Duru za kuaminika za ndani ya jeshi la Nigeria zimefichua kuwa, asilimia
kubwa ya silaha za kundi la Boko Haram zinatoka ndani ya jeshi la nchi
hiyo na wala hazitoki kwa mtandao wa al Qaida ambao unatuhumiwa kufanya
vitendo vingi vya kigaidi katika nchi jirani za Chad, Niger, Mali na
Mauritania.
Televisheni ya lugha ya Kiingereza ya Aljazeera ya Qatar imezinukuu duru
hizo za jeshi la Nigeria ambazo haikuzitaja jina zikisema kuwa, kuna
uwezekano mkubwa sana kwamba baadhi ya maafisa wa kijeshi wa nchi hiyo
wanashirikiana na Boko Haram.
Matamshi hayo yamekuja baada ya ripota wa televisheni hiyo kuripoti
kutoka Nigeria kwamba, wanamgambo wa Boko Haram leo Jumapili wameanzisha
mashambulizi makubwa dhidi ya mji wa Maiduguri, makao makuu ya jimbo la
Borno pamoja na mji wa Monguno wa jimbo hilo.
Hadi tunaandaa habari hiyo, mapigano makali yalikuwa yanaendelea katika
viunga vya Maiduguri kati ya jeshi na wanamgambo wa Boko Haram. Jeshi la
Nigeria limekuwa likifanya pia mashambulizi ya anga dhidi ya wanamgambo
hao na kutekeleza pia sheria ya hali ya hatari katika mji huo.
Kundi hilo la kitakfiri limeanza operesheni ya kuushambulia mji wa
Maiduguri kutokea katika eneo la Njimtilo. Hivi karibuni pia kundi la
Boko Haram liliripotiwa kufanya mauaji makubwa ya watu katika mji wa
Baga, karibu na mpaka wa Chad baada ya kuuteka mji huo.
cHANZO: kiswahili.irib.ir

إرسال تعليق