Wafanyakazi TAZARA Wasota Mahakamani kusubiri Hukumu


Sakata la mgomo wa wafanyakazi 1,500 wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia  (TAZARA), ulioingia katika siku ya sita, limechukua sura mpya baada ya wafanyakazi hao waliofunguliwa kesi katika Mahakama ya Kazi, kusota kwa siku nzima wakisubiri hukumu yao.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa na Jaji Iman Aboud wa mahakama hiyo saa 3:30 asubuhi hadi 6 mchana jana na kisha kuaihirishwa hadi saa 8 mchana, ambapo ilitarajiwa ingetolewa  hukumu.
 
Akizungumza na Mpekuzi, Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli (TRAWU) Kanda ya Dar es Salaam, Yassin Mleke alisema Jaji Iman Aboud  anayesikiliza kesi hiyo tangu alipotoka  saa 6 mchana hakurejea hadi saa 12:00 jioni wakati alipozungumza na Mpekuzi kwa njia ya simu. Alisema hatua ya jaji huyo, kuchelewa kurejea, ilisababisha wao kushindwa kujua kama kuna majadiliano ya hukumu yanayoendelea au la.
 
Hadi Mpekuzi anaondoka eneo hilo, wafanyakazi hao walikuwa bado mahakamani hapo wakisubiri kutolewa kwa hukumu hiyo.
 
Alipoulizwa kuhusu msimamo wao, Mleke alisema msimamo wao ni kutorejea kazini hata kama hukumu itakayotoka, itawataka kurejea kazini.
 
“Yaani hata itoke hukumu ya aina gani, msimamo wetu uko pale pale, haturudi kazini hadi tutakapolipwa mishahara yote ya miezi mitano na sio hivyo tu, pia kuonana na Waziri (Dk Harrison Mwakyembe) ili kujua hatima ya Tazara ili tuweze kumaliza haya matatizo ya migomo,” alisema Mleke.
 
Madai yaliyowasilishwa na menejimenti hiyo katika Mahakama ya Kazi ni kuiomba mahakama hiyo, kubatilisha mgomo huo na kuwataka wafanyakazi hao 1,500 kurudi kazini kwa madai mgomo huo ni batili kwani haukufuata sheria.
 
Aidha, mgomo unaoendelea unalenga kushinikiza kulipwa kwa mishahara yao na kutaka kukutana na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harisson Mwakyembe kwa ajili ya kujadili hatma ya Tazara.
 
Mgomo huo umesababisha athari kwa watumiaji wa usafiri huo wa treni za mamlaka hiyo, hali iliyosababisha Jumanne wiki hii uongozi kurudisha nauli za abiria, waliokuwa wakitarajia kusafiri kati ya Dar es Salaam na Tunduma mkoani Mbeya.
 
Lakini, pia mgomo huo umeathiri wasafiri wa Jiji la Dar es Salaam wanaosafiri na  treni ndogo kutoka stesheni ya Tazara hadi Pugu Mwakanga, nje kidogo ya jiji.

Post a Comment

أحدث أقدم