Vijana Watatu wa Ubungo Kibangu wadai kuteswa na wanajeshi wa kambi ya Makoka

WANAJESHI wapatao wanane wanadaiwa kuwatesa na kuwapiga vijana watatu katika eneo la Ubungo Kibangu, Dar es Salaam pasipokuwa na sababu maalumu.
 
Wakizungumza na mwandishi wetu jana, vijana hao walieleza kuwa walikamatwa na wanajeshi hao na kupelekwa porini kisha wakateswa na kupigwa kwa zaidi ya saa tano bila kufahamu kosa lao na hata walipohoji waliambiwa hawaruhusiwi kuhoji wanajeshi.
 
Mmoja wa vijana hao, Sebastian Mlekano (40) alisema saa 12:30 jioni ya Januari 13 mwaka huu katika eneo la Ubungo Kibangu karibu na kambi ya jeshi ya Makoka, alisimamishwa na wanajeshi wapatao wanane na kuamuriwa wakae chini.
 
“Nilikuwa napita njia iliyopo karibu na jeshi nikakutana na kundi la wanajeshi wapatao wanane na wakaniambia kaa chini. Nikawauliza nimefanyaje? Wakanijibu wewe huoni sisi ni wanajeshi hupaswi kuuliza umefanya nini.”
 
“Baada ya hapo wakaniambia wewe tufuate, hatua chache mbele tukakutana na kijana mmoja na alipoona mimi nipo chini ya ulinzi aliamua kukimbia na wakamkimbiza na kumkamata kisha wakatupeleka porini. Tulipofika kule muda mfupi wakamleta na mtu mwingine tukafikia idadi ya watu watatu."
 
Aliendelea kuongeza kuwa, “Tulipofikishwa porini tukaanza kufanyishwa mazoezi magumu na kupigwa sana kama ambavyo unaona majeraha haya yote. Nilizimia kwa muda na nilipopata fahamu kipigo kiliendelea kama kawaida kwa muda usiopungua saa tano,” alisema Mlekano.
 
Alisema walipoona wamewaumiza sana waliamua kuwaachia huru na wakarudi majumbani kwao.
 
Walipofika barabarani kutokea porini kwenye mateso, walikutana na kundi kubwa la watu waliokuwa wanawafuata kwani mama mzazi wa Godfrey Mchari alikuwa amemtuma mwanawe dukani na alipoona amechelewa aliamua kuongozana na majirani kujua hatma ya mtoto wake.
 
“Godfrey alipomwona mama yake na kundi hilo la watu waliotufuata alianguka chini akazimia, wakambeba na kumpeleka hospitali moja kwa moja. Mimi na mwenzangu kila mtu alikwenda kwake,” alisema Mlekano. Baada ya hapo Mlekano alisema alienda kutoa taarifa kituo cha Polisi cha Mwongozo na kupatiwa fomu ya matibabu.
 
Pia analalamika kupoteza kadi ya bima ya afya, leseni ya gari pamoja na kiasi cha fedha. Godfrey Mchari kwa upande alisema alitumwa dukani na mama yake kwenda kutuma pesa dukani kwa wakala wa M-pesa na kabla hajafika alikutana na wanajeshi waliomwamrisha akae chini na ndipo yeye akaamua kukimbia.
 
Akijibu tuhuma hizo pamoja na hatua zilizochukuliwa na Jeshi kufuatia kadhia hiyo, msemaji wa jeshi Meja Joseph Masanja alisema taarifa hiyo bado haijawafikia na kuahidi atafuatilia jambo hilo ikiwa ni pamoja na kuonana na walalamikaji ili kulipatia ufumbuzi na ufafanuzi zaidi.
 
“Hizo taarifa bado hazijatufikia na nashukuru kwa kunipa taarifa hii, tutafuatilia na kutoa taarifa kamili wiki ijayo” alisema Masanja

Post a Comment

أحدث أقدم