Waziri mkuu Mizengo Pinda.
MWAKA 1985 wakati Mwalimu Julius Nyerere alipong’atuka serikalini na kubakia kuwa kwenye chama, nilikuwa bado mdogo nisiyejua hata kusoma magazeti. Lakini miaka kadhaa mbele, nikagundua kuwa uamuzi wa Baba wa Taifa, ulikuwa wa ghafla na ambao haukutegemewa.
Nimesikia simulizi nyingi zinazomhusu Mwalimu, lakini karibu zote, zikimuonyesha kama mtu wa aina ya peke yake, asiyefanana hata kidogo na wanasiasa wengine, wakiwemo aliofanya nao kazi. Lakini katika simulizi zote, ninavutiwa na moja tu, inayosema kuwa enzi zake, mtu yeyote, kwa nafasi yoyote aliyonayo, ilikuwa akisikia anaitwa Ikulu, woga ulimtawala!
Kwa nini waliogopa? Ni kwa sababu Mwalimu alikuwa hatabiriki, ilikuwa ni vigumu kujua kama utendaji wao wa kazi ameufurahia au la. Ninao mfano mmoja. Waziri mmoja alisubiri Baba wa Taifa kasafiri kwenda ng’ambo, akatumia muda huo kukarabati njia iendayo nyumbani kwake, kule Msasani.
Aliporudi, akitaraji angesifiwa, badala yake almanusura apoteze kazi, maana aliulizwa ni wapi alikopata fedha za kufanya ukarabati ule, kwa sababu Mwalimu anajua hakukuwa na bajeti ya ujenzi ule.
Kama hata Waziri Mkuu aliogopa alipoitwa ofisi kubwa, ni wazi kuwa Ikulu iliheshimika. Baada ya Mwalimu kuondoka Magogoni, kidogokidogo hadhi yake ilianza kupungua. Mzee Ruksa aliwakaribisha wafanyabiashara Ikulu, waliokwenda kwa kisingizio cha ufadhili wa mpira kwa klabu za Simba na Yanga, tunawakumbuka!
Hii ilipunguza heshima ya Ikulu, ikaonekana kama mtu akifanya ujanjaujanja anaweza kupenya na kujikuta Magogoni.Siwakumbuki washindani wa Ali Hassan Mwinyi katika Urais wa Tanzania baada ya Mwalimu, lakini natambua mwaka 1995, ilibidi Baba wa Taifa aingilie kati, wakati wana-CCM wengi walipojitokeza kutaka urithi wa mzee Ruksa, bila shaka baada ya kuona kumbe Ikulu ni sehemu ya kujidai, badala ya kuwatumikia wananchi.
Ni wakati wa Mwinyi ndipo wajanja wengi walipoibuka na kujipatia fedha nyingi zisizo na maelezo. Katika kipindi cha miaka kumi ya utawala wake, fedha zetu zilishuka thamani na noti zilipanda harakaharaka, kutoka ile ya shilingi mia mbili, hadi elfu kumi!
Mwanzoni mwa miaka ya 2000, chama cha soka nchini (FAT) enzi hizo, kilikuwa kinafanya uchaguzi baada ya Muhidin Ndolanga (Mwenyekiti) kuwa amezuiwa na serikali kushiriki. Watu wengi walijitokeza kuchukua fomu. Aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya soka wakati huo, Burkhad Pape, raia wa Ujerumani, baada ya mazoezi ya Stars pale Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) aliniambia;
“Katika Ujerumani ni watu wawili au watatu wangejitokeza kuwania hii nafasi, kwa sababu ni nafasi kubwa na nyeti, inaonekana Tanzania kuna watu wengi sana wanaoweza uongozi.”Ilikuwa ni kauli ya kejeli, maana alipomaliza kuitamka, alinitazama usoni na kuibetua midomo yake kwa staili ya kukejeli. Nilimwelewa!
Kuna kitu alikiongeza, akaniambia ukiona watu wanakimbilia nafasi kubwa na nyeti, wanafikiria kunufaika nayo, vinginevyo zile ni kazi za lawama zinazoweza kugharimu maisha ya watu. Ndiyo, tumeshuhudia mara nyingi Ulaya, mashabiki wa soka wanapoteza maisha!
Sasa tunapoona watu wanakimbilia ofisi kubwa kuliko zote, tena wakiwa tayari kutapanya mabilioni ya fedha ili kuifikia, ni wazi kuwa taasisi imezidiwa.Siamini katika maneno ya yule Mjerumani eti tuna watu wengi wanaoweza uongozi. Zaidi ya nusu ya wanaoomba wamewahi kuwa viongozi serikalini, kama kweli wao ni wazuri, taifa letu lingekuwa hatua nyingi mbele kuliko hapa tulipo.
Umeshika nafasi kubwa serikalini kwa miaka 15 na bado ulishindwa kulisaidia taifa kujikwamua hata kwa wananchi wake kujimudu kwa chakula tu, tena katika ardhi kubwa na yenye rutuba, sembuse leo unakuja na sera za kulisogeza mbele taifa kwa sababu ya gesi?
Wanaimba kila siku kuwa kilimo ndiyo uti wa mgongo, lakini ni viongozi hawahawa wameshindwa kupunguza bei za pembejeo, wameshindwa kulinda soko la mazao na wanashirikiana na wafanyabiashara kuwaibia wakulima kwa kununua bidhaa zao kwa bei ya chini, lakini wakibariki uuzwaji wa bei kubwa kwa walaji!
Tuwe makini, hawa wanaogongana kuwania hiyo nafasi kubwa kabisa, wanatafuta masilahi yao, siyo yetu. Tuangalie nani anatupigania kwa dhati, tusifuate mlio wa shilingi sakafuni, hujui kama ilipoangukia ndipo iliposimama au inaendelea kuvingirika!
إرسال تعليق