Matumizi ya vijiti vya kuchokoa meno maarufu kama ‘toothpick’ ni
namna nyepesi zaidi ya kuondoa mabaki ya nyama, mboga za majani au
matunda yaliyonasa katika meno badala ya kufanya hivyo kwa kidole ama
kitu kingine.
Wapo wengine ambao hata kama wamekwishaondoa mabaki ya vyakula kwenye meno huona raha kutembea huku wakikitafuna kijiti hicho.
Unaifahamu hatari ya kutumia vijiti hivi ambavyo pengine ni biashara kubwa ya watu wengi hapa nchini?
Hatari ya vijiti hivi inayotajwa na Daktari bingwa
wa meno kutoka Kliniki ya Meno ya SD, Israel Kombole ni kupanua fizi
kunakochangia jino kushambuliwa kirahisi na magonjwa na hata kung’oka
kwa meno.
Tabia ya kuchokoa meno inaelezwa na Dk Kombole
kuwa inasababisha kutanuka kwa fizi ambako huweza kuwa hifadhi ya mabaki
ya chakula ambayo yakioza huwa ndicho chanzo cha kuharibika kwa meno.
“Meno yanaathirika kwa urahisi zaidi halafu vijiti
hivi husababisha hata mtu akaharibu umbile la meno kwa sababu
atakapozoea basi nafasi ya jino na jino huongezeka,” anasema
Mbadala wa vijiti hivi unatajwa na Dk Kombole kuwa ni uzi mwembamba maalumu kwa kuondolea uchafu kwenye meno.
Sambamba na kutengeneza mashimo kwenye fizi, pia vijiti hivi vinaelezwa kuwa husababisha mdomo kuwa na vidonda mara kwa mara.
“Mtu anayetumia toothpick mara kwa mara hupata
vidonda mdomoni kutokana na kukwaruzwa na mara nyingi, mtumiaji anaweza
asihisi kama amepata jeraha. Baadaye anaweza kubaini kuwa amepata
vidonda na kumbe vidonda vimesababishwa na toothpick,” anasema.
Vidonda hivi, Dk Kombole anasema huweza kuwa vikubwa hasa pale bakteria wanapoingia kupitia uchafu ule ule ulio katika meno.
Anaeleza madhara mengine ni kupata tatizo la kuvuja damu mara kwa mara kutokana na tabia ya kuchokoa kila baada ya kula.
“Kama ‘toothpick’ itakandamizwa kwa nguvu mdomoni,
inaweza kuleta kidonda ama mchubuko hivyo mara nyingine kufanya
kidonda, pia kama wapenzi watapigana busu muda huo huo baada ya
kujichokoa, uwezekano wa maambukizi ya magonjwa ni mkubwa,” anasema Dk
Kombole.

Post a Comment