Dar es Salaam. Serikali imewasilisha ombi la
kutaka mahakama itupilie mbali maombi ya walalamikaji katika sakata la
Akaunti ya Tegeta Escrow ya kuzuia utekelezaji wa maazimio ya Bunge.
Kesi ya kuzuia utekelezaji huo ilifunguliwa na
kampuni za Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Pan African Power
Solution pamoja na mwenyekiti mtendaji wa kampuni hizo, Singh Seth dhidi
ya Waziri Mkuu na Spika wa Bunge.
Sambamba na kesi hiyo namba 59 ya mwaka 2014, pia
walalamikaji hao walifungua maombi ya zuio la muda la utekelezaji ili
kusubiri uamuzi wa kesi hiyo ya kikatiba na wakiainisha hoja tano,
zitakazofafanuliwa wakati za usikilizwaji.
Katika hoja zake za pingamizi, Serikali inadai
kuwa maombi hayo hayana mashiko kwa kuwa yanakiuka Ibara ya 63 na ya 100
za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 5 cha
Sheria ya Kinga, Mamlaka na Haki za Bunge.
Katika hoja nyingine, Serikali inadai kuwa maombi hayo yameambatanishwa na hati ya kiapo chenye kasoro za kisheria.
Hoja nyingine ni kwamba maombi hayo ni batili kwa kuwa hayakuainisha kifungu cha sheria kinachosimamia.
Pingamizi hilo lilitarajiwa kusikilizwa jana na
jopo la majaji watatu, Agustine Mwarija (kiongozi wa jopo), Gadi Mjemas
na Stellah Mugasha, lakini usikilizwaji huo ulikwama baada ya mawakili
wawili wa IPTL kushindwa kufika mahakamani.
Mmoja wa mawakili wanaotetea walalamikaji,
Melickzedek Lutema aliieleza Mahakama kuwa kiongozi wa jopo la mawakili
wa IPTL, Joseph Makandege ni mgonjwa.
Lutema pia alisema wakili mwingine, Gabriel
Mnyele alisafiri kwenda Mpanda na alitarajiwa kuwasili juzi, lakini
alikosa usafiri.
Aliiomba kesi hiyo iahirishwe ili awasiliane wenzake.
Mahakama ilikubaliana na ombi hilo na kuamua kuwa pingamizi hilo litasikilizwa na jaji mmoja.
Baada ya mawakili wa pande zote kukubaliana, Jaji
Mwarija alisema suala hilo litapelekwa kwa Jaji Kiongozi ili ateue jaji
atakayesikiliza pingamizi hilo na tarehe ya usikilizwaji watajulishwa.
Kesi hiyo itatajwa Januari 13, 2015.
إرسال تعليق