Aprili 2015 kama Serikali haitabadili mwelekeo wake.
Mimi ni kama nilivoandika kwamba kura yangu kwa Katiba hiyo ninayoiita ya CCM ni “hapana, hapana, hapana”.
Nitapiga kura ya “Hapana” na kuwashawishi Watanzania wanaopenda mabadiliko na maendeleo kuungana nami kwa sababu katiba hii iliyopendekezwa kwa mabavu ya bunduki na mabomu ya dola, haina masilahi kwa wananchi wa kawaida.
Katiba hii inayopendekezwa, ina kazi moja tu; kulinda ufisadi na mali za kikundi cha watu wa chache ndani ya Serikali ya CCM.
Wewe mwananchi wa kawaida ambaye huna manufaa nayo, utaipigia kura ya kuipitisha ili iweje?
Maoni ya Tume ya Marekebisho ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba yalipendekeza kuwapo kwa “TUME HURU YA UCHAGUZI” ambayo inakidhi mahitaji ya siasa za vyama vingi na sio chama tawala tu cha CCM.
Swali langu ni je, Serikali ya CCM itakubali kuunda Tume Huru ya Uchaguzi, wakati ikijua kwamba ushindi wake katika chaguzi unategemea sana tume hii ya sasa ya CCM chini ya mamlaka ya Rais ambaye ni mwenyekiti wa CCM?
Nathubutu kuandika kwamba, sasa Watanzania wenzangu kazi ni moja tu, yaani kudai kuundwa kwa TUME HURU YA UCHAGUZI” kama ilivyokusudiwa na wananchi kwenye Rasimu ya Katiba.
Chombo hiki ni cha kitaifa si cha chama kimoja. Kwa hivyo wananchi wote bila kujali chama, dini, kabila, cheo, ukanda unakotoka wala rangi, tuungane kudai ili iundwe haraka na kushughulikia masuala yote ya uchaguzi kwa haki, uhuru, uwazi na usawa kwa vyama vyote na kuondokana na malalamiko ya miaka mingi.
Tume hii huru itaratibu sheria na kanuni za uchaguzi, kusimamia uchaguzi wenyewe, kushughulikia kesi na kero pamoja na kuwatangaza washindi wa kweli mwisho wa uchaguzi.
Tume hiyo itashughulika na uboreshwaji wa daftari la wapiga kura nchini Tanzania.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post