Vichokoa meno vizuri ila vyaweza kukuathiri fizi, meno

Matumizi ya vijiti vya kuchokoa meno maarufu kama ‘toothpick’ ni namna nyepesi zaidi ya kuondoa mabaki ya nyama, mboga za majani au matunda yaliyonasa katika meno badala ya kufanya hivyo kwa kidole ama kitu kingine.
Wapo wengine ambao hata kama wamekwishaondoa mabaki ya vyakula kwenye meno huona raha kutembea huku wakikitafuna kijiti hicho.
Unaifahamu hatari ya kutumia vijiti hivi ambavyo pengine ni biashara kubwa ya watu wengi hapa nchini?
Hatari ya vijiti hivi inayotajwa na Daktari bingwa wa meno kutoka Kliniki ya Meno ya SD, Israel Kombole ni kupanua fizi kunakochangia jino kushambuliwa kirahisi na magonjwa na hata kung’oka kwa meno.
Tabia ya kuchokoa meno inaelezwa na Dk Kombole kuwa inasababisha kutanuka kwa fizi ambako huweza kuwa hifadhi ya mabaki ya chakula ambayo yakioza huwa ndicho chanzo cha kuharibika kwa meno.
“Meno yanaathirika kwa urahisi zaidi halafu vijiti hivi husababisha hata mtu akaharibu umbile la meno kwa sababu atakapozoea basi nafasi ya jino na jino huongezeka,” anasema
Mbadala wa vijiti hivi unatajwa na Dk Kombole kuwa ni uzi mwembamba maalumu kwa kuondolea uchafu kwenye meno.
Sambamba na kutengeneza mashimo kwenye fizi, pia vijiti hivi vinaelezwa kuwa husababisha mdomo kuwa na vidonda mara kwa mara.
“Mtu anayetumia toothpick mara kwa mara hupata vidonda mdomoni kutokana na kukwaruzwa na mara nyingi, mtumiaji anaweza asihisi kama amepata jeraha. Baadaye anaweza kubaini kuwa amepata vidonda na kumbe vidonda vimesababishwa na toothpick,” anasema.
Vidonda hivi, Dk Kombole anasema huweza kuwa vikubwa hasa pale bakteria wanapoingia kupitia uchafu ule ule ulio katika meno.
Anaeleza madhara mengine ni kupata tatizo la kuvuja damu mara kwa mara kutokana na tabia ya kuchokoa kila baada ya kula.
“Kama ‘toothpick’ itakandamizwa kwa nguvu mdomoni, inaweza kuleta kidonda ama mchubuko hivyo mara nyingine kufanya kidonda, pia kama wapenzi watapigana busu muda huo huo baada ya kujichokoa, uwezekano wa maambukizi ya magonjwa ni mkubwa,” anasema Dk Kombole.

Post a Comment

أحدث أقدم