SMZ kuwasilisha hati ya dharura kudhibiti mawasiliano

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeshauriwa kuwasilisha katika kikao kijacho cha Baraza la Wawakilishi hati ya dharura ya  muswada wa sheria wa kudhibiti mitandao ya kijamii ikiwa ni njia mojawapo ya kudhibiti matumizi mabaya ya njia za mawasiliano.
Akihutubia mkutano wa hadhara wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi  Zanzibar (UVCCM) , Naibu Katibu Mkuu Shaka Hamdu Shaka, alisema  wakati umefika kwa serikali kuwasilisha muswada huo ili kuzuia matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.

Shaka alisema  mageuzi ya teknolojia na ujio wa utandawazi  kwa  dunia ya tatu ikiwemo Zanzibar umezikuta wakati zikiwa hazijajitayarisha na ujio huo na kwa sababu hiyo hivi  jamii inashuhudia ukiukwaji mkubwa wa maadili, mila na utamaduni  wa kuheshimu utu, huku baadhi ya wamiliki na waendesha mitandao ya kijamii wakiwavunjia heshima wananchi.

“Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema  uhuru bila ya utii ni ujinga na akasema pia uhuru usio na mipaka ni sawa na wendawazimu…kwa maana hiyo sithubutu kukandamiza uhuru wa maoni, ila ninachohimiza ni wajibu katika jamii inayoheshimu umoja, amani na upendo” Alisema Shaka.

Alisema kutungwa kwa sheria hiyo ambayo itahusisha matumizi ya tovuti, umiliki na uendeshaji kutasaidia kuepusha jamii kuingia katika mifarakano inayosababisha na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.

Shaka alitoa mifano ya nchi kadhaa ambazo zimetumbukia katika mifarakano kwa sababu ya chokochoko zilizokuwa zikienezwa katika mitandao ya kijamii.

Akizungumzia hali ya kisiasa, alisema wapinzani na hasa Chama cha CUF wasitegemee kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwani mbinu na ujanja wao wanaotumia hasa katika majimbo ya Pemba umebainika na CCM haitakubali tena mbinu chafu zisizo za kidemokrasia, alisisitiza Shaka.

Post a Comment

أحدث أقدم