TBS kuanzisha 'jeshi' kudhibiti bidhaa feki

Shirika la Viwango (TBS).
Katika jitihada za kupambana na uingizwaji wa bidhaa feki na duni, Shirika la Viwango (TBS), linatarajia kuajiri vijana 200 katika  vituo vya mpakani   pamoja na viwanja vya ndege kwa lengo la kuongeza nguvu ili kukabiliana na tatizo hilo.
Msemaji wa shirika hilo Rhoida Andusamile, alieleza hayo  wakati akihojiwa na kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na  Radio One  Sterio.

Afisa huyo alisema kuna  bidhaa feki  sokoni kutokana na kuwa na mianya mingi ya uingizaji wake  ikiwa ni pamoja na kuzipitisha  mipakani mathalani Tunduma kwa upande wa Zambia , Kasumulu upande wa Malawi, Sirari, Namanga  vituo vya mipaka ya Kenya na viwanja vya ndege vya Dar es Salaam na Kia Arusha.

“Tuna mpango wa kuajiri vijana 200, kwa lengo la kuongeza nguvu ya udhibiti wa uingizaji wa bidhaa hafifu nchini, hawa watakuwa na ofisi mipakani  pamoja na vituo vya uwanja wa ndege,”alifafanua

Rhoida alieleza kuwa  bidhaa zisizo na ubora bado zinazagaa madukani tatizo likiwa ni pamoja na watumiaji kutoelewa madharaa yake  na hata wale wanaoyajua wanazifurahia kwa kisingizio kuwa zina  bei nafuu tofauti na zile zenye ubora unaotakiwa lakini wanasahau gharama za matibabu  ni ghali na madhara yake ni makubwa, iwapo ni za vyakula.

Aidha aliiambia Radio One kuwa shirika hilo limebuni mbinu mbadala wakuwa na alama mpya itakayotumika kwa bidhaa zinazotoka nje. Pia zile    ambazo hazina ubora wa kimataifa hazitaruhusiwa kuuzwa  nchini, mbinu nyingine ni pamoja na kutoa elimu kwa watumiaji hata kwa wale wafanyabiashara wanaoziuza.

Msemaji wa TBS alisema hatua kali zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya wafanyabiashara wa nguo za mitumba ikiwa ni pamoja na wale wanaouza nguo za ndani na kuwashitaki wanauza nguo zilizopigwa marufuku ambazo hazina  viwango.

Hivi karibuni shirika hilo lilifungia kiwanda cha kutengeneza juice mkoani Morogoro na kiwanda cha kutengeneza chumvi cha Sea Salt cha  mkoani Pwani kwa tuhuma za kutengeneza bidhaa zisizo na viwango vya kitaifa na kimataifa na zisizojali  afya za walaji. Mwaka jana 2014 wafanyabiashara 47 walifikishwa mahakamani na kutozwa faini kwa  makosa mbalimbali.

Mdhibiti Ubora wa  TBS Deusdedith Pascal,  alisema kuwa kiwanda hicho hakitaruhusiwa kuendelea na uzalishaji  bidhaa hiyo hadi itakaporekebisha kasoro ikiwa ni pamoja na kuongeza madini joto ndani ya chumvi hiyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post