Sakata
la mgomo wa wafanyakazi 1,500 wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia
(TAZARA), ulioingia katika siku ya sita, limechukua sura mpya baada ya
wafanyakazi hao waliofunguliwa kesi katika Mahakama ya Kazi, kusota kwa
siku nzima wakisubiri hukumu yao.
Kesi
hiyo ilianza kusikilizwa na Jaji Iman Aboud wa mahakama hiyo saa 3:30
asubuhi hadi 6 mchana jana na kisha kuaihirishwa hadi saa 8 mchana,
ambapo ilitarajiwa ingetolewa hukumu.
Akizungumza
na Mpekuzi, Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli (TRAWU)
Kanda ya Dar es Salaam, Yassin Mleke alisema Jaji Iman Aboud
anayesikiliza kesi hiyo tangu alipotoka saa 6 mchana hakurejea hadi saa
12:00 jioni wakati alipozungumza na Mpekuzi kwa njia ya simu. Alisema
hatua ya jaji huyo, kuchelewa kurejea, ilisababisha wao kushindwa kujua
kama kuna majadiliano ya hukumu yanayoendelea au la.
Hadi Mpekuzi anaondoka eneo hilo, wafanyakazi hao walikuwa bado mahakamani hapo wakisubiri kutolewa kwa hukumu hiyo.
Alipoulizwa
kuhusu msimamo wao, Mleke alisema msimamo wao ni kutorejea kazini hata
kama hukumu itakayotoka, itawataka kurejea kazini.
“Yaani
hata itoke hukumu ya aina gani, msimamo wetu uko pale pale, haturudi
kazini hadi tutakapolipwa mishahara yote ya miezi mitano na sio hivyo
tu, pia kuonana na Waziri (Dk Harrison Mwakyembe) ili kujua hatima ya
Tazara ili tuweze kumaliza haya matatizo ya migomo,” alisema Mleke.
Madai
yaliyowasilishwa na menejimenti hiyo katika Mahakama ya Kazi ni kuiomba
mahakama hiyo, kubatilisha mgomo huo na kuwataka wafanyakazi hao 1,500
kurudi kazini kwa madai mgomo huo ni batili kwani haukufuata sheria.
Aidha,
mgomo unaoendelea unalenga kushinikiza kulipwa kwa mishahara yao na
kutaka kukutana na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harisson Mwakyembe kwa ajili
ya kujadili hatma ya Tazara.
Mgomo
huo umesababisha athari kwa watumiaji wa usafiri huo wa treni za
mamlaka hiyo, hali iliyosababisha Jumanne wiki hii uongozi kurudisha
nauli za abiria, waliokuwa wakitarajia kusafiri kati ya Dar es Salaam na
Tunduma mkoani Mbeya.
Lakini,
pia mgomo huo umeathiri wasafiri wa Jiji la Dar es Salaam wanaosafiri
na treni ndogo kutoka stesheni ya Tazara hadi Pugu Mwakanga, nje kidogo
ya jiji.
Post a Comment