TRA yasubiri kodi Escrow kwa kina Chenge, Tibaijuka, Wamo Ngeleja, Askofu Kilaini, Jaji Mujulizi

  Wamo Ngeleja, Askofu Kilaini, Jaji Mujulizi
Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.
Ahadi ya Wizara ya Fedha kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano la kuwatoza kodi watu wote waliopata mgawo wa fedha zilizochotwa katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeshindwa kutekelezeka.
Kukwama kwa ahadi hiyo iliyotolewa na Naibu Waziri wa fedha, Mwigulu Nchemba, kumetokana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kueleza kuwa inasubiri kwanza vyombo vya dola vikamilishe uchunguzi zaidi kuhusiana na suala la Escrow.

 Hata hivyo, kauli hiyo ya TRA inapingana na ahadi iliyotolewa na Nchemba wakati wa mkutano wa bunge wa 16 na 17 alipolieleza Bunge wakati wa mjadala wa sakata la akaunti ya  Escrow kwamba watu wote waliopokea mgawo watalipa kodi ya mapato kabla ya Desemba 31, mwaka jana na atakayeshindwa baada ya hapo TRA itamshukia.

Wakati wa mkutano huo, Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) iliwataja watu waliopewa mgawo wa fedha hizo kutoka kampuni ya VIP Engineering kuwa ni aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka (sh. bilioni 1.6), ambaye ametimuliwa kazi na Rais Jakaya Kikwete kwa kupokea kiasi hicho kikubwa cha fedha kupitia akaunti yake binafsi badala ya akaunti za shule na kwamba ni kinyume na maadili.

 Wengine ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge (Sh1.6 bilioni); aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye pia ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (Sh. 40.4 milioni) na Mbunge mstaafu wa Sumbawanga (CCM), Paul Kimiti (Sh 40.4 milioni).

Wengine ni aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh. 40.4 milioni); aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk. Enos Bukuku (Sh. 161.7 milioni), Majaji wa Mahakama Kuu, Profesa Eudes Ruhangisa (Sh. 404.25 milioni) na Jaji Aloysius Mujulizi (Sh. 40.4 milioni) pamoja na Mkurugenzi mstaafu wa Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita), Philip Saliboko (Sh. 40.4 milioni).

Pia wamo aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Daniel Ole Naiko (Sh. 40.4 milioni), Ofisa wa TRA, Lucy Appollo (Sh. 80.8 milioni); Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Dk. Methodius Kilaini (Sh. 80.9 milioni); Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa (Sh. 40.4 milioni) na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh. 40.4 milioni).

KAULI YA TRA
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, akizungumza na NIPASHE iliyotaka kujua  kama kodi imeanza kukusanywa kutoka kwa wanufaika wa mgawo huo, hao alisema utekelezaji wake bado haujaanza kutokana na kusubiri uchunguzi zaidi unaofanywa na vyombo vya dola.

“Kama ulivyosikia Mheshimiwa Rais alivyosema kwamba kuna vyombo vya dola vitachunguza zaidi suala hili la akaunti ya Tergeta Escrow mbali na uchunguzi uliofanywa na Kamati ya Hesabu za Serikali na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu Hesabu za Serikali, na sisi TRA tunasubiri uchunguzi ukamilike,” alisema Kayombo.

Kayombo alisema matokeo yatakayotokana na uchunguzi huo ndio yatatoa mwanga kama viongozi hao waliopata mgawo wa fedha za Escrow wanastahili kutozwa kodi au la.

Alisema pamoja na kwamba mtu kupata fedha ni mapato, lakini uchunguzi utakapofanyika utatoa ufafanuzi mzuri na baada ya hapo taratibu za kuwatoza fedha wahusika zitafuata.

 Pamoja na TRA kusema kwamba wanasubiri uchunguzi ambao Rais Kikwete aliagiza ufanyike, lakini baadhi ya wanaotajwa kupokea mgawo wa fedha hizo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa VIP Engineering and Marketing Ltd, James Rugamalira, wameshakiri kuzipokea mamilioni hayo ya fedha.

 Baadhi ya waliokiri kupokea fedha hizo kutoka kwa Rugemalira ni Prof. Tibaijuka, Askofu Nzigilwa, Ole Naiko, Askofu Kilaini, Jaji Ruhangisa.

 Walieleza kwamba walipokea fedha hizo kutokana na mahusiano yao ya karibu na mkurugenzi huyo.

MKUYA, NCHEMBA, MALIMA KIMYA
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na Naibu wake, Nchemba walipotafutwa kwa siku tatu mfululizo simu zao zilikuwa zikiita bila kupokelewa na hata walipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) kuulizwa suala hilo hawakujibu.

Naibu Waziri mwingine, Adam Malima alipotafutwa jana, simu yake ilikuwa inaita bila majibu na hata alipotumiwa sms hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.

KATIBU MKUU ANENA
Hata hivyo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwalile, alipoulizwa jana, alisema suala hilo litatolewa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari na Waziri Mkuya.

Wakati wa mkutano wa Bunge ulioahirishwa Novemba 29, mwaka jana, Nchemba alisema watu waliopokea mgawo wa fedha hizo watapewa fomu za kuthibitisha mapato yao ili wakatwe kodi kutokana na fedha hizo ambazo pia zinapaswa kuhakikiwa na vyombo vya usalama kwamba ni mapato halali.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mapato ya Kodi ya 2012  inaelekeza mlipaji wa kodi kuwasilisha ankara za hesabu za mapato yake kwa TRA kila ifikapo mwisho wa mwaka na hesabu hizo huiwezesha mamlaka hiyo kutathmini kiwango cha kodi inayopaswa kulipwa na mhusika.

Kama waliotajwa kupata mgao huo watakatwa asilimia 30 ya fedha walizopewa kama kodi ya mapato, TRA itakusanya zaidi ya Sh. 9.3 bilioni.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم